Mawaziri wakutana kujadili wanariadha michezo Madola

Muktasari:

Mawaziri hao walikutana faragha kutafuta namna bora ya kuhakikisha nyota hao wanashiriki michezo ya Madola nchini Australia.

Dar es Salaam. Kuondolewa wanariadha tisa kwenye timu ya Taifa ya Madola kumewakutanisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na mwenzake wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi.

Mawaziri hao walikutana faragha kutafuta namna bora ya kuhakikisha nyota hao wanashiriki michezo ya Madola nchini Australia.

JKT iliwaondoa wanariadha hao kwenye kambi ya timu ya Taifa na kuwapeleka katika mafunzo maalum ya kijeshi.

Wanariadha hao walikuwa wakijiandaa na michezo ya Madola, mbio za dunia nusu marathoni (kilomita 21) zilizopangwa kufanyika Machi 22 nchini Hispania na London marathoni zitakazofanyika Aprili 24, Uingereza.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday, alisema ana taarifa baadhi ya wanariadha Emnanuel Giniki, Fabiano Joseph, Alphonce Simbu na Magdalena Shauri wana majukumu mengine ya kikazi.

Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Yusuph Singo alisema suala la wanariadha hao kushiriki au kutokushiriki litajulikana muda mfupi ujao.

“Waziri (Dk Mwakyembe) alikuwa na mazungumzo na Waziri wa Ulinzi (Dk Mwinyi) juu ya suala hilo, tunategemea ndani ya siku mbili tutapata mwafaka na wenzetu wa Jeshi,”alisema Singo.

Kuondolewa wanariadha hao kuliripotiwa mara ya kwanza na gazeti hili na siku chache baadaye, Mkuu wa Majeshi, Venance Mabeyo alisema wamepelekwa kwenye mafunzo.

Juzi Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema Tanzania itawakilishwa na wanamichezo 19 na viongozi 12.

Katika riadha Tanzania itawakilishwa na Emmanuel Giniki, Augostino Sulle, Said Makula, Failuna Abdi, Magdalena Shauri, Stephano Huche, Sarah Ramadhan, Ally Gulam, Anthony Mwanga na makocha Lwiza John na Zakaria Barie.

Kwa upande wa ngumi ni mabondia Kassim Mbutike, Selemani Kidunda, Ezra Paul, Haruna Swanga na kocha Benjamin Oyombo.

Kuogelea ni Hilal Hilal, Sonia Tumiotto na kocha Khalid Lushaka. Mpira wa Meza ni Amon Tumaini, Masoud Mtalaso, Neema Mwaisyula, Fathiya Pazi na kocha ni Ramadhani Selemani.

Viongozi watakaokuwa kwenye msafara wa timu hiyo ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza, Nasra Mohammed, Joakim Mshanga, Gullam Rashid, Petro Kivike, Singo na Bayi.