Kumbe ishu ya Ajibu ipo hivi aisee!

Muktasari:

Ndio, ni kama vile straika huyo mpya wa Jangwani, ameiingiza mkenge timu yake hiyo baada ya kufunga bao moja tu katika mechi 19 zilizopita.

WATETEZI wa Ligi Kuu Bara, Yanga, kesho Jumatano watashuka Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam kucheza na Majimaji, lakini imebainika mashabiki wake bado hawana raha kutokana na mwenendo wa kusuasua wa straika wao, Ibrahim Ajibu.

Mashabiki hao wanashindwa kujua ile kasi ya Ajibu aliyoanza nayo msimu huu imeishia wapi.

Ndio, ni kama vile straika huyo mpya wa Jangwani, ameiingiza mkenge timu yake hiyo baada ya kufunga bao moja tu katika mechi 19 zilizopita.

Ajibu aliyetua Yanga kwa mbwembwe akitokea kwa watani zao Simba, alianza msimu kwa kasi akifunga mabao matano na kutoa pasi tatu za mabao katika mechi saba za mwanzoni, lakini sasa upepo umemkataa kabisa.

Tangu staa huyo afunge bao la mwisho la Ligi Kuu Bara Oktoba 22 mwaka jana, Yanga imecheza mechi 10 za ligi sawa na dakika 900, huku staa huyo akishindwa kabisa kucheka na nyavu.

Habari mbaya zaidi ni kwamba katika mashindano yote, tangu mwishoni mwa Oktoba, Yanga imecheza mechi 19 sawa na dakika 1,710 lakini staa huyo amefunga bao moja tu. Alifunga dhidi ya Taifa Jang’ombe katika Kombe la Mapinduzi.

Ubutu huo wa Ajibu umemfanya staa mwingine wa timu hiyo, Obrey Chirwa, sasa kuwa tegemeo na amefunga mabao saba Ligi Kuu zikiwamo Hat Trick mbili tangu Ajibu alipofunga bao la mwisho.

WADAU WAMTETEA

Straika wa zamani wa Prisons na Yanga, Herry Morris, amesema: “Ajibu ni mchezaji mzuri, alionyesha umuhimu wake katika mechi za mwanzoni. Kukosekana kwa watu kama Chirwa na Ngoma kwa nyakati fulani, kumemfanya apotee kwa sababu mabeki wamekuwa wanamkamia.”

Kiungo wa zamani wa Yanga, Omary Kapilima, alisema upepo wa staa huyo umegeuka licha ya kuanza vizuri katika mechi za mwanzoni mwa msimu, lakini sasa anapaswa kuongeza juhudi ili kuibeba timu yake.

“Nadhani anajua kwamba Yanga inamtegemea sana hivi sasa, ni kweli upepo umebadilika kwake, lakini anatakiwa afanye mazoezi sana ili ufiti uongezeke, timu hizi zinahitaji matokeo wakati wote,” alisema.

“Kuna wakati alikuwa majeruhi, lakini si kivile, labda tu kwamba alikosa mechi baada ya kupata kadi tatu za njano, lakini hata hivyo amecheza mechi nyingi kwa hiyo bado alikuwa na uwezo wa kufunga tena mabao mengi,” alisema.