Mashabiki wavamia mazoezi Yanga Songea

Muktasari:

Yanga ipo Songea ikijiandaa na mechi yake ya Kombe la FA dhidi ya Majimaji itakayochezwa kesho

Songea. Mashabiki wa Yanga wamezua tafrani kwenye Uwanja wa Majimaji Mjini Songea baada ya 'mabaunsa' wa timu hiyo kuwazuia kuingia uwanjani ili kushuhudia mazoezi ya wachezaji wao.

Wachezaji wa Yanga waliingia uwanjani hapo kufanya mazoezi yao saa 11:15 jioni ikiwa ni masaa machache tangu watue mjini hapa wakitokea Jijini Dar es salaam kwa ajili ya mechi yao ya Kombe la FA dhidi ya Maji Maji 'Wanalizombe'.

Baada wachezaji hao kuingia uwanjani wakitumia basi lao, mashabiki waliokuwa wamefurika nje ya uwanja walivamia geti kuu wakitaka kuingia lakini mabaunsa waikuwa imara zaidi na walifanikiwa kuwazuia kwa muda.

Hata hivyo, mashabiki waliendelea kupiga kelele nje ya geti hilo wakisema 'tunataka kuwaona wachezaji wetu, kwani ni timu yetu.... Turuhusini tuingie...'.

Kutokana na kelele za mashabiki hao, viongozi wa timu waliokuwa ndani ya uwanja walishauriana na wakafikia mwafaka wa kuwaruhusu mashabiki hao kuingia uwanjani.

Mazoezi ya Yanga yalidumu kwa takribani dakika 60 kisha wakarejea hotelin walikofikia.