Yanga wapigwa kiroho safi, hamna figisu

Muktasari:

Pambano hilo lilizikutanisha timu hizo zikiwa na tofauti ya pointi mbili, Simba ikiwa kileleni na pointi 51 wakati watani zao Yanga wakiwa na alama 49.

LIGi Kuu Tanzania Bara inayoshirikisha timu16 wikiendi iliyopita ilishuhudiwa ikiwa na pambano la kukata na shoka la watani wa jadi, Simba na Yanga.

Pambano hilo lilizikutanisha timu hizo zikiwa na tofauti ya pointi mbili, Simba ikiwa kileleni na pointi 51 wakati watani zao Yanga wakiwa na alama 49.

Kwa jinsi ligi hiyo ilivyo ni kwamba mbio za ubingwa zimebaki kwa mafarasi hao wawili ambao ni hao Simba na Yanga na baada ya dakika 90 za pambano lao, Yanga ilijikuta ikilala mabao 2-1 kwa Simba.

Kichapo hicho kiliwawahuzunisha mashabiki wa Yanga kote duniani na baadhi yao waliingia mitandaoni huku na kule kuwakashifu wachezaji na makocha wao na kadhalika kwamba wamechangia kipigo hicho.

Ukweli ulivyo ni kwamba Watanzania ni mashabiki wa kweli wa soka na jambo linalofahamika ni kwamba timu zikutanapo moja kati ya mambo matatu lazima litatokea. Aidha moja ishinde, kufungwa ama kutoka sare.

Mambo mengi yamezungumzwa mitandaoni kuhusu wachezaji kutocheza vizuri kisa na maana hawajalipwa mishahara yao, mara wengine hawakujituma katika mechi hiyo, lakini tunachokisahau ni kuwa timu zote huwa zimejipanga.Wengine wamezungumza kwamba Yanga hawakutembelea babu zao kitu ambacho naziona ni porojo tupu.

Ushirikina katika soka hauna nafasi hapa duniani, mtu asijidanganye kwamba ushirikina unaweza kufanya ushinde ama ufungwe. La hasha. Soka lazima ujipange kimazoezi, kimbinu, kiufundi, kiakili na kadhalika.

Lazima uweke Mungu mbele wakati wowote unapotaka kufanya jambo lolote. Mimi mwenyewe nimecheza Yanga na kwangu ilikuwa ni mazoezi na kujiamini na kazi tu. Mambo ya kishirikina hayakuwa yananihusu hata chembe. Kwa hivyo hapo ndugu zanguni mtoke kabisa.

Mkubali kwamba mechi Simba ilishinda kwa uhalali kabisa uwanjani na wala hakuna hila zozote.

Kwa upande mwingine nimesoma kwamba mashabiki wanalaumu baadhi ya wachezaji kucheza kwa viwango vya chini kwa sababu ya kucheleweshwa kwa malipo yao ya mishahara.

Kwa wachezaji ambao wanaweza kuwa wanasoma makala yangu, tafadhalini ndugu zanguni najua kuwa mishahara ni lazima tulipwe, ni lazima, lakini iwapo umeamua kuingia uwanjani kusakata soka tafadhali jambo ambalo nawasihi ni kuwa iwapo umekubali kufanya kazi basi ifanye na roho moja. Nitawapa mfano. Ipo siku nikiwa Yanga tulikosana kabisa na wachezaji kadhaa wa Yanga kisa na maana walikuwa wanataka tugome kucheza mechi dhidi ya Al Ahly ya Misri kisa na maana kuna posho fulani hazikuwa zimelipwa.

Ilikuwa shida sana. Ilibidi niingilie kati kisa na maana hata Kocha Dusan Kundic alikuwa ameshindwa cha kufanya. Niliambia wachezaji wanaotaka kugoma waondoke kambini wasije wakatuharibia kambi. Wachezaji kadhaa walileta shida lakini nikaweka ngumu na nikaweleza kwamba hilo jambo ambalo wanataka kulifanya ni mbaya sana kisoka kwani itakuwa ni aibu kubwa sisi kutocheza hiyo mechi eti tunadai posho za mechi. Niliwaambia ni jambo la kawaida kwa mishahara na posho za wachezaji kuchelewa lakini sio wazo zuri kugoma kucheza mechi. Hatimaye walinisikiliza na mechi ikapigwa. Nikawaambia mwenye anafikiria kuwa ni lazima hizo hela zilipwe kabla mechi aondoke kambini.

Siasa za kijinga ndogo ndogo kama hizo huleta mtafaruku sana ndani ya klabu. Mechi ya Simba na Yanga ni mechi kubwa. Ni mechi ambayo mchezaji akijua hayuko katika hali yake ya kawaida afadhali asijaribu kuicheza. Ni mechi ambayo iko na ushabiki mkubwa saana. Ushabiki ambao kwa kweli sijawahi kuona klabu yeyote niliyochezea duniani.

Machungu makubwa ya mashabiki wa Yanga ni kuwa kufungwa na Simba wakiwa wachezaji 10 uwanjani kunaleta shida, lakini wafahamu kuwa Simba wachezaji wao walijiamini saana katika hiyo mechi ndipo walipata ushindi huo.

Makosa ya Yanga ni wakati walipofunga bao la kwanza walilala. Wakati mchezaji wa Simba alipewa kadi nyekundu basi wakafikiria kuwa mechi imekwisha. Yanga shida yao walipunguza kasi ya mechi, wakaona kuwa watashinda. Mechi ni dakika 90 cha kuongeza wachezaji wengi wa Yanga walizembea. Walizembea kabisa kiasi ni wachache tu walifanya juhudi ya kushinda hiyo mechi. Kelvin Yondani ni mojawapo ya wachezaji wa Yanga ambao kwa kweli alijitolea sana katika mechi hiyo. Alijaribu sana na kwa kweli bila yeye hapo nyuma mambo yangekuwa magumu zaidi.

Kwa hivyo iwapo wachezaji wa Yanga wangejitolea hata kiasi tu, basi hiyo mechi wangeshinda. Ni aibu kwa kweli kufungwa na timu ambayo ipo na wachezaji 10 uwanjani lakini ikumbukwe hakuna kitu kibaya sana kucheza ni timu iko na upungufu wa mchezaji mmoja,kwani wao hujitolea sana.

Na pia uzito wa mechi hiyo ulidhihirishwa na wachezaji wa Simba. Ni funzo kubwa kwa wachezaji wa Yanga wajue kuwa mechi hushindwa punde tu refa anapopuliza kipyenga cha mwisho ndugu zanguni. Kabla hivyo lazima kila mchezaji ajitolee ndani ya dakika 90 za mchezo na pia ndani ya dakika za ziada. Kwa soka mashabiki wa Yanga poleni. Na mkumbuke asiye kubali kushindwa sio mshindani.