Man United hivi mmemsikia Mane?

LIVERPOOL, ENGLAND. STAA wa Liverpool, Sadio Mane amewachimba mkwara Manchester United akiwaambia kwamba Liverpool ya sasa ipo moto na yeyote atakayekatiza mbele ni kipigo tu.
Liverpool itakwenda kuifuata Man United huko Old Trafford Jumamosi hii kwenye mchezo wa Ligi Kuu England na kwamba haitakuwa na presha kwani tayari imeshatinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Wababe hao wanaonolewa na Jurgen Klopp wamepoteza mechi moja tu kwenye Ligi Kuu England tangu mwaka huu uenza na hilo linamfanya Mane kuwa na uhakika kwamba watakwenda kutoa kipigo kwa mahasimu wao hao. Kwenye mechi sita za mwisho ilizocheza kwenye ligi, Liverpool imeshinda tano na kutoka sare moja tu.
Juzi Jumanne ilichezesha kikosi dhaifu kabisa kwenye mechi ya marudiano dhidi ya FC Porto iliyomalizika kwa sare ya bila mabao, hasa baada ya kushinda mechi ya kwanza iliyofanyika Ureno kwa mabao 5-0. Lakini, kwenye mechi hiyo ya Old Trafford, mastaa wote wa timu hiyo wakiwamo wale watatu wanaounda safu ya ushambuliaji; Mohamed Salah, Roberto Firmino na Mane, wote wataanzishwa.
“Haitakuwa mechi rahisi, lakini siku zote nimekuwa nikisema Liverpool ya sasa inaweza kuifunga timu yoyote duniani,” alisema Mane.
“Wao Manchester United ni timu nzuri England na hata duniani, lakini kama ilivyo kwetu pia. Ni ndoto za kila mmoja kucheza mechi za aina hii.”