Yanga ianze maandalizi sasa dhidi ya Zanaco

Muktasari:

  • Zanaco ililazimishwa suluhu nyumbani wiki iliyopita kabla ya juzi Jumamosi kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini na kukata tiketi ya kusonga mbele.

KLABU ya Yanga imefanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya juzi Jumamosi kuing’oa Ngaya de Mbe ya Comoro.

Yanga ililazimishwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam katika mechi ya marudiano, lakini imesonga mbele kwa jumla ya mabao 6-2 kwani awali ilishinda ugenini wiki iliyopita kwa mabao 5-1.

Kufanikiwa huko kwa Yanga kuingia raundi ya kwanza maana yake ni kwamba sasa itavaana na Zanaco ya Zambia ambayo iliing’oa APR ya Rwanda kwa jumla ya bao 1-0.

Zanaco ililazimishwa suluhu nyumbani wiki iliyopita kabla ya juzi Jumamosi kupata ushindi wa bao 1-0 ugenini na kukata tiketi ya kusonga mbele.

Ratiba inaonyesha kuwa, mechi ya kwanza ya Yanga katika raundi ya kwanza dhidi ya Zanaco itaanzia nyumbani kabla ya kwenda kumalizia ugenini. Ndivyo itakavyokuwa pia kwa Azam inayoiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikianzia raundi ya kwanza.

Azam itaikaribisha Mbabane Swallows ya Swaziland iliyoitupa nje wawakilishi wa Botswana Orapa United kwa jumla ya mabao 4-2. Hivyo kama ambavyo Yanga inavyotakiwa kuanza kuifikiria mechi yake ya Zanaco na kuanza mikakati ya mapema, ndivyo ambavyo hata Azam inapaswa ifanye sasa.

Yanga wamebakisha hatua moja kabla ya kuingia makundi, hivyo ni lazima ikaze. Zanaco siyo timu nyepesi na bahati nzuri ilishawahi kukutana nao mwaka 2006 katika mechi za raundi ya awali na Yanga kugaragazwa kwa jumla ya mabao 3-2. Yanga ilishinda nyumbani 2-1 na kwenda kulala ugenini mabao 2-0.

Hivyo siyo timu nyepesi na inafahamika wazi kisoka Zambia wameitangulia sana Tanzania, hivyo ni lazima wawakilishi wetu wajipange kwelikweli.

Hata Azam nao hawapaswi kuichukuliwa wepesi Mbabane hata kama nchi wanayotoka haitishi sana kisoka, lazima kuwe na mipango mkakati ya kuhakikisha wanashinda ili kufuzu hatua ya mwisho ya play-off kabla ya kuingia makundi.

Timu zetu zitambue kuwa mashabiki wamechoka kuona wawakilishi wetu wanakuwa wasindikizaji, hivyo wajipange na kupambana kuhakikisha zote mbili zinatinga makundi na kuanza kuogelea kwenye mamilioni ya fedha za CAF.

Michuano hii ina fedha nyingi, lakini ni kama klabu zetu hazina mpango nazo ndiyo maana huwa hazielekezi nguvu kubwa kwenye michuano hiyo ya kimataifa na kuishia kuwa wasindikizaji wa wenzao.

Mwaka 2017 uwe mwaka wa mabadiliko na klabu zetu ziweke nia ya kuhakikisha zinafika mbali, ziingie kwenye makundi na kufanya vyema na kusonga mbele mpaka hatua zinazofuata za robo fainali, nusu fainali na fainali kwa jumla.

Mwanaspoti linaamini hiyo inawezekana kwa sababu Tanzania ni moja ya nchi zenye vipaji vya soka, ila uzembe unaofanywa na viongozi na hata wachezaji wakati wa mashindano hayo na kutojiamini ndiko kunakotuangusha.

Tusikubali tena kuendelea kuwa wasindikizaji, klabu zetu lazima zipambane kiume na haziwezi kufanikiwa kama hazitaanza mapema maandalizi yao.