Mashaga, Lwakatare kusuka au kunyoa BFT

Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la ndondi za ridhaa (BFT), Muta Lwakatare na katibu mkuu, Makore Mashaga kesho ni siku kuamua hatma yao katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo utakaofanyika mjini Dodoma.

Rais anayemaliza muda wake Lwakatare anatetea nafasi yake wakati Mashaga anagombea nafasi ya makamu wa rais pamoja na Andrew Mhoja aliyewahi kuwa mlezi wa klabu ya ngumi ya JKT.

Jana wagombea hao walishiriki kwenye zoezi la usaili lililoongozwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohamed Kiganja huku habari za ndani zikibainisha kuwa kuna uwezekano, vigogo wote wanaotetea nafasi zao BFT kuondoshwa katika usaili.

Habari zaidi zilifafanua kuwa, kuporomoka kwa masumbwi ya ridhaa nchini kinatajwa kuwa kipimo cha kutowapa nafasi nyingine Mashaga na Lwakatare kugombea kwenye uchaguzi huo.

"Mpango uliopo ni kuiondoa kamati yote ya utendaji inayomaliza muda wake kwa kuwa kwenye kipindi cha miaka minne walichokaa madarakani, ngumi zimeshuka," alidokeza mmoja wa wajumbe wa kamati ya uchaguzi huo.

Hata hivyo, Kiganja alitarajiwa kutangaza matokeo ya usaili leo jioni, lakini pia habari zaidi zilifafanua kuwa kuna uwezekano wa BMT kuteua viongozi wa mpito kwa mujibu wa mamlaka iliyopewa kikanuni.

"Kama wataondoshwa kwenye usaili basi BMT itateua viongozi wa mpito na itaitisha uchaguzi mwingine ndani ya miezi mitatu kuanzia leo," alisema mjumbe huyo wa kamati ya uchaguzi.

Lwakatare alijitosa kutetea nafasi yake akichuana na Samwel Sumwa, wakati Mashaga ambaye namaliza kipindi chake cha ukatibu anachuana na Mhoja katika nafasi ya makamu wa rais.

Makamu wa rais anayemaliza muda wake, Lukelo Wililo amejitosa kuwania ukatibu mkuu akichuana na mjumbe wa kamati tendaji anayomaliza muda wake, Anthony Mwang'onda.

Nafasi za ujumbe  zinawania na Scolastika Kevela, Yono Kevela, Zainabu Mbonde, Suzane Masawe, Potipoti Ndanga, Aisha Voniatis, Riadha Iddi na Donatha Masawe.