Maveterani kukinukisha Kirumba na Nyamagana

Mwanza.Timu 14 zinatarajia kuwasha moto jijini hapa kwenye bonanza la Maveterani kutoka Afrika Mashariki na Kati yatakayodumu kwa siku mbili kuanzia leo Jumamosi hadi kesho Jumapili.

Mashindano hayo ambayo ni msimu wa tatu tangu kuanza kwake mwaka 2015 nchini Rwanda,kwa sasa bingwa mtetezi ni Uganda ambaye alitwaa ubingwa akiwa nchini kwake mwak jana.

 

 Mwaka huu Tanzania ndio mwenyeji wa michuano hiyo,ambayo itawakilishwa na timu tisa ikiwani za Wanaume tatu,ambazo ni Mabibo Veteran,Mwanza Veteran na Rock City Veteran kwa mchezo wa soka na sita za Wanawake ambapo nne ni kutoka Mwanza,huku Geita na Shinyanga zikiwakilishwa na timu moja moja kwa mchezo wa Netiboli .

Mwenyekiti wa Mwanza Veteran ambao ndio wasimamizi wa mashindano hayo,Bellen Rugina alisema kuwa tayari timu zote zimeshathibitisha ushiriki wake na kwamba wamejipanga kuwakilisha vyema nchi.

 

Alisema kuwa nchi ambazo zinashiriki ni DRC Kongo,Uganda,Rwanda,Burundi na Tanzania ambao ndio wenyeji na kwamba viwanja vya Nyamagana na CCM Kirumba ndivyo vitatumika.

“Nchi ya DRC Kongo na Burundi zitakuwa na timu moja moja,lakini Uganda na Rwanda zitakuwa na timu mbili kila uapande na sisi wenyeji (Tanzania) tutakuwa na timu tisa”alisema Rugina.

 

 

 

Alisema kuwa lengo kubwa la mashindano hayo ni kujenga mahusiano kwa mataifa hayo na kwamba zawadi kwa washindi zitakuwapo na kuwaomba wadau wa soka kujitokeza kushuhudia uwezo wa wachezaji wa zamani.