RT yalia JKT kuwaondoa wanariadha wake kambini

Tuesday February 13 2018

 

By Imani Makongoro,Yohana Challe

Dar es Salaam.Ndoto ya Tanzania kupata medali katika michezo ya Jumuiya ya Madola, mashindano ya nusu marathoni pamoja London marathoni imeingia doa baada ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuwaondoa wanariadha tisa katika kikosi cha timu ya taifa.
Wanariadha waliondolewa kambini na JKT ni pamoja na Emmanuel Giniki, Joseph Panga na Magdalena Shauri waliokuwa kwenye timu ya Madola, wengine ni Faraja Lazaro, Fabian Joseph, Sesilia Ginoka, Mayselina Mbua, Angelina Tsere waliokuwa wakijiandaa na Mashindano ya Dunia ya Nusu Marathon na Alphonce Simbu aliyekuwa ashiriki London Marathon.
Akizungumzia uamuzi huo wa JKT, katibu mkuu wa Shirikisho la riadha Tanzania (RT),Wilhelim Gidabuday alisema wamekata tamaa ya kuiletea nchi medali katika mashindano hayo.
Katibu huyo wa RT alisema wanariadha hao waliondolewa kambini Sakina  jijini Arusha mwishoni mwa wiki wakijianda mashindano hayo.
Michezo ya madola itaanza Aprili 4 mpaka 15 nchini Australia wakati ile ya dunia itafanyika Machi 24 nchini  Hispania.
"Wanariadha wote tisa ni waajiliwa wa JKT, RT iliwaombea ruhusa tangu Desemba, lakini baadae tumeambiwa ruhusa yao haipo tena kwa kuwa wanamajukumu mengine, hivyo hatuna uhakika kama tutakuwa nao," alisema Gidabuday.
"Wanariadha hao ndiyo tegemeo la timu yetu kwani wote wamefikia viwango, kukosekana kwao basi tusitarajie medali ya riadha," alisema Katibu wa RT.
Alisema kama msimamo wa JKT utaendelea hivyo basi Watanzania wasitegemee chochote kutoka kwa wanariadha na kuna uwezekano mkubwa wa kuvunjwa kwa kambi hiyo katika siku chache zijazo.
“Nasikitishwa na kitendo cha kutembezwa gizani kwa kuwa wao wametuambia wanariadha hao wamepangiwa kazi nyingine yaani inaonekana kukanusha barua ya awali ambayo iliwaruhusu wanariadha hao.”
“Wanatakiwa kuangalia mifano ya nyuma ya kina Filbert Bayi na Juma Ikangaa aliupata Ukanali akiwa bado mwanariadha na alikuwa anaruhusiwa kwenda kuiwakilisha nchi kwenye mashindano mengi makubwa, lakini kwanini hawa wasipewe ruhusa?” alihoji Gidabuday.
 Gidabuday alisema kuwa hadi sasa hajui hatma ya wanariadha hao na watauelezaje umma juu ya maandalizi ambayo waliyaandaa tangu awali kwao huku siku chache zilizopita walitumia mamilioni ya fedha kwaajili ya kambi hiyo.
Aliongeza endapo wanariadha hao watakuwa wamewapeleka kwenye mazoezi magumu ya Kijeshi itakuwa wanawaumiza na kushindwa kuwa tayari kwa  mashindano hayo.
“Nimejaribu kuliwasilisha kwa Mkurugenzi wa Wizara ya Michezo, Yusuph Singo ambaye ni mkuu wa msafara wa Timu ya Jumuiya ya Madola mwaka huu, lakini naona mafanikio ya kupata ni kidogo mno hadi sasa.”
Mkurugenzi wa maendeleo ya Michezo Nchini, Yusuf Singo aikiri kuwa na taarifa za wanariadha hao kutokuwepo kwenye timu na amesisitiza kulihughulikia suala hilo.