Kuna Tshishimbi, Ajibu presha ya nini?

Muktasari:

  • Yanga imekwenda visiwani humo kwa mchezo wao wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St Louis, ikiwa na kikosi cha wachezaji 19, huku nyota kadhaa akiwamo Chirwa na Dante walio na matatizo ya kiafya wakiachwa jijini Dar.

MASHABIKI wa Yanga wameshtuka kusikia kuwa straika wao mkali, Obrey Chirwa pamoja na beki wa kati, Andrew Vincent ‘Dante’ hayumo kwenye msafara wa kikosi cha timu hiyo kilichoondoka alfajiri ya leo kwenda Visiwa vya Shelisheli.

Yanga imekwenda visiwani humo kwa mchezo wao wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St Louis, ikiwa na kikosi cha wachezaji 19, huku nyota kadhaa akiwamo Chirwa na Dante walio na matatizo ya kiafya wakiachwa jijini Dar.

Hata hivyo, kwa kutambua presha kubwa waliyonayo mashabiki wa klabu hiyo, benchi la ufundi la timu hiyo limefanya jambo la maana baada ya kuangalia rekodi yao katika mechi za kimataifa wanazocheza ugenini.

Benchi hilo limeamua kuwapa jukumu la kuivusha Yanga katika raundi hiyo ya awali kiungo Kabamba Tshishimbi na straika Ibrahim Ajibu, wakisaidiwa na nyota wengine waliopaa leo kwa usafiri wa ndege.

REKODI ZILIVYO

Mwanaspoti limefukunyua kabrasha zake za mechi za kimataifa za ugenini za Yanga na kubaini kuwa, imekuwa ikichemka zaidi kuliko inapocheza nyumbani hasa zile za kuamua hatma yao kwani tangu mwaka 2010 wawakilishi wameponzwa na mechi za ugenini, ukiacha chache ilizoshinda hasa kwa timu za visiwani.

Rekodi zinaonyesha mwaka 2010 ilipoteza ugenini kwa FC Lupopo ya DR Congo kwa bao 1-0 baada ya awali kupigwa nyumbani mabao 3-2 na kung’olewa kwa 4-2.

Mwaka 2012 ilipoteza kwa Zamalek bao 1-0 ugenini baada ya sare ya 1-1 nyumbani na kuondolewa mashindanoni kabla ya kurejea tena mwaka 2014 kwa kulala 1-0 dhidi ya Al Ahly ya Misri baada ya awali kushinda nyumbani bao 1-0 na kutolewa kwa penalti 4-3.

Waarabu waliendelea kuwapoteza Yanga baada ya mwaka 2016, kuwafunga mabao 2-1 ugenini baada ya sare ya 1-1 nyumbani na hata mwaka jana tena Yanga ililazimishwa sare ya 0-0 baada ya sare ya 1-1 nyumbani katika Ligi ya Mabingwa.

Katika Kombe la Shirikisho ndani ya kipindi hicho cha kuanzia mwaka 2010 ililala 2-0 ugenini dhidi ya Dedebit ya Ethiopia mwaka 2010 baada ya sare ya 4-4 nyumbani, huku mwaka 2015 ililala ugenini mabao 2-0, salama yao ni baada ya kuilaza BDF ya Botswana mabao 2-1 nyumbani na kusonga kwa jumla ya mabao 3-2 na kukutana na FC Platinum ya Zimbabwe na kulala tena 1-0 ugenini baada ya ushindi wa 5-1 nyumbani kabla ya kulala 1-0 kwa Etoile du Sahel ya Tunisia baada ya sare ya 1-1 nyumbani na kuwa mwisho wa safari yao kwa mwaka huo wa 2015.

Mwaka 2016 baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa waliangukia katika Kombe la Shirikisho hatua ya playoffs na kulala ugenini 1-0 dhidi ya SD Esperanca ya Angola na kubebwa na ushindi wa nyumbani wa mabao 2-0 na kusonga mbele kuingia makundi ambapo hakuna mechi hata moja iliyoshinda ugenini katika kundi lao.

NSAJIGWA AFUNGUKA

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa, alisema ni kweli Yanga rekodi zake kwa mechi za ugenini hazivutii, lakini hiyo ni zilipendwa na kwamba kwa sasa akienda na Yanga kama kocha anaamini kila kitu kitakuwa sawa.

“Nilikuwa ninakwenda kama mchezaji na kupata matokeo mabaya, lakini sasa hivi ninakwenda nikiwa kama mwalimu, matumaini yangu kwamba tutavuka hatua hii na nina Imani kubwa kutokana na maandalizi ambayo tumeyafanya,” alisema akiwa na imani na akina Tshishimbi na Ajibu na wenzake wataivusha Yanga.