Wazee wa klabu kubwa wasiwe chanzo cha migogoro

Muktasari:

Kutokana na hali hiyo ya wazee kuaminiwa, kuheshimiwa na kupewa kipaumbele cha kusikilizwa kwa kila jambo lenye utata, ilitarajiwa hata wazee wa klabu za Simba na Yanga nao wawe mfano wa kuigwa katika kurekebisha mambo klabuni kwao.


UZEE ni hekima na busara ndiyo maana upo msemo kuwa utu uzima dawa. Misemo hiyo na hata ile kauli kwamba palipo wazee huwa hapaharibiki jambo, hii inaonyesha namna gani uzee unavyoheshimiwa katika jamii.

Hata katika maisha ya kawaida katika jamii, wenye kufanya uamuzi inapotokea tatizo, aghalabu huwa ni wazee kwa sababu ya kuaminiwa kwa busara walizonazo.

Ni nadra kuona vikao vya uamuzi vikiendeshwa na kuamuliwa na vijana kwa sababu ya kuhofia uamuzi usiyo na hekima wala busara, japo hiyo ni dhana tu.

Kutokana na hali hiyo ya wazee kuaminiwa, kuheshimiwa na kupewa kipaumbele cha kusikilizwa kwa kila jambo lenye utata, ilitarajiwa hata wazee wa klabu za Simba na Yanga nao wawe mfano wa kuigwa katika kurekebisha mambo klabuni kwao.

Klabu hizo kwa kutambua umuhimu wa wazee, wemeunda mabaraza ya wazee, sio kwa kuwapa heshima tu kwa vile ni waasisi wa klabu zao, lakini ni kwa kuwaamini kuwa, hekima na busara walizonazo ni msaada mkubwa mambo yanapoharibika.

Inawezekana viongozi wanaoingia madarakani ambao wengi wao ni vijana wenye uwezo mkubwa kiuchumi na elimu ya kutosha kulinganisha na wazee, kiasi cha kufikia hatua ya kuwadharau wazee na kutowashirikisha katika baadhi ya mambo. Pia, huenda wazee wamekuwa wakipuuzwa kwa sababu baadhi yao hufanya mambo yasiyotofautiana na vijana wenye mihemko, kuongozwa na hisia na uamuzi sawa na mwendokasi unaohatarisha amani na utulivu wa klabu zao.

Baadhi ya wazee wa klabu hizo wamekuwa wakifanya mambo yanayozua maswali mengi kuliko majibu juu ya uwepo wao na hekima na busara walizonazo katika kuhimili mihemko na mambo yanayojitokeza ndani ya klabu zao.

Tumewahi kusikia wazee wa Yanga wakikurupuka katika kupinga kila jambo la kuiletea maendeleo klabu hiyo, wakiponda wakati mwingine viongozi, makocha na hata wachezaji mbali na kupondana au kulumbana wenyewe kwa wenyewe.

Kadhalika upande wa pili kwa watani zao Simba, kuna baadhi ya wazee nao wamekuwa mstari wa mbele katika kuleta vurugu kwa kupinga kila jambo la maana na wakati mwingine kufanya mambo ya ovyo pengine kuliko hata vijana. Kwa mfano kwa sasa wazee wa Simba wamecharuka wakitaka kwenda kumwona Rais John Magufuli, wakitishia kama hawatasikilizwa watakimbilia mahakamani, kisa ni mvutano juu ya suala la kufanyika mabadiliko ya uongozi klabuni kwao.

Mwanaspoti halipingi misimamo ya wazee hao na hata wale wa Yanga, lakini kwa kuzingatia kuwa utu uzima ni dawa, tulitarajia wazee hao ndio wawe wa kwanza kurekebisha hali ya mambo ndani ya klabu hizo kwa ustawi wa Simba na Yanga.

Simba na Yanga zina miaka mingi zikiwa tegemezi, zimekuwa hazikui kama klabu nyingine zilizoanzishwa sambamba nazo kwa sababu ya kukosa watu wa kuzipa miongozo ya kimaendeleo. Kwa kuwa dunia imebadilika, baadhi ya watu wanaoona mbali wamekuwa wakitaka kuzikwamua hapo zilipo, lakini wazee wamekuwa watu wa kwanza kuzuia mabadiliko hayo kwa sababu ya utashi na masilahi yao binafsi.

Hatujawahi kuwasikia wazee wakiibuka kutangaza kusaidia kuwalipa wachezaji na makocha mishahara pale viongozi wanapokuwa wamekwama ama kuchelewa kuwalipa mpaka kusababisha wakati mwingine migomo baridi. Pia kujitolea kusafirisha na kuzihudumia timu hizo katika ushiriki wao wa michuano ya ndani ama ile ya kimataifa, kazi hizo zinafanywa na viongozi katika mazingira magumu, ilimradi klabu hizo zisiaibike.

Hata hivyo, ni wazee wanaokuwa wa kwanza kuwashambulia kwa maneno viongozi na wafadhili ama wahisani wanaozibeba timu zao, pale tu wanapohisi masilahi yao yanaguswa.

Inawezekana wazee wanapuuzwa na viongozi, labda kwa vile mabaraza yao hayatambuliki moja kwa moja, mikatiba ama wanapuuzwa tu, kwa kuonekana ndio tatizo la migogoro klabuni kwao, lakini bado kama wanachama wa klabu hizo wana nafasi kubwa ya kurekebisha matatizo kupitia vikao na mikutano yao. Wanastahili kuwa mfano mbele ya wanachama wengine katika kuweka mambo sawa na kama hawasikilizwi na viongozi, ni haki yao kuyafikisha hayo mbele ya wanachama wenzao ili kujivua lawama.

Kadhalika ni vyema viongozi wakawapa heshima na kuwasikiliza wazee wa klabu zao kwa kuzingatia kuwa, bila ya wazee hao nafasi za kuja kuziongoza wasingezipata, iwapo Simba na Yanga zisingekuwapo. Wasipuuzwe.

Wazee hao walivuja jasho na kuziasisi, kuziendeleza na kuzilinda klabu hizo kuwa hai mpaka leo, hivyo wapewe heshima zao, lakini pale wanapoenda kombo pia ni vyema kukumbushwa kuwa wao ni mfano na tegemeo kwa klabu hizo.