Vita vya dawa za kulevya ihamishiwe kwenye michezo

Muktasari:

  • Hii ni vita ngumu ambayo inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania mwenye nia njema dhidi ya kizazi kilichopo na kijacho kutokana na ukweli dawa hizi zimekuwa zikiteketeza nguvu kazi na wazalishaji mali wa taifa.

KWA wiki ya pili sasa mjadala mkuu nchini na hasa viunga vya Jiji la Dar es Salaam ni vita vilivyoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda dhidi ya dawa za kulevya.

Wasanii mbalimbali na watu wengine maarufu wamekuwa wakitajwa kuhusishwa na dawa za kulevya, baadhi yao kwa sasa wakisota korokoroni baada ya kufunguliwa mashtaka kwa kukutwa na vithibiti katika maeneo yao.

Hii ni vita ngumu ambayo inapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania mwenye nia njema dhidi ya kizazi kilichopo na kijacho kutokana na ukweli dawa hizi zimekuwa zikiteketeza nguvu kazi na wazalishaji mali wa taifa. Kwa muda mrefu wasanii wamekuwa wakitajwa kama wahanga wakubwa wa dawa hizi kuanzia kutumia mpaka kutumika kubeba wakitumiwa na wafanyabiashara wa dawa hizo, japo imekuwa ngumu kupatikana ushahidi.

Baadhi ya wasanii wametajwa kuwahi kupoteza uhai kwa sababu ya ‘unga’ na wengine kufungwa nje ya nchi kutokana na kubambwa wakisafirisha unga, lakini bado haijaweza kuwatisha wengine kujihusisha na biashara hiyo.

Imani yetu ni kwamba kilichoanzishwa na Makonda kitaendelezwa na kuungwa mkono na Watanzania wote, lakini tulikuwa hatutaki vita hiyo iishie kwa wasanii tu. Vita hiyo igeukie pia kwenye michezo kwa nia ya kuwanusuru wachezaji wetu dhidi ya janga hilo la kitaifa.

Sekta ya michezo kama ilivyo kwa sanaa nayo imekuwa ikiathirika kutokana na wanamichezo kudaiwa kujihusisha na dawa za kulevya ama kwa kutumia ama kutumika kusafirisha na kusambaza kwa usiri mkubwa.

Wapo baadhi ya wachezaji wamekuwa wakidaiwa kuporomosha viwango vyao kwa sababu ya unga, kuna wengine wanakiri kutumia vilevi hivyo hasa bangi kiasi cha kufanya mambo ya ajabu.

Hata kwenye viwanja vya soka, biashara ya mihadarati hasa bangi imekuwa ikifanyika pasi na usiri wowote, ni kama vile imehalalishwa na wengine wanapuliza bangi mbele ya watoto wanaohudhuria viwanjani.

Achana na viwanja vinavyotumika kwa mechi za mchangani, hata katika mechi za ligi ngazi mbalimbali ulevi huo umekuwa ukitumika hadharani na biashaa kufanywa mbele ya macho ya watu bila hatua zozote kuchukuliwa. Wachezaji wamekuwa wahanga wakubwa wa biashara hiyo kwa kutumia vilevi hivyo na wakati mwingine kuchangia kushusha viwango vyao na kuwa sababu ya kuporomoka kwa soka letu, licha ya mikakati mingi ya kuiendeleza. Katika ngumi nako kunatajwa ndio kwenye balaa zaidi, biashara ya dawa za kulevya zinafanywa bila kificho na mabondia wanatumia sana vilevi hivyo, hasa bangi na ndiyo maana wanamichezo wake hawasomeki mbele ya jamii.

Skendo zilizowahi kulitia aibu taifa la mabondia wake wa timu ya taifa kukamatwa na dawa za kulevya nchini Mauritius ni uthibitisho juu ya kile tunachokisema.

Kifupi ni kwamba kama mapambano yameanzia kwa wasanii, kwa sasa ni zamu ya kuhamishwa kwenye michezo kwa nia ya kuokoa vijana wanaoangamizwa na kujiangamiza wenyewe kwa sababu ya dawa za kulevya.

Hivi karibuni Chama cha Kuzuia Dawa Haramu Michezoni Duniani (Wada) kiliendesha semina na wadau wa michezo nchini, ikiwa na lengo la kutoa elimu na kuhamasisha wanamichezo kuepukana na matumizi ya dawa haramu.

Inawezekana sio kila mwanamichezo alifanikiwa kuhudhuria semina hiyo ama kupewa elimu juu ya tatizo hilo, lakini kama kilichohamishwa na Makonda kitahamia michezoni ni wazi tutawaokoa wengi.

Kufumbiwa macho kwa tatizo hilo michezoni kutaendelea kutuvurugia vijana wetu na kupoteza vipaji ambavyo vingekuwa na manufaa kwa taifa katika ushiriki wa michuano mbalimbali ya kimataifa.

Vipaji vilivyokatishwa makali yao kwa sababu ya ‘unga’ ni mfano wa athari za dawa za kulevya, kukamatwa na kufungwa kwa baadhi ya wanamichezo wetu katika nchi za watu ni aibu kwa taifa na kuonyesha namna gani tusivyo makini.

Tukemee, tulaani na kushirikiana kupambana ili kuhakikisha kauli ya Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana kwa kuibadilisha ili kwa sasa kuwa, michezo bila dawa za kulevya inawezekana. Tushirikiane kupambana sasa.