Mastraika waikwamisha Singida

Muktasari:

Singida ilikosa mabao matano ya wazi kwenye mchezo huo dhidi ya Ndanda, ikiwa ni mwendelezo wa ubovu wa safu yake ya ushambuliaji ambapo mpaka sasa hakuna straika hata mmoja wa timu hiyo aliyeweza kufikisha mabao matano.

SINGIDA United imeporomoka hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, baada ya kusuluhu na Ndanda huku sababu kubwa ya anguko hilo ikitajwa kuwa ni ubutu wa washambuliaji.

Singida ilikosa mabao matano ya wazi kwenye mchezo huo dhidi ya Ndanda, ikiwa ni mwendelezo wa ubovu wa safu yake ya ushambuliaji ambapo mpaka sasa hakuna straika hata mmoja wa timu hiyo aliyeweza kufikisha mabao matano.

Kocha Msaidizi wa Singida, Jumanne Chale alisema msimu huu walifanya usajili mara mbili na kusajili washambuliaji kadhaa wa kigeni, lakini wameshindwa kabisa kuwa msaada klabuni hapo.

Alisema Singida ina malengo ya kufanya vizuri msimu huu na kumaliza nafasi za juu, lakini safu yao ya ushambuliaji inawaangusha mno kwani, wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi za kufunga ila wanashindwa kufanya hivyo.

“Tatizo letu kubwa msimu huu ni kufunga, lakini timu inacheza vizuri kwenye maeneo yote,” alisema Chale na kuongeza: “Matokeo si mazuri kama tulivyotarajia hapo awali, lakini malengo yetu ya kumaliza katika nafasi za juu yapo pale pale.

“Katika usajili ambao tutafanya kuelekea msimu ujao tutaangalia mastraika wenye uwezo kama Emmanuel Okwi na Obrey Chirwa ili kurahisisha kazi ya kufunga.”