Maguli atoa somo kuendeleza vipaji

Muktasari:

Asema chipukizi ambao wana vipaji vya hali ya juu kama Yohana Mkomola wanatakiwa kuendelezwa vyema ili waweze kufika mbali.

NYOTA wa zamani wa Simba na Stand United 'Chama la Wana', Elias Maguli ambaye kwa sasa hana timu, amesema hayupo nyuma kuifutilia Ligi Kuu, ili aweze kujifunza vitu vya kiufundi.

Maguli anasema kwa mchezaji mwenye ndoto za kufika mbali haachi kujifunza katika ligi yake ya ndani na nje, akiamini akifanya hivyo anaweza akabaini kiwango chake anapaswa kukiboresha wapi.

"Ukikubali kujifunza, unakuwa umekubali kupiga hatua mbele, nje na kuangalia mechi zinazoendelea pia nina programu maalum ya mazoezi ili kuufanya mwili wangu uwe tayari kwa kazi,"

Kuhusu mipango yake ya atacheza wapi! Anajibu "Zipo timu ndani na nje, ila baada ya kumalizika kwa ligi lolote linaweza kutokea ndio maana nafuatilia kila kitu kwa ukaribu," anasema.

Pia amekiri kwamba katika Ligi Kuu, kuna chipukizi ambao wana vipaji vya hali ya juu kama Yohana Mkomola ambao wanatakiwa kuendelezwa vema ili waweze kufika mbali.

"Tanzania kuna vipaji, ili vifike mbali lazima viwekewe misingi ya mwendelezo na kuvijengea uzoefu wa namna ya kufikia malengo yao na kuwa msaada kwenye kikosi cha Taifa Stars," anasema.