Yanga ina kila sababu ya kuifunga Medeama ugenini

Muktasari:

  • Yanga iliyoondoka mwishoni mwa wiki hii kuelekea Ghana, ina kila sababu ya kuhakikisha inapata ushindi ugenini, kwani matokeo yoyote zaidi ya ushindi itakuwa na maana ya kujiengua miongoni mwa timu za kuwania kutinga nusu fainali.

MABINGWA wa soka wa Tanzania na wawakilishi pekee wa michuano ya kimataifa, Yanga leo Jumanne itakuwa ugenini kuvaana na Medeama ya Ghana katika mechi ya marudiano ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Yanga na Medeama zipo Kundi A pamoja na timu za TP Mazembe ya DR Congo na Mo Bejaia ya Algeria na mpaka sasa msimamo unaoonyesha kuwa wawakilishi wetu wanaburuza mkia katika kundi hilo wakiwa na pointi moja tu.

Pointi hiyo waliipata kwenye mchezo wa wiki iliyopita uliochezwa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Hiyo ilikuwa sare pekee na mechi ya kwanza kwa Yanga kuvuna pointi katika kundi hilo, kwani mechi zake mbili za awali dhidi ya Bejaia na Mazembe ilipoteza kwa kipigo cha bao 1-0 kwa kila mchezo.

Yanga iliyoondoka mwishoni mwa wiki hii kuelekea Ghana, ina kila sababu ya kuhakikisha inapata ushindi ugenini, kwani matokeo yoyote zaidi ya ushindi itakuwa na maana ya kujiengua miongoni mwa timu za kuwania kutinga nusu fainali.

Awali Yanga ilipoteza matumaini ya kujiweka pazuri katika mbio za kutinga nusu fainali, baada ya sare dhidi ya Medeama, lakini matokeo ya suluhu yaliyopatikana katika mechi ya Bejaia na Mazembe yalirejesha uhai wa wawakilishi hao katika mbio hizo.

Hata hivyo, matumaini hayo hayatakuwa na maana kama Yanga leo itashindwa kupata ushindi wa aina ugenini dhidi ya Medeama, huku pia ikiomba pambano la marudiano baina ya wapinzani wa kundi hilo, Bejaia na Mazembe likose mshindi.

Mazembe ndio inayoongoza msimamo wa kundi hilo mpaka sasa ikiwa na pointi saba baada ya mechi tatu, ikifuatiwa na Bejaia yenye alama tano katika mechi zake tatu na Medeama ikiwa nyuma yao ikiwa na  pointi 2.

Ukiangalia msimamo huo ni wazi ushindi ndio silaha pekee ya kuisaidia Yanga katika vita ya kuwania kuweka rekodi ya kucheza hatua ya nusu fainali, hasa kama itafanya vema pia katika mechi zake mbili za kukamilisha ratiba ya kundi lake.

Mechi mojawapo ni ile ya nyumbani itakayochezwa baada ya mchezo wa kesho ambapo itaumana na Bejaia na  mwishoni mwa mwezi ujao itakapoifuata Mazembe, lakini ikiwa imeshajua mwelekeo wake kwenye kundi hilo. Mwanaspoti linaungana na wadau wote wa michezo wenye kuiombea dua njema Yanga ili ifanye vizuri ugenini, lakini pia ikiwakumbusha wachezaji na benchi zima la ufundi kuwa wanadhima kubwa ya kuthibitisha ubora wao.

Watalithibitisha hilo kwa kuhakikisha wanashuka uwanjani kwa umakini mkubwa na kuhakikisha hawafanyi makosa ya kizembe ambao yamekuwa yakiigharimu timu hiyo katika mechi zake za michuano hiyo.

Tatizo la mabeki wa timu hiyo pamoja na kipa wao la kukaba kwa macho wakiwa langoni mwao limesababisha Yanga ipoteze pointi nane katika dakika 270 ilizotumia katika mechi zake tatu za awali.

Kosa kama hilo halipaswi kurudiwa tena Ghana, kwani siku zote mtu hujifunza kutokana na makosa na tunaamini makosa ya mechi dhidi ya Bejaia, Mazembe na hata Medema katika mechi iliyopita itakuwa ni somo tosha kwa Yanga katika kujirekebisha.

Mastraika wa Yanga, ni lazima nao wawe makini na kuzitumia vema nafasi zote zinazotengenezwa uwanjani ili kuipa timu yao mabao ya kutosha.