Waamuzi wasiwe chanzo cha vurugu viwanjani

Friday March 3 2017CHIRWA

CHIRWA 

MASHABIKI wa soka hasa wa klabu ya Yanga bado hawafahamu mpaka sasa kitu gani kilichotokea Uwanja wa Taifa, mpaka mwamuzi Ahmed Simba akalikataa bao la straika wao Mzambia, Obrey Chirwa.

Pia, hawafahamu ni kwa nini mwamuzi huyo alimuonyesha kadi ya njano Chirwa mara baada ya kulikataa bao lake la kichwa, ambalo lilikuwa likiipa Yanga uongozi wa mabao 2-0 kabla ya kwenda mapumziko.

Kila shabiki aliyekuwa uwanjani na hata waliofuatilia pambano hilo kupitia matangazo ya runinga, hawafahamu kilichotokea na labda hata kamisaa wa mchezo huo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Ruvu Shooting bao anajiuliza.

Ndio! Hii ni kwa sababu haikuonekana kama Chirwa alifanya madhambi yoyote aliporuka hewani na kutumbukiza mpira kimiani langoni mwa Ruvu.

Krosi iliyopigwa ilikuwa ya wazi na ndio maana haikuwa ajabu kipa wa maafande hao Bidii Hussein, ambaye alionekana kuwalaumu mabeki wake kwa uzembe walioufanya na kumruhusu straika huyo kufunga bao hilo kwa kichwa tena akiwa peke yake.

Inawezekana mwamuzi aliona labda Chirwa aliutumbukiza mpira kwa mkono, inawezekana ndivyo jicho lake lilivyoona, lakini waliokuwa uwanjani na hata wachezaji walishindwa kufahamu kilichomfanya Simba kukataa bao lile kisha kumzawadia kadi ya njano.

Lakini, kwa kuwa waamuzi ni binadamu, inawezekana amefanya kosa la kibinadamu kwa kuamua kulikata bao la Chirwa ni kama ambavyo Martin Saanya alivyolikataa bao lililoonekana halali la Ibrahim Ajib katika mechi ya kwanza ya watani, Oktoba Mosi, mwaka jana. Haya yote hutokea uwanjani.

Hata hivyo, Mwanaspoti kama wadau wa michezo nchini, tulikuwa tunatoa rai kwa waamuzi kuwa makini viwanjani ili kuepusha kuibuka kwa vurugu na machafuko yasiyo ya lazima.

Oktoba Mosi, mashabiki wa Simba walishindwa kuvumilia maamuzi ya Saanya na kuamua kuvunja na kung’oa viti uwanjani.

Mbali na kukata bao hilo la Ajib, Saanya pia aliruhusu bao la Amisi Tambwe, ambaye kabla ya kupachika mpira wavuni mwa Simba, aliuchota kwa mkono na kuuweka sawa mguuni kisha kufunga kistadi kabisa.

Walichokifanya sio jambo zuri na wala halikubaliki katika jamii ya wastaarabu na wanamichezo kwa ujumla, lakini kuna wakati mihemko na jazba za mashabiki zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na umakini mdogo wa waamuzi wetu waliopewa dhamana.

Kwa hali iliyotokea juzi Uwanja wa Taifa iwapo mashabiki wa Yanga wangehamaki kwa kilichofanywa na Simba hali ingekuwaje uwanjani hapo?.

Bila ya shaka kungetokea vurugu ambazo zingechafua taswira ya soka letu kama lilivyochafuliwa kwa matukio ya vurugu katika Ligi Daraja la Kwanza kwa baadhi ya michezo kutokana na waamuzi kufanya makosa ya wazi kabisa katika maamuzi.

Ifike wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kamati ya Waamuzi kuhakikisha inakuwa makini katika kupanga waamuzi wa kuzichezesha mechi hizi za kuelekea mwishoni mwa msimu.

Hizi ni mechi za lawama na zinazoweza kuchafua soka letu kutokana na maamuzi yenye utata kama yaliyojitojkeza kwenye mechi za mwishoni mwa Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Tunarudia tena kusema waamuzi ni binadamu kama binadamu wengine na kuna wakati hukosea kutokana na udhaifu wa kibinadamu, lakini ni vema kusisitizwa umakini zaidi uwanjani ili kutoivuruga Ligi Kuu na soka la Tanzania kwa ujumla.

Ikumbukwe kwamba mamuzi mabovu ya waamuzi wetu hayasababishi vurugu pekee uwanjani, bali husababisha soka kuzorota na kukosa msisimko. Kwa mantiki hiyo basi, TFF haina budi kuwa makini na waamuzi ili kuongeza hamasa na ushindani uwanjani.