MAKALA: Singida inaacha maswali mengi Simba

KUNA stori mbili za kusisimua katika msimu huu wa mashindano. Kuna stori ya Singida United halafu kuna ile ya Simba. Zote za Ligi Kuu Bara.

Timu hizo mbili zilifanya kitu kinachofanana mwanzoni mwa msimu. Singida iliingia sokoni na kununua mastaa kibao, kama vile Simba walivyofanya. Singida ilinunua mastaa saba wa kigeni ambao wanacheza katika timu zao za Taifa. Shafiq Batambuze (Uganda), Michael Rusheshangoga na Danny Usengimana (Rwanda), Elisha Muroiwa, Tafadzwa Kutinyu, Nhivi Simbarashe na Michelle Katsvairo (Zimbabwe). Pia ilisajili mastaa wengine wakubwa wa Ligi Kuu kama Deus Kaseke (Yanga), Kenny Ally (Mbeya City), Mudathir Yahya (Azam) na wengineo.

Mwisho wa yote ikampa ajira Kocha Mdachi, Hans Van Pluijm ambaye ana rekodi ya kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, moja la FA na Ngao ya Hisani.

Stori yao haitofautiani na ile ya Simba hata kidogo. Simba nayo iliingia sokoni ikasajili mastaa wa kutosha. Ilikwenda nje na kuwaleta Emmanuel Okwi na Nicholas Gyan. Ikawasajili Haruna Niyonzima, John Bocco, Shomary Kapombe na wengineo. Ilisajili wachezaji wengi wa maana.

Bila kupepesa macho, Simba ilifanya usajili mkubwa zaidi Ligi Kuu. Ofisa Habari wao, Haji Manara huwa anasema ni usajili wa Sh1.3 bilioni. Usajili wa kutisha.

Pamoja na yote bado Simba ilikuwa na faida kuliko Singida. Mbali na kufanya usajili mkubwa, Simba bado ilikuwa na mastaa wakubwa kama Mzamiru Yassin, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, James Kotei na wengineo.

Singida haikuwa na mastaa hapo kabla. Ilikuwa ndio kwanza imepanda daraja. Wachezaji wake wengi walikuwa na viwango vya kawaida hivyo ilihitaji maboresho. Ni tofauti na Simba iliyokuwa imetoka kutwaa taji la FA na kumaliza nafasi ya pili tena kwa tofauti tu ya mabao.

Matarajio yalikuwa msimu huu Simba ingekuwa haikamatiki. Ingezifunga timu zote zikiwemo Yanga na Azam FC. Simba ilikuwa imefanya usajili mkubwa wa kuwawezesha kufanya hivyo. Nini kimetokea?

Ni kweli Simba inaongoza Ligi Kuu Bara. Ila ni kwa wastani mzuri tu wa mabao ya kufunga na kufungwa. Tena mabao mengi iliyafunga kwenye mechi ya Ruvu Shooting waliyoshinda 7-0. Mechi nyingine zilikuwa kawaida tu.

Kwenye Kombe la FA tayari wamevuliwa ubingwa na timu ndogo Green Warriors. Kwenye Kombe la Mapinduzi ndiyo kama mnavyoona. Simba imeshinda mechi moja tu katika tatu walizocheza. Inashangaza hawa wawakilishi wetu Kombe la Shirikisho Afrika.

Singida kwa upande wake, ilipoteza mchezo wa kwaza wa Ligi Kuu, Agosti 26, lakini tangu hapo hawajapoteza tena. Wameachwa pointi tatu tu na Simba inayoongoza Ligi.

Mbali na hilo, Singida inacheza soka safi na la kuvutia. Kwenye kombe la Mapinduzi haijapata sare hata mchezo mmoja. Imeshinda mechi zote nne tena kwa mabao mawili ama zaidi. Tena imekuwa ikicheza kila siku, haina muda wa kupumzika kama Simba.

Kwenye Kombe la FA imefuzu raundi inayofuata na imepangwa kucheza na Green Warriors iliyoifunga Simba. Kwa kifupi, mpaka kufikia hapa Singida imekuwa na kiwango bora kuliko Simba.

Pointi tatu walizoachwa kwenye ligi wanaweza kuzifikia, tena bila wasiwasi. Kwa sasa tayari wamecheza na Azam na Yanga bila kupoteza. Tena Yanga waliomba mpira umalizike mapema pale Namfua, Singida.

Ukifanya tathmini utaona wazi kabisa Singida imekuwa na kiwango bora kuliko Simba. Nini kimeipata Simba? Tathmini ya usajili inaonyesha Simba ina kikosi bora zaidi lakini uwanjani Singida inacheza soka la kuvutia zaidi. Mashabiki na viongozi wa Simba waliamini tatizo la awali lilikuwa Kocha Joseph Omog, wakamtimua. Vipi sasa, tatizo ni Masudi Djuma au wachezaji? Ukitazama kiuchezaji, kuna mahali Masudi anakosea, lakini kuna tatizo kubwa zaidi ndani ya Simba. Nidhamu ya mastaa wake siyo nzuri. Pia, wapo wachezaji wazuri ambao wameharibiwa kisaikolojia na benchi la ufundi ama viongozi wao.

Mohammed Ibrahim aliyekuwa akitandaza soka la kuvutia siyo huyu wa sasa. Mzamiru Yassin aliyekuwa akicheza kandanda safi siyo huyu wa sasa. Haruna Niyonzima, Laudit Mavugo ni kama hawapo kwenye timu.

Vipi kuhusu Emmanuel Okwi. Ni kweli ameumia, lakini kwa nini hataki kuungana na wachezaji wenzake apatiwe uangalizi akiwa kwenye timu? Kwa nini viongozi wamemruhusu awe msumbufu kiasi hiki? Naambiwa wakati Simba inajiandaa na mechi ya FA mwezi uliopita, baadhi ya wachezaji wake waligoma kufanya mazoezi ya penalti kwa madai wangemaliza mechi mapema. Nini kilitokea? Pia, mabadiliko yaliyoletwa na Masudi sasa yanaweza kuwashusha morali baadhi ya wachezaji wake. Unamchezeshaje Shiza Kichuya kama beki? Hata kama ni mfumo, siyo kwa mchezaji wa aina ya Kichuya.

Kichuya ndiye staa wa timu. Ndiye mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi tangu msimu uliopita. Anakuwa hatari sana akicheza mbele, hasa akitokea upande wa kulia. Kwa nini Masudi anawaharibu wachezaji wazuri?

Simba inatakiwa kuitazama Singida United na kujifunza kitu. Singida imesajili vizuri, inawaheshimu wachezaji wake na inafanya vizuri. Hakuna mtu mwenye maswali sasa kuhusu Singida. Na kwa namna Singida wanavyozidi kuimarika, ni wazi tutaendelea kupata maswali mengi kuhusu Simba.

Hakuna mashaka Kocha Hans Van Pluijm ndiye chachu ya soka safi la Singida kwa sasa. Vipi kuhusu Simba, kocha wao siyo mzuri?