Wanafiki wanaokaa jukwaa la VIP A na hadithi za Samatta

Muktasari:

Hii ni kauli ya kinafiki. Inakuja kutoka katika midomo ya viongozi wetu wa soka wa ngazi za klabu, hasa wale wa Simba na Yanga. Linapokuja suala la Taifa Stars wanatoa kauli tamu tamu. Mechi zinapoondoka wanakuwa wanadamu wengine kabisa.

WANAFIKI wanakaa juu pale katika jukwaa la VIP A. Wana suti nzuri kweli kweli. Wanamshangilia Mbwana Samatta katika ubora wake ndani ya timu ya taifa na katika klabu yake ya Genk. Mwisho kabisa utawasikia ‘Yaani tungepata akina Samatta sita tu tungekuwa mbali.’

Hii ni kauli ya kinafiki. Inakuja kutoka katika midomo ya viongozi wetu wa soka wa ngazi za klabu, hasa wale wa Simba na Yanga. Linapokuja suala la Taifa Stars wanatoa kauli tamu tamu. Mechi zinapoondoka wanakuwa wanadamu wengine kabisa.

Majuzi tu Simba walimkatalia Said Ndemla kwenda Sweden kufanya majaribio ya mwezi moja. Sababu kubwa nadhani lilikuwa pambano la Simba na Yanga. Baadaye ikasemwa kuwa Ndemla ni mchezaji muhimu kikosini.

Mwezi mmoja Simba wanaweza kucheza mechi nne tu. Kati ya hizo, Ndemla anaweza kukaa benchi mechi mbili. Niliongea na Thomas Ulimwengu alikuwa akimsubiri Ndemla kwa hamu pale Sweden. Nikamwambia asahau. Hakuamini. Nadhani nafasi yake itakwenda kwa mchezaji kutoka Ivory Coast, Ghana, Cameroon au kwingineko. Wazungu hawana muda wa kumsubiri mchezaji kutoka dunia ya tatu.

Watu hao hao wanaozuia dili ndio wanavaa suti na kwenda kuangalia mechi za Taifa Stars, huku wakitoa kauli hii ya kwamba ‘Tungekuwa na kina Samatta sita tungekuwa mbali’. Inatokea mara nyingi tu.

Mpaka leo wachezaji wetu wanatoroka kwenda kufanya majaribio. Sababu ni hii hii tu. Ukipeleka maombi ya kwenda kufanya majaribio utasikia; ‘Ngoja uongozi ukutane mwezi ujao’. Wengine utasikia wanamwambia mchezaji ‘Tukikuruhusu wewe unafikiri tutawaambia nini Wanachama’. Wakishindwa kikwazo hicho viongozi wetu wanaanza mambo ya ajabu. Huwa wanatangaza bei ya ajabu. Unaweza kuulizia bei ya Simon Msuva Yanga watakwambia anauzwa dola milioni moja. Ni bei ya kijinga ambayo sio thamani halisi ya Msuva, lakini ndio njia ya haraka zaidi ya kuzuia dili hilo lisifanyike ili Msuva abakie Yanga.

Iliwahi kutokea wakati fulani Mrisho Ngassa alitakiwa Norway. Timu iliyomtaka ilipiga hesabu kwamba Ngassa angeweza kupatikana kwa Dola 50,000 halafu baada ya hapo kama angeuzwa kwenda kwingineko basi Yanga na hiyo timu ya Norway zingegawana mapato.

Yanga wakaibuka na kutaka Dola 250,000. Bei ambayo haikuwa thamani ya Ngassa wakati huo. Miaka miwili baadaye wakamuuza Ngassa kwenda Azam kwa Sh 50 milioni. Baadaye Ngassa alirudi tena Yanga na walipoona kasi yake imepungua wakaruhusu amalize mkataba wake na wakamuacha huru kwenda Afrika Kusini huku miguu yake ikiwa haina kasi tena. Viongozi hawa hawa waliotaja bei ya ajabu kwa Ngassa alipotakiwa kwenda Norway ndio huwa wanakaa pale VIP A na suti zao halafu wanakwambia ‘Nchi hii ingekuwa na akina Samatta sita basi Taifa Stars ingekuwa mbali’. Huu ndio unafiki wetu wa Kitanzania. Ilikaribia kutokea hivi hivi kwa Farid Mussa alipokuwa Azam. Bahati nzuri kijana anajitambua na alipigana kufa na kupona kuhakikisha anakwenda kucheza Ulaya. Vinginevyo mpaka leo angekuwa anavaa jezi ya Azam FC.

Sio viongozi tu. Hata mashabiki na wachezaji wenyewe wana unafiki huu. Mashabiki wanaokwenda Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi za Taifa Stars huwa wanajifanya ni tofauti na mashabiki wanaokwenda kutazama mechi za Simba na Yanga au kwenda katika mikutano ya klabu zao. Wakiwa katika mechi za Taifa Stars huwa wanasema ‘Tungekuwa na kina Samatta sita tungekuwa mbali.’ Lakini ni hawa hawa mashabiki ndio huwa wanatamani kuona wachezaji hawa hawaondoki klabuni. Mchezaji staa akiondoka kikosini mashabiki wanamwaga lawama kwa uongozi. Kwa upande wa wachezaji nao usiwaamini kauli zao. Wao wana kauli zao maarufu katika siku za karibuni. Karibu wote utasikia; ‘Nataka kufuata nyayo za Samatta’. Hii ndio kauli yao maarufu siku hizi. Lakini ni mara ngapi unasikia mchezaji anatoa kauli hii halafu baada ya wiki mbili anasaini mkataba mpya kwa klabu yake.

Kifupi mchezaji huyu anakuwa anajifunga kwa viongozi wale wale ambao anajua wazi kwamba wakati ukifika watagoma kumuuza. Mchezaji anaangalia pesa mbele. Laiti kama angejua ni kiasi gani Samatta na Thomas Ulimwengu waliziacha kwa kutosaini mikataba mipya TP Mazembe ndipo angejua kuwa hatuwezi kuwa na Samatta sita katika kikosi cha Taifa Stars.