ROHO NYEUPE: Wanaosajili na kuajiri Azam wanamtia hasara Bakhresa

Muktasari:

  • Kwanza watu hawa wamekuwa na tatizo la kufahamu wachezaji wazuri hasa kwa upande wa wachezaji wa kigeni. Pili, watu hawa wamekuwa wakinunua wachezaji wa kawaida kwa fedha nyingi, bila kutazama soko linasemaje.

SAID Salim Bakhressa na upole wake kama alivyo. Ana pesa si mchezo. Kwa Tanzania huwezi kutaja matajiri watatu wakubwa na kuacha kumtaja Bakhressa, hata kama humpendi.

Pamoja na pesa zake, Bakhressa anapenda soka vilivyo. Humwambii kitu kuhusu soka. Miaka ya nyuma alikuwa shabiki wa kutupwa wa Simba, kiasi cha kuwa mmoja wa wafadhili walioisaidia klabu hiyo.

Kwa siku hizi ana timu yake ya Azam FC. Mapenzi haya ya soka yapo pia kwa watoto wake Yusuff na Aboubakar Bakhressa. Kwa kifupi ni kwamba familia yao ni ya watu wa soka.

Hata hivyo, licha ya mapenzi yake makubwa ya soka kuna watu wanamrudisha Bakhressa nyuma. Licha ya fedha zake nyingi anazotoa katika soka watu wanamrudisha nyuma. Hawa watu wapo katika makundi mawili.

Kundi la kwanza ni lile la watu wanaofanya usajili katika timu yake. Hawa watu ni tatizo kubwa na wamekuwa wakimpa hasara kubwa Bakhressa. Imefikia hatua unaona hata aibu kuwatazama.

Kwanza watu hawa wamekuwa na tatizo la kufahamu wachezaji wazuri hasa kwa upande wa wachezaji wa kigeni. Pili, watu hawa wamekuwa wakinunua wachezaji wa kawaida kwa fedha nyingi, bila kutazama soko linasemaje. Yaani unaweza kukuta mchezaji mwenye thamani ya Dola 20,000 ananunuliwa na Azam kwa Dola 50,000. Imekuwa ni jambo la kawaida. Sina hakina kama wanafanya hili kwa bahati mbaya ama kwa makusudi ili wapate chochote kitu

Msimu huu pekee Azam FC imesajili mastraika wawili, Gonazo Bi Ya Thomas na Fransesco Zekumbawira kutoka Zimbabwe na ndani ya miezi mitano tu walionekana si lolote si chochote na wakaachwa.

Hapa timu ilipata hasara mara mbili. Kwanza iliwasajili wachezaji hao kwa fedha nyingi na pili imelipa gharama kubwa kuvunja mikataba yao wakati ambapo hawajaitumikia timu hiyo hata kwa miezi sita iliyokamilika.

Katika dirisha dogo lililofungwa wiki mbili zilizopita Azam imelipa zaidi ya Sh 100 milioni kuvunja mikataba ya Jean Mugiraneza, Ya Thomas na Zekumbawira. Ni fedha nyingi hata kwa kuzitamka tu.

Huo ni mfano wa msimu huu pekee. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Azam iliwasajili Ismail Kone, Ismail Diara, Leonel Saint Preux, Allan Wanga, Brian Majwenga na Racine Diof kwa fedha nyingi lakini wote walishindwa kufanya vizuri na kuachwa. Ni jambo la aibu sana.

Watu hawa wanaofanya usajili Azam wanampa Bakhressa hasara kubwa. Inaumiza kwamba tajiri amejitolea kuwekeza katika soka halafu watu ambao wanalipwa mishahara mikubwa wanashindwa kuifanya kazi yao kwa ufasaha na kumrudisha nyuma.

Katika kipindi hicho cha miaka miwili ni Sergie Wawa na Didier Kavumbagu walioweza kusajiliwa Azam na kufanya vizuri, hii ni kwa upande wa wachezaji wa kigeni. Wengine wote waliletwa wakiwa hovyo.

Ilifikia hatua Azam ikawa inasajili wachezaji wagonjwa. Ismail Kone alisajiliwa akiwa na majeraha ya goti. Alikaa Chamazi kwa miezi sita yote akila chakula cha bure na hadi anatemwa alikuwa hajaisaidia timu hiyo katika kitu chochote. Katika hali ya kawaida timu inakubali vipi kusajili mchezaji mgonjwa?

Ismail Diara naye alisajiliwa akiwa majeruhi. Miezi yake ndani ya timu haikuwa na msaada wowote. Muda mwingi alishinda na daktari kuliko kocha. Ni jambo la kutia aibu sana.

Msimu uliopita Racine Diof alisajiliwa akiwa mgonjwa. Alicheza mechi tatu kisha akarejea benchi. Hata hivyo, baada ya hapo alitumia muda mwingi akiwa na daktrari kuliko kocha. Hadi mwisho wa msimu hakuwa amefanya la maana. Kwa nini tunazikatili fedha za Bakhressa kwa kiasi hiki? Kwa nini tunamtenda hivi Bakhressa?

Turejee katika upande wa pili wa kuajiri. Azam imeachana na makocha wao Wahispanyola wakiongozwa na Kocha Mkuu Zeben Hernandez.

Jopo hilo la makocha watano limetimuliwa miezi sita baada ya kuajiriwa. Hata hivyo, kocha kufukuzwa si habari sana lakini naomba tutazame mtiririko mzima wa kitengo hiki.

Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ni makocha wawili tu wa maana waliowahi kuajiriwa na Azam. Ni Stewart Hall na Joseph Omog, wengine ni vituko. Hall aliisaidia Azam kujenga msingi wa ubingwa msimu wa 2013/14 na baadaye Omog akaisaidia kubeba taji hilo.

Hall baadaye alirejea na kuipa Azam taji la Kagame. Ikumbukwe kwamba Hall amewahi pia kuisaidia Azam kufika hatua ya mwisho ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2012 na nusura ingefuzu hatua ya makundi.

Tofauti na makocha hawa wawili, unamfahamu kocha yupi mwingine wa Azam? Neider Do Santos, Itamar Amorim na Boris Bunjak wote walikuwa ovyo. Sitaki kuzungumza chochote kuhusu Zeben Hernandez na wenzake ambao wameondoka wakiiacha Azam katika nafasi ya tano katika Ligi Kuu.

Nadhani ifike wakati sasa watu wanaopewa fedha hizi nyingi na Bakhressa waziheshimu na kuzithamini. Hapa ndipo tutakapotengeneza msingi mzuri wa matajiri kuwekeza katika soka. Kama tutaendelea kucheza na fedha hizi za Bakhressa tutakuwa tunalirudisha nyuma soka letu.