Wachezaji wawe makini dirisha la usajili linalokaribia

Muktasari:

Tayari tumeanza kusikia baadhi ya klabu na wachezaji wakichangamkia usajili kabla hata dirisha halijafunguliwa, siyo jambo baya ilimradi wale wanaotaka kutua katika klabu mpya hawabanwi kimkataba ili kuepuka kuingia matatani.

KUMALIZIKA kwa Ligi Kuu Bara msimu wa 2016-2017, inamaanisha kuanza kwa maandalizi ya msimu mpya wa 2017-2018.

Maandalizi hayo ya msimu mpya yataanza na kufunguliwa kwa dirisha kubwa la usajili ambapo, kwa sasa umeanza hata kabla ya kufunguliwa rasmi. Kipindi hiki ni neema kwa wachezaji, pia ni wakati wa wapiga dili kuvuna fedha kupitia migongo ya klabu na wachezaji wanaochangamkia usajili huo.

Tayari tumeanza kusikia baadhi ya klabu na wachezaji wakichangamkia usajili kabla hata dirisha halijafunguliwa, siyo jambo baya ilimradi wale wanaotaka kutua katika klabu mpya hawabanwi kimkataba ili kuepuka kuingia matatani.

Mwanaspoti halipendi yatokee kama yaliyomkumba beki, Hassan Kessy ama sakata la kina Mohammed Mkopi aliyetua Mbeya City wakati akibanwa na mkataba wake na klabu yake ya zamani ya Prisons na kumponza kufungiwa msimu mzima.

Licha ya kutaka umakini katika kukimbilia zoezi hilo la usajili hata kabla dirisha halijafunguliwa, lakini pia tulikuwa tunataka kuwakumbusha wachezaji kuwa makini katika kusaini mikataba wanayoingia na klabu zinazowataka kwa sasa.

Wachezaji wajaribu kuwashirikisha wanasheria ama watu wenye upeo mkubwa wa mambo ya mikataba kisheria, ili waisome na kuielewa mikataba wanayoletewa mbele yao kabla ya kuanguka saini.

Wasikurupuke kusaini bila kuelewa kile wanachokisaini kwa sababu tu, wameahidiwa kulipwa mamilioni ya fedha. Kukurupuka kwao na kusaini kwa pupa ndiko ambako kumekuwa kukiwagharimu wachezaji mbele ya safari mambo yakiharibika.

Mkataba ni mafungamano ya kisheria na ni vema kila mmoja kusoma na kuielewa na kama kuna vipengele ambavyo havipo sawa ni wajibu wao kuomba virekebishwe ili kila upande uridhie na kutomnyonya mwenzake.

Lakini, bahati mbaya ni kwamba wachezaji wengi wamekuwa wakisainishwa mikataba na klabu bila ya kusimamiwa na wanasheria au watu ambao, wanapaswa kuwa mashahidi kwa kile wanachokisainia baada ya kueleweshwa vyema.

Mwishowe hujikuta wakibanwa kisheria inapotokea pande mbili kushindwa kuelewana na kukiukwa kwa baadhi ya vipengele ambavyo kisheria wakati mwingine hufanya mkataba husika kuvunjika rasmi.

Mbali na kutaka wachezaji kuwa makini na kile wanachokisaini, pia ni vizuri wakawa na utamaduni wa kupewa nakala ya mkataba huo ili uje kuwasaidia pale mambo yanayoenda kombo kwa ajili ya kutunza kumbukumbu yao.

Baadhi ya viongozi wa klabu huwa sio waaminifu, wamekuwa wakiwageuza wachezaji kama watoto wadogo kwa kuwasainisha mikataba mingine na kile kinachoenda kutunzwa mikononi mwao huwa kitu kingine. Hii imefanyika mara kadhaa na kuzua utata mkubwa kwenye migogoro ya wachezaji mbalimbali hadi kulifanya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuingilia kati kuamua mzozo wa aina hiyo.

Ndio maana tunawakumbusha wachezaji na watu wanaowasimamia kuwa makini na hila za baadhi ya viongozi wa klabu ambao wamekuwa na kauli mbilimbili na wakati mwingine kutaka kuwaingiza mkenge wachezaji wasio makini katika suala zima la kusaini mikataba.

Wachezaji na wasimamizi wao, hata wakati wanapokuwa wameshaisoma na kuiewela kabla ya kusaini wairudie kusoma nakala moja moja ili kuona kama kweli zinawiana, kusudi wasije wakasainishwa mikataba miwili tofauti bila ya wao kujua.

Wasikubali kupumbazwa na maburungutu ya fedha wanayowekewa mezani kabla ya kusaini, ingawa kwa sasa jambo hilo halifanyiki kama ilivyokuwa miaka michache iliyopita wachezaji walipowekewa fedha mezani wakati wa kusaini mikataba yao.

Wachezaji na wasimamizi wao lazima wawe makini kabla ya kusaini mikataba kwa vile hayo ni mafungano ambayo kama yakija kukiukwa huleta shida kwa mhusika kutokana na ukweli yeye ndiye aliyesaini kuonyesha ameafiki kila kilichopo ndani.

Mwanaspoti inaamini kama wachezaji watazingatia ushauri huu na viongozi nao wakafanya usajili wao kwa umakini bila ya hila yoyote ni wazi hatutarajii kusikia mizozo ya mikataba mbele ya safari kama pande mbili zikitaka kuachana kwa hiari.

Muhimu kila upande uheshimu na kutekeleza kwa ufanisi makubaliano na vipengele vilivyomo kwenye mikataba hiyo waliyoisaini, ili kuepuka mizozo isiyo ya maana sambamba na kuepuka hali ya unyonyaji baina ya pande zilizokubaliana kama ambavyo imekuwa ikishuhudiwa kila mara kutokana na kukosekana umakini.

Mara nyingi wachezaji ndio wamejikuta wakiwa wahanga wa kudhulumiwa au kunyonywa jasho lao pale inapotokea mzozo baina yao klabu, lakini hii inatokana na kule kukimbilia kusaini mikataba husika bila kuisoma kwa makini na kuielewa.