Kumbe moto wa Okwi chamtoto tu

Muktasari:

  • Luhende aliyewahi kutamba na Yanga kabla ya kwenda Mwadui, alikiri Okwi bado ni mchezaji hatari na anatumia akili na mbinu za kutengeza mabao ili timu yake iweze kupata matokeo mazuri, lakini akasema kwa upande wa kasi staa huyo amepungukiwa.

LICHA ya Emmanuel Okwi wa Simba kuwa kinara wa mabao Ligi Kuu Bara akiwa ameshafunga mara 14 hadi sasa msimu huu, beki wa Mwadui FC, David Luhende, amefichua kuwa staa huyo angekuwa na kasi kama zamani, moto wake ungekuwa haushikiki.

Luhende aliyewahi kutamba na Yanga kabla ya kwenda Mwadui, alikiri Okwi bado ni mchezaji hatari na anatumia akili na mbinu za kutengeza mabao ili timu yake iweze kupata matokeo mazuri, lakini akasema kwa upande wa kasi staa huyo amepungukiwa.

“Licha ya kwamba tumetoka nao sare, ila Okwi ataendelea kufunga sana kwenye mechi za Ligi Kuu. Anatumia akili kuliko nguvu, hilo ndilo linalowasahaulisha mabeki kazi yao ya kumchunga tofauti na straika anayetumia nguvu,” alisema.

“Futilia mabao anayofunga Okwi, mengi ni ya kiufundi ndio maana nasema atasumbua sana Ligi Kuu, pia atawasaidia Simba kwenye michuano ya kimataifa ambako kunatumika mbinu zaidi kuliko nguvu.”

Katika hatua nyingine, Luhende aliwashauri Simba kuongeza umakini ili wazidi kuendeleza wimbi la ushindi dhidi ya Gendarmerie ya Djibouti kwenye mechi ya marudiano ya raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika itakayochezwa Jumanne ijayo.

JUUKO AMEZIDI

Katika hatua nyingine nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay, ambaye sasa ni mchambuzi wa soka wa kituo cha Azam TV, ameshangazwa na rafu anazofanya beki Juuko Murshid akidai hazina ulazima na zinaigharimu Simba.

Juuko alijikuta kwenye wakati mgumu juzi baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano zilizozaa nyekundu kwenye mchezo dhidi ya Mwadui ambao timu yake ya Simba iliambulia alama moja kufuatia sare ya mabao 2-2.

Mayay alimtaka Juuko kufahamu kwamba hata kama ni beki, si lazima acheze faulo nyingi kwani kwa kufanya hivyo atakuwa akijishushia heshima.

“Simba wanaelekea kwenye mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho, benchi la ufundi linatakiwa kumfunda awe mwangalifu ili kuepusha kadi zisizo na sababu,” alisema Mayay.

“Vinginevyo ataigharimu timu yake, kwenye mechi kubwa ni hatari sana hiyo.”