Mao, Junior waacha pengo Azam

Muktasari:

Mao amekosa mechi nne ziliopita za Azam akiwa Afrika Kusini katika Hospitali ya Vincent Pallotti kwa ajili ya uchunguzi wa goti la mguu wake wa kulia linalomsumbua kwa muda mrefu.

Dar es Salaam. Nahodha na kiungo wa Azam, Himid Mao atakaa nje ya uwanja kwa wiki tatu akiuguza majerahi yake ya goti.

Mao amekosa mechi nne ziliopita za Azam akiwa Afrika Kusini katika Hospitali ya Vincent Pallotti kwa ajili ya uchunguzi wa goti la mguu wake wa kulia linalomsumbua kwa muda mrefu.

Mao ataikosa mechi ya Azam dhidi ya Singida United, Mwadui na Mbao pamoja na mechi za Kombe la FA dhidi ya KMC zitakazochezwa katika kipindi hicho.

Afisa Habari wa Azam, Jaffar Iddy alisema tayari Himid amefanyiwa uchunguzi na kugundulika kuwa na damu iliyovilia katika goti lake.

"Ameshafanyiwa uchunguzi na ripoti ya daktari imesema kuwa kuna damu imevilia kwenye goti na ndio inasababisha apate maumivu makali.

"Kutokana na ripoti hiyo hatafanyiwa upasuaji bali kuna dawa amepewa atumie kwa wiki tatu na atakuwa tayari kurejea uwanjani"alisema Iddy.

Wakati huo huo; mshambuliaji wa timu hiyo Wazir Junior anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mdogo wa mguu katika hospitali ya Muhimbili kitengo cha mifupa (Moi)baada ya donge la damu kuvilia chini ya mguu.

Daktari wa Azam, Mwanandi Mwankemwa alisema,"Junior alikuwa na tatizo kwenye kifundo cha mguu na tumemfanyia vipimo vyote vya M.R.I, X-Ray na alikuwa akitibiwa Moi sasa hivi taratibu zinafanyika ili afanyiwe matibabu zaidi ambapo atafanyiwa upasuaji mdogo baada ya kujulikana kuwa chini ya mguu kuna bonge la damu.