Liverpool, Man City mwisho wa enzi

Saturday January 13 2018

 

LIVERPOOL, ENGLAND. LIVERPOOL iliokota mipira mara tano kwenye wavu wao mara ya mwisho ilipokutana na Manchester City kwenye Ligi Kuu England, hivyo kesho Jumapili itakuwa nyumbani Anfield kusaka namna ya kulipa kisasi.

Walipigwa 5-0 kwenye mechi ya Etihad, ambayo walikuwa vizuri na kufungwa 1-0 tu kabla ya Sadio Mane hajaonyeshwa kadi nyekundu na kilichofuatia baada ya hapo ni mabao tu kumiminika kwenye goli la vijana hao wa Jurgen Klopp.

Lakini, safari hii Klopp atahitaji kulipa kisasi kufanya ligi hiyo kuwa kwenye upinzani mkali. Ukiweka kando kisasi, Liverpool itahitaji kushinda pia mechi hiyo ili kupunguza pengo dhidi ya Man City, ambao ni vinara wa ligi hiyo. Liverpool ina pointi 44 na Man City wao wana pointi 62.

Hakuna ubishi kwenye mechi hiyo  makocha wote vigogo kuanzia Jose Mourinho, Arsene Wenger, Antonio Conte na Mauricio Pochettino watakuwa upande wa Klopp dhidi ya Pep Guardiola ili kumpunguza spidi Mhispaniola huyo.

 Mourinho na Man United yake yupo nyuma kwa pointi 15 dhidi ya Man City ya Guardiola na yeye kibarua chake kitakuwa Jumatatu wakati atakapowakaribisha Stoke City huko Old Trafford.

Jambo hilo linafanya vita kuwa kali. Wenger na kikosi chake cha Arsenal naye atacheza kesho Jumapili akiwafuata Bournemouth kwao, huku Pochettino kibarua chake kikiwa leo kwa kukipiga na Everton huko Wembley.

 Ni bato la kukata na shoka kwenye Ligi Kuu England wikiendi hii wakati vigogo vitakapojaribu kupigana vikumbo. Man City wao bado hawajapoteza mechi yoyote kwenye ligi hiyo hadi sasa ikiwa imetoka sare mara mbili tu na kushinda mechi 20 katika 22 ilizocheza msimu huu.

Liverpool wameshikilia funguo ya kuwa timu ya kwanza kuwafunga Man City msimu huu itakapowakaribisha huko Anfield licha ya kwamba hawatakuwa na huduma ya staa wao, Philippe Coutinho, aliyetimkia Barcelona.

Kama rekodi ya City ya kutofungwa hatoharibika Anfield, zitabakia kushinda mechi 15 tu ili kujitangazia ubingwa mapema na huku wakiendelea kuisaka kuivunja rekodi ya Arsenal msimu wa 2003-04 na Preston msimu 1888-89, ndiyo timu pekee zilizotwaa ubingwa bila ya kufungwa msimu mzima.

"Ni wazi kama unataka kupata mafanikio mazuri na kutwaa ubingwa unatakiwa kushinda aina hii ya mechi," alisema Guardiola.

"Msimu huu kwenye Uwanja wa Stamford Bridge tulifanikiwa kushinda pale, lakini sasa tunakwenda Anfield, baadaye Emirates kabla ya kuivaa Tottenham.

"Bado tuna mechi ngumu ugenini, bado kuna mambo mengi ya kufanya. Kwetu sisi huu ni mtihani mgumu, kwenda kucheza Anfield, moja ya viwanja vizuri na kuna timu bora yenye sifa ya kucheza vizuri wakati wote, hii ni mechi kubwa kwetu.

"Mechi dhidi ya Liverpool ni muhimu kwetu, itakayotuonyesha kama kwetu tupo tayari kufanya jambo kubwa msimu huu, pia tupo katika hatua nzuri katika Ligi ya Mabingwa."

Tangu walipofungwa na Tottenham mwezi Oktoba 22, 2017, Liverpool haijafungwa katika mechi 17 za mashindano yote kati ya hizo mechi 13 ni za Ligi Kuu yakiwa ni mafanikio makubwa kwa kocha Jurgen Klopp.

Tangu walipofungwa 5-0 na City mwanzo wa msimu huu kikiwa ni kipigo kikubwa kwa Klopp tangu alipochukua jukumu la kuifundisha timu hiyo.

City wanakuja wakati Liverpool wakiwa na pengo la kuondoka kwa Philippe Coutinho aliyetimkia Barcelona.

"Ni jambo zuri kucheza dhidi ya City. Wanacheza soka la hali ya juu, kama hutoheshimu hilo utajikuta katika matatizo makubwa," alisema Klopp.

"Pia, kama haujabadilisha mbinu yako ya uchezaji, pia unaweza kujikuta katika matatizo. Unahitaji kujituma."