UCHAMBUZI : Yanga, Azam ziwe makini mechi za kimataifa Afrika

Saturday February 11 2017Ali Mayay

Ali Mayay 

By Ali Mayay mayay@yahoo.com

SHIRIKISHO la Soka Afrika (Caf) limefanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa uendeshaji wa mashindano yake kwa ngazi za klabu barani humu.

Caf inasimamia Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ambapo mabingwa wake kwa sasa ni Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na TP Mazembe ya DR Congo zilizoshinda mataji hayo mwishoni mwa mwaka jana.

Mabadiliko yaliyofanyika ni kuongeza kwa idadi ya timu zitakazoshiriki katika hatua ya makundi kutoka nane za awali na 16, hivyo kuwa na makundi manne ya timu nne kila kundi.

Hizo zote ni jitihada za Caf za kutaka soka lisambae katika bara zima la Afrika kwa kujaribu kushirikisha timu nyingi katika hatua ya mwisho, ili kuzijengea uwezo wa kushindana na hatimaye kufanikiwa kufika hatua za maendeleo ya soka kama ilivyo baadhi ya nchi za Ulaya na Marekani Kusini.

Mashindano Ligi ya Mabingwa Afrika ni miongoni mwa mashindano makongwe barani humu, kwani mwaka huu utakuwa ni msimu wake wa 53 tangu yalipoasisiwa na yatakuwa ya 21 tangu Caf ilipoanzisha utaratibu mpya wa kuyaendesha kwa mechi za nyumbani na ugenini ambao ulisaidia kupatikana kwa udhamini kutoka kwa makampuni mbalimbali.

Hivyo, ukongwe wake unatakiwa kutafsiri mafanikio ya soka kuanzia ngazi za klabu hadi ngazi ya taifa kwa nchi za Afrika.

Katika mashindano haya ya msimu wa 2017, Yanga na Azam zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zinatarajiwa kutuwakilisha katika mashindano hayo yanayosimamiwa na Caf. Azam yenyewe itaiwakilisha Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho Afrika kama ilivyokuwa mwaka uliopita, lakini ikianzia raundi ya kwanza baada ya Caf kutoipanga katika ratiba ya mechi za awali.

Matajiri hao wa Bongo wanasubiri kuanza ngarambe yao mwezi ujao kwa kuvaana na mshindi wa mechi kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland.

Mabingwa wa Tanzania, Yanga kesho Jumapili wataanza mechi zao za raundi za awali kwa kuvaana wakiwa ugenini dhidi ya Ngaya Club kutoka Visiwa vya Comoro watakaorudiana nao wikiendi ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Azam na Yanga zimekuwa zikishiriki kwa miaka ya hivi karibuni mfululizo katika michuano hii ya kimataifa bila ya mafanikio kama wadau wengi wa soka wanavyotarajia iwe kwao.

Katika msimu uliopita Azam iliondolewa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho kwa kufungwa na Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda mabao 2-1 nyumbani kabla ya kwenda kupoteza ugenini mabao 3-0.

Yanga yenyewe ilijitahidi na kuweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza ya Tanzania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika katika raundi ya pili na kuangukia kapu la shirikisho.

Vijana hao wa Jangwani chini ya Kocha Hans Pluijm, walizing’oa Cercle De Joachim ya Mauritius na APR ya Rwanda kabla ya kukwama kwa Al Ahly ya Misri waliotoka nao sare ya 1-1 nyumbani kisha kwenda kulala ugenini nchini Misri kwa mabao 2-1 na hatimaye kuingia katika hatua ya mtoano katika Kombe la Shirikisho.

Katika hatua hiyo katika mechi ya Play-off, Yanga waliiondosha GD Sagrada Esperanca ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, yaliyotokana na ushindi wa mabao 2-0 nyumbani na kwenda kupoteza ugenini Angola bao 1-0.

Ushindi huo dhidi ya Waangola uliwaingiza Yanga kwenye makundi na kupangwa kundi moja na klabu za MO Bejaia ya Algeria, TP Mazembe ya DR Congo na Medeama ya Ghana. Kundi lao ndilo lililotoa timu zilizocheza fainali iliyozikutanisha MO Bejaia na Mazembe na Wakongo kubeba taji hilo.

Katika kundi lake, Yanga ilishinda mechi moja tu dhidi ya Waaljeria na kupata sare moja na Medeama, huku mechi nyingine zote ikipoteza na kuburuza mkia.

Hivyo, ukiangalia ushiriki wa timu hizo katika mashindano hayo ya Afrika ukirejea kwenye mfumo wake ulivyobadilishwa msimu huu kwa Caf kwa kuongeza idadi ya timu zitakazoshiriki katika hatua ya makundi utaona ni mteremko kwao.

Yanga na Azam zina kila sababu ya kuvuka hatua za awali na kushiriki makundi, hivyo zinawajibika kuingia katika hatua hiyo kwani kinyume na hilo itakuwa ni sawa na kuporomoka zaidi na kurudi nyuma tena kwa hatua nyingi mno.

Kama Yanga itafanikiwa kuifunga Ngaya Club katika hatua ya awali, itasubiri mshindi kati ya Zanaco ya Zambia na APR ya Rwanda kabla ya kuingia katika hatua makundi, Azam yenyewe itasubiri mwezi ujao kujua hatma yao pia.

Manufaa pekee ambayo soka la Tanzania itapata kupitia wawakilishi wao katika michuano ya kimataifa ni kushinda michezo yao ili zicheze makundi ili tushuhudie mechi sita za kimataifa katika viwanja vyetu.

Ndio maana naziombea zifanye kweli, lakini kuwa na umakini kusudi wasituangushe katika uwakilishi wao msimu huu kama zilivyofanya msimu uliopita.