Wawakilishi wa Tanzania wasifanye uzembe tena

Muktasari:

  • Kwa miaka mingi wawakilishi wa Tanzania wamekuwa kama wasindikizaji na mwaka huu ndio angalau kidogo Yanga ilifanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya awali kutemwa Ligi ya Mabingwa.

SHIRIKISHO la Soka Afrika (Caf) juzi Jumatano ilitangaza ratiba ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu wa mwaka 2017. Ratiba hiyo ilipatikana katika droo iliyoendeshwa kwa usiri mkubwa kwenye Makao Makuu ya shirikisho hilo mjini Cairo, Misri ambapo wawakilishi wa Tanzania Bara, Yanga na Azam pamoja na wale wa visiwani Zanzibar, Zimamoto na KVZ wamefahamu zitaumana na timu gani.

Yanga itakayoshiriki Ligi ya Mabingwa itaanzia mechi za hatua ya awali kwa kuvaana ugenini na Ngaya Club de Mde ya Comoro, wakati washiriki wa Kombe la Shirikisho, Azam itaanzia raundi ya kwanza kama mwaka huu.

Azam itasubiri kuanza mechi za mkondo huo kwa kupatikana mshindi wa mechi za awali kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland. Mwaka huu Azam ilianzia pia hatua kama hiyo kwa kupangwa kuvaana na Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

Wawakilishi wa Zanzibar, Zimamoto na KZV zinazoshiriki michuano hiyo ya Afrika kwa mara ya kwanza, zitaanzia nyumbani mechi za hatua ya awali kwa Zimamoto kuialika Ferroviario Beira ya Msumbiji katika Ligi ya Mabingwa na KVZ itaikaribisha Le Messager Ngozi ya Burundi kwenye Kombe la Shirikisho. Katika michuano ya mwaka ujao kuna tofauti kubwa ya uendeshwaji wake, baada ya timu kupenya mechi za raundi ya kwanza tu, zitaingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi itakayojumuisha timu 16. Yaani Ligi ya Mabingwa itakuwa na timu 16 ambapo, makundi manne yatakayokuwa na timu nne kila moja, sawa na itakavyokuwa kwa michuano ya Kombe la Shirikisho.

Baada ya hapo timu zitachuana katika hatua hiyo ili kusaka timu nane ya kila michuano kuwania kucheza hatua robo fainali na kuchujana mpaka fainali zitakazochezwa kati ya Septemba- Novemba, 2017. Kutoka kwa ratiba hiyo na kubadilishwa kwa mfumo wa uendeshwaji wa michuano hiyo fursa kwa wawakilishi wetu kujipanga mapema ili kuona safari hii hawarudii makosa ya miaka ya nyuma.

Kwa miaka mingi wawakilishi wa Tanzania wamekuwa kama wasindikizaji na mwaka huu ndio angalau kidogo Yanga ilifanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya awali kutemwa Ligi ya Mabingwa.

Mwanaspoti linaamini kuwa, wawakilishi wetu safari hii zitajipanga vema ili kufanya vizuri zaidi na kuiletea sifa Tanzania katika anga la kimataifa, pia wasijaribu kupuuza wapinzani wao hata kidogo.

Tayari kuna wadau wa soka wanaamini Yanga imepangwa kibonde kutoka Comoro na ikipenya hapo haitakuwa na kazi ngumu kwa vile itacheza na APR ya Rwanda ama Zanaco ya Zambia. Hii ni kutaka kuwatia ujinga Yanga. APR, Zanaco na hata hao Comoro sio wepesi katika maana halisi ya mchezo wa soka ambapo, timu huadhibiwa kutokana na makosa.

Yanga na wawakilishi wengine, itambue kuwa wapinzani wao wana ndoto kama walizonazo hivyo wapambane hatua moja hadi nyingine ili kufanikisha malengo ya kufika hatua za juu zaidi.

Kufanya dharau yoyote ni kukata tiketi ya kuaibika na kuishia njiani na kuyaacha mamilioni ya Caf yakiendelea kuwapitia mbali.

Imani yetu kama wadau wa soka ni kwamba, mabadiliko yaliyofanywa kwenye vikosi vya timu za Yanga na Azam yanaweza kuwasaidia timu hizo kufanya kweli kwenye michuano hiyo ya kimataifa na kujitangaza zaidi.

Mbali na nyota kadhaa wa kimataifa wa ndani na nje ya nchi, pia timu zote zina makocha wa kimataifa ambao wanapaswa kuthibitisha ubora wao kwa kuzibeba klabu hizo na kuacha visingizio.

Hata klabu za Zanzibar ambazo zimekuwa wasindikizaji zaidi katika michuano ya kimataifa, nazo zinaingia kwenye dirisha dogo la usajili lililofunguliwa visiwani humo na kufungwa Januari 15, mwakani.

Kama klabu hizo zitatumia vema dirisha hilo la usajili kuimarisha vikosi vyao ili angalau kufanya kweli katika michuano hiyo na kuondokana na usindikizaji wa miaka mingi kwenye michuano hiyo kiasi cha kuwa jamvi la wageni.

Naamini kwa vile tunaingia mwaka mpya, bila shaka kila kitu ndani ya wawakilishi wetu nacho kitakuwa kipya kwa maana ya mipango mkakati na hata malengo ndani ya ushiriki wao wa michuano ya mwakani. Inawezekana!