Viwanja vikiboreshwa, soka letu litainuka

Muktasari:

  • Ili soka na hata michezo mingine iweze kusonga mbele inahitajika mambo ya msingi, ikiwamo utawala bora, uwekezaji, makocha, waamuzi na wadau wengine sambamba na miundombinu rafiki kuwezesha vipaji kuendelezwa tangu utotoni.

SOKA ni moja ya michezo inayoshabikiwa na kupendwa na watu wengi duniani, hata Tanzania soka ndiyo mchezo unaoshika nafasi ya kwanza kwa kupendwa na mashabiki wa michezo.

Kwa namna soka linavyovutia wengi, hata baadhi ya mataifa ambayo yaliupa kisogo mchezo huo kama India na Marekani leo wamekumbatia soka na kuanza kupenya katika mioyo ya raia wa nchi hizo. 

Ili soka na hata michezo mingine iweze kusonga mbele inahitajika mambo ya msingi, ikiwamo utawala bora, uwekezaji, makocha, waamuzi na wadau wengine sambamba na miundombinu rafiki kuwezesha vipaji kuendelezwa tangu utotoni.

Suala la viwanja ni jambo la msingi zaidi kwa vile hata kama vipaji vitakuwepo, makocha wakiwepo na utawala mzuri sambamba na uwekezaji wa kutosha bado hivyo vyote haviwezi kufanikisha bila viwanja. Katika viwanjani ndipo wachezaji hufunzwa soka tangu wakiwa wadogo kama hakunaviwanja au havina ubora ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu.

Hakuna uwezekano wa kupata maendeleo katika mchezo husika kama hakuna viwanja labda tu kwa kuishi kwa mazoea kama ilivyo kwa sasa nchini, wachezaji wenye vipaji wanaishi na kucheza katika viwanja vya soka kwa mtindo wa bora liende.

Mara kadhaa wachezaji waliozoea kucheza kwenye viwanja vibovu wanapata tabu kutandaza soka kwenye viwanja bora na vya kisasa kama vya Taifa, Uhuru ama Chamazi na sasa Kaitaba mjini Bukoba.

Hakuna ubishi kwamba viwanja vingi vinavyotumiwa na soka letu, hasa kwa Ligi Kuu na Daraja la Kwanza, havistahili kwa kuwa miundombinu yake mpaka eneo la kuchezea (pitch) ni ovyo.

Kelele zimekuwa nyingi, lakini ni kama hazisikiki na kwa bahati mbaya ni kwamba asilimia kubwa ya viwanja vinavyotumiwa kwenye ligi za nchi yetu vinamilikiwa na Chama Tawala, CCM, lakini wenyewe ni kama wamevitelekeza.

Hata hivyo, kuna juhudi kubwa zimekuwa zikifanywa miaka ya karibuni angalau kuboresha baadhi ya viwanja vya soka kama ilivyotokea kwa Uhuru jijini Dar es Salaam, Kaitaba Bukoba na sasa Nyamagana Mwanza.

Ukiacha Uwanja wa Uhuru, viwanja vingine vimeboreshwa kwa kuwekwa nyasi bandia kwa msaada wa fedha za Shirikisho la Soka Duniani, Fifa ikishirikiana na vyama vya soka vya mikoa husika, kitu ambacho kuna haja ukarabati kama huo kuhamia kwa viwanja vingine vikiwamo vilivyo chini ya CCM.

Tunaamini kama kila mkoa ukiwa na kiwanja kimoja kizuri cha kuruhusu kuchezwa mechi za Ligi na hata michuano ya kimataifa, kutasaidia kulisongesha  mbele soka la Tanzania.

Hivyo Mwanaspoti inatoa wito kwa wamiliki wa viwanja na hata serikali za mikoa kuvikumbuka viwanja vilivyo katika maeneo yao ili kuviboresha na kurahisisha soka na michezo mingine kuchezwa kwa ufanisi.

Soka kwa sasa ni ajira, kadhalika wamiliki wanaweza kuchuma fedha za kutosha kupitia vitega uchumi hivyo vya viwanja, badala ya kusubiri kukusanya mapato ya mechi tu. Kwa mfano haieleweki inakuwaje Uwanja wa kisasa kama wa Ali Hassan Mwinyi Tabora ama CCM Kirumba, Mwanza na Sheikh Amri Abeid Arusha vimeachwa vichakae wakati ni hazina kubwa ya kuchuma fedha na kusaidia kuinua soka letu.

Inawezekana wamiliki hawaoni umuhimu wa viwanja hivyo kwa sasa kwa sababu ofisi na majengo yaliyovizunguka viwanja hivyo vinawaingizia kodi kwa wale waliowapangisha, lakini kumbe viwanja vikiboreshwa zaidi vinaweza kushawishi hata kutumika kwa michezo ya kimataifa na kuwaingizia fedha zaidi.

Ndiyo maana tunakumbusha wasimamizi wa soka, serikali na wamiliki wa viwanja vinavyotegemewa kwa mechi za ligi mbalimbali kuboresha viwanja vyao.