Manji awatia kiburi Yanga

Muktasari:

  • Yanga imeapa kufa na Simba inayoongoza msimamo kwa sasa kwa tofauti ya pointi tano, ikiwa na alama 54 dhidi ya 49 ya vijana hao wa Jangwani, huku Kocha Msaidizi Juma Mwambusi akitamba kuwa mapambano yanaendelea.

KIPIGO cha mabao 2-1 ilichopewa Yanga ikiwa ni cha kwanza kutoka kwa Simba tangu Emmanuel Okwi alipowalaza mapema Machi 8, 2015 ikiwa ni miaka miwili kasoro siku 17 tu, kimewafanya waliweke rehani taji lao la Ligi Kuu Bara.

Lakini kiu ya kutaka kumfariji Mwenyekiti wao, Yusuf Manji aliyepo kwenye  misukosuko kwa sasa, imelifanya benchi la ufundi na wachezaji wa klabu hiyo kupata kiburi na kuapa kupambana mpaka dakika za mwisho za msimu huu.

Yanga imeapa kufa na Simba inayoongoza msimamo kwa sasa kwa tofauti ya pointi tano, ikiwa na alama 54 dhidi ya 49 ya vijana hao wa Jangwani, huku Kocha Msaidizi Juma Mwambusi akitamba kuwa mapambano yanaendelea.

Mwambusi alisema pamoja na kwamba wamepoteza kwa Simba, hawana wasiwasi kwani wapinzani wao hao walishafikisha wigo wa pointi nane na wakazipunguza hadi zikamalizika hivyo pointi hizo tano si kitu kwa Yanga.

“Bado tuna uwezo wa kurejea tena kileleni, Simba walishaweka wigo mkubwa zaidi ya huu wa sasa na tukafanikiwa kuupunguza. Nadhani kikubwa ni kujipanga upya, hatujakata tamaa,” alisema Mwambusi.

“Unapofungwa mchezo mmoja si sababu ya kupoteza michezo mingine, tukitoka hapa tunaenda kujipanga kwa mchezo mwingine.”

Nao baadhi ya nyota wa klabu hiyo, walisema wamedhamiria kuhakikisha wanashinda mechi zao zilizosalia ili kulitetea taji lao iwe kama faraja kwa Mwenyekiti wao anayekabiliwa na tuhuma za kutumia dawa za kulevya na kuajiri wageni wasio na vibali vya kufanyia kazi nchini.

“Tumehuzunishwa kupoteza pambano hili, lakini hatujakata tamaa tutapigana hadi mwisho ili kuona tunabeba tena taji kumfariji Mwenyekiti wetu, hatukutegemea kupoteza kwa Simba, ila wasijidanganye, tunao,” alisema moja ya nyota wa klabu hiyo ambaye hakupenda kuandikwa gazetini.

Hata hivyo, Kocha Mwambusi akizungumzia sababu zilizopelekea kupoteza mchezo huo, alisema kuumia kwa kiungo wao Thabani Kamusoko kulitibua mipango yao kwani kiungo aliyeingia, Said Juma ‘Makapu’ hakuweza kwenda na kasi ya mchezo.

“Ukitazama mchezo hadi mapumziko tulikuwa tumeukamata lakini baada ya kuumia kwa Kamusoko tulishindwa kuwa na kasi ile tena. Kama unavyofahamu Kamusoko ni kiungo Mwandamizi ndani ya timu hivyo kushindwa kuendelea kwake kulitugharimu.

“Simba walibana pia uwanja katika kipindi cha pili na kutufanya tutegemee zaidi mashambulizi ya pembeni ambayo hayakuzaa matunda, hizo ndizo sababu kubwa,” alisema Mwambusi.

Lwandamina atema wanne

Achana na Donald Ngoma ambaye sakata lake bado linaendelea kujadiliwa Jangwani, ukweli ni kwamba Kocha Mkuu wa timu hiyo, George Lwandamina ni kama ameondoa kikosini mwake wachezaji wanne katika mipango yake ya sasa.

Lwandamina aliyeshuhudia vijana wake wakipoteza mechi ya pili mfululizo dhidi ya Yanga ndani ya mwezi mmoja na ushei, ameacha kuwatumia wachezaji hao ambao angalau walikuwa wakipata dakika chache enzi za Hans Pluijm.

Ni hivi. Mzambia huyo amewatosa kimoja, kipa Beno Kakolanya, beki Pato Ngonyani na straika Malimi Busungu ambao hawajacheza kabisa chini yake.

Mchezaji mwingine ambaye amecheza kwa dakika 10 katika utawala wa kocha huyo ni straika Matteo Antony na ilikuwa katika mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Ashanti United na tangu hapo hajabahatika kucheza tena.

Kutokutumika kwa wachezaji hao ni wazi kuwa wako njiapanda kuendelea kucheza Yanga kwani mikataba ya Matteo, Busungu na Pato inaelekea ukingoni huku Kakolanya akishindwa kabisa hata kuwa chaguo la pili.

Wachezaji wengine ambao wamekuwa na nafasi finyu katika kikosi cha kwanza ni; mabeki Hassan Kessy na Oscar Joshua, Geofrey Mwashiuya na chipukizi Yusuf Mhilu.