Lwandamina: Yanga ushindi lazima Uwanja wa Taifa

Muktasari:

Yanga kwa sasa ipo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 22 ikiachwa kwa pointi saba na watani wao Simba.

Dar es Salaam.Kocha wa Yanga, George Lwandamina anajua ushindi pekee dhidi ya Ruvu Shooting leo Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, utapunguza hasira za mashabiki wake waliochukizwa na kiwango kibovu katika mchezo uliopita dhidi ya Mwadui.

Mashabiki wa Yanga walimvaa Katibu Mkuu wa Klabu hiyo, Charles Mkwasa baada ya mchezo kumalizika dhidi ya Mwadui na kumshinikiza kuondolewa kwa kocha msaidizi Shadrack Nsajigwa.

Mashabiki walikuwa wakihoji kiwango cha Yanga huku wakipata wasiwasi kwa kiwango kile timu hiyo kweli itafika mbali kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.

Yanga kwa sasa ipo nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 22 ikiachwa kwa pointi nane na watani wao Simba.

Lwandamina alikaa jukwaani wakati Yanga ikilazimishwa suluhu na Mwadui jambo linalofanya Mzambia huyo kuhakikisha wanapata ushindi dhidi ya Ruvu Shooting na kurudisha imani kwa mashabiki wake. Hata hivyo, Yanga itaendelea kuwakosa washambuliaji wake tegemeo katika mchezo huo Obrey Chirwa anatumikia adhabu ya kufungiwa mechi tatu, Donald Ngoma ni mgonjwa wakati Amissi Tambwe ameonekana bado hayuko fiti kutokana na kurejea taratibu akitokea katika majeraha.

Pia, Lwandamina ataendelea kuwakosa beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ na Geofrey Mwashiuya lakini kiungo Papy Tshishimbi atarejea baada ya kukosekana katika mchezo uliopita.

Mabingwa hao wanaingia uwanjani wakiwa na rekodi nzuri dhidi ya Ruvu Shooting kila mara timu hizo zinapokutana, lakini itatakiwa kucheza kufa au kupona leo kuhakikisha ushindi unapatikana.

Nsajigwa alisema wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanapata matokeo mazuri katika mchezo huo.

“Mchezo uliopita hatukupata matokeo mazuri, hivyo inabidi tujitahidi kushinda mchezo huu ili kujiweka pazuri kwenye msimamo wa ligi,”alisema Nsajigwa.

Naye kocha wa Ruvu Shooting, Abdulmutic Hadji alisema wamejiandaa kufuta rekodi mbaya kila wanapokutana na Yanga na watahakikisha leo wanaondoka na pointi tatu. “Nafurahi wachezaji wangu wawili ambao niliwakosa katika mechi zote zilizopita, mshambuliaji Fully Maganga na beki Damas Makwaya wamerejea naweza kuwatumia katika mchezo wa kesho (leo).

“Katika kikosi cha Yanga namuhofia Ibrahim Ajibu yeye ndio injini ya timu hiyo, anajua nini anafanya uwanjani hivyo tunapaswa kumchunga asilete madhara,” alisema Hadji.

Matokeo yoyote mabaya ya Yanga yanazidi kuwaweka pabaya kwa kuwa wapinzani wao katika mbio za ubingwa Simba wamerejea katika makali yao, baada ya kuichapa Singida United mabao 4-0 na kesho watakuwa Bukoba kucheza dhidi ya Kagera Sugar.

Azam inayoshika nafasi ya pili baada ya kulazimishwa sare 1-1 na Majimaji, leo watakuwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuwavaa Prisons.

Matokeo ya mechi za jana Mbao 0-1 Stand United, Mtibwa Sugar 0-0 Njombe Mji.