Majimaji yajipanga kuiduwaza Azam

Muktasari:

Timu hiyo ya Songea ipo nafasi 13 katika msimamo hivyo kujiweka katika mazingira mabaya ya kushuka daraja

Mbeya. Kocha wa Majimaji, Peter Mhina amesema kikosi chake kipo tayari kuivaa Azam Fc katika mchezo utakaochezwa Alhamisi Januari 18, kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Kocha Mhina alisema wanaiheshimu Azam fc kutokana na mafanikio yao katika ligi, lakini dakika 90, ndizo zitakazoamua mchezo huo.

“Tunaendelea na mazoezi kwaajili ya mechi zetu mbili zinazokuja, lakini haswa ni hii inayochezwa Alhamisi, tumejipanga kwaajili ya kuchukua pointi tatu dhidi ya mabingwa  wa Kombe la Mapinduzi.”

Mhina alisema kufungwa mechi mbili mfululizo kumewapa somo la kurekebisha makosa yaliyoonekana na kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu kwa kila mechi.

“Ingawa nimeichukua timu hii baadaye, lakini kadri siku zinavyozidi kwenda wachezaji wanazidi kuzoea mfumo wangu na mbinu zangu, kwa hiyo ni imani yangu kwamba hawataniangusha siku hiyo.’’