Vipigo vya Barca, Arsenal funzo tosha kwa klabu zetu

Friday February 17 2017

 

By MWANASPOTI

KLABU za Simba na Yanga zenye umri mrefu tangu kuasisiwa kwao na zenye mafanikio makubwa miongoni mwa klabu za Tanzania, wiki ijayo zinatarajiwa kuvaana kwenye pambano lao marudiano ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

Timu hizo zenye mashabiki wengi ndani na nje ya nchi zitapepetana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Februari 25, baada ya awali pambano lao la kwanza lililopigwa Oktoba Mosi, mwaka jana kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mechi hiyo ya kwanza ilijaa matukio tata na kusababisha mashabiki wa klabu zote kufanya fujo na kuleta uharibifu mkubwa ya miundo mbinu ya uwanja huo.

Mashabiki wa Yanga walivunja mageti wakati wa kuingia uwanjani na wale wa Simba kuvunja viti zaidi ya 1500 kutokana na kupinga bao linalodaiwa kuwa la mkono la Amissi Tambwe wa Yanga na kadi nyekundu ya nahodha wao, Jonas Mkude.

Kadi hiyo kwa bahati nzuri ilifutwa siku chache baada ya Kamati ya Saa 72 kukutana kuutathmini mchezo huo na kumsimamisha mwamuzi aliyeuchezesha, Martin Saanya kwa kubainika alishindwa kulimudu pambano hilo la watani.

Wakati mashabiki, viongozi, wachezaji na wanachama wakianza kutambiana kuelekea pambano hilo, barani Ulaya katikati ya wiki hii kumechezwa mechi za awali za mtoano za Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Barcelona ya Hispania ikiwa na nyota wote uwanjani, walijikuta wakichezea kichapo cha mabao 4-0 toka kwa PSG ya Ufaransa, kabla ya juzi Jumatano Arsenal ikiwa ugenini nchini Ujerumani ilifumuliwa 5-1 na Bayern Munich.

Kila shabiki wa soka hakutarajia matokeo ya aina hiyo kwa timu hizo mbili mbili za Barca na Arsenal zinazosifiwa kwa kucheza soka la kuvutia na la kiufundi, lakini kwa kuwa soka ni mchezo wenye matokeo ya kikatili, ndivyo ilivyokuwa.

Matokeo hayo yanatoa funzo kubwa kwa klabu zetu hasa Simba na Yanga ambazo huwa hazina utamaduni wa kukubali na kuamini kuwa kama timu zao zinaweza kufungwa ama kupata matokeo ya kustaajabisha kama hayo.

Klabu hizo zimekuwa zikijiaminisha kuwa, timu zao ni bora na zisizofungika na ikitokea ikapoteza mechi iwe kwa idadi kubwa ya mabao kama ilivyopigwa Barcelona na Arsenal, basi lazima hali ya hewa ichafukwe katika klabu hizo.

Tuhuma za kuhujumiana na kusaka mchawi ama kutimua makocha ni mambo ya kawaida. Tuliona kwenye duru la kwanza vipigo viwili mfululizo ilivyopanda Simba kwenye mechi zao za mwisho za duru la kwanza kulivyozua mapya. Baadhi ya wachezaji walituhumiwa kabla ya kipa Vincent Angban kutimuliwa katika dirisha dogo na nafasi yake kuchukuliwa na Mghana Daniel Agyei. Yanga wenyewe walishawahi kuwatimua makocha wao, Ernie Brandts na Marcio Maximo kwa sababu ya vipigo  kutoka kwa Simba katika mechi za bonanza lililokufa baada ya miaka miwili ya kutamba la  Nani Mtani Jembe. Makocha na wachezaji wanakuwa kwenye mtihani mkubwa mara baada ya matokeo ya mechi ya watani wa jadi kama hiyo inayokuja, hakuna aliye tayari kukubali kuwa katika soka kuna matokeo matatu yasiyokwepeka.

Ni lazima viongozi, wanachama na mashabiki wa klabu hizo kujiuliza kama Barcelona yenye Lionel Messi, Neymar, Luis Suarez ama Arsenal yenye Alexis Sanchez, Olivier Giroud, Theo Walcot, Mesut Ozil na  nyota wengine watambao duniani wamepigwa na wapinzani wao, je wao ni kina nani hata wasifungwe?

Soka ndivyo lilivyo, hata ukiwa na kikosi imara kiasi gani, timu moja ikifanya makosa uwanjani ni lazima iadhibiwe kama ilivyoadhibiwa Barcelona, Arsenal na klabu nyingine zinazoshuhudiwa zikifungwa bila mashabiki wengi kutarajia.

Kwa wenzetu wanatambua kufungwa, kushinda ama kutoka sare ni matokeo yaliyopo ndani ya uwanja na huikumba klabu yoyote, lakini kwetu mashabiki na hata viongozi wao wanataka ushindi tu, kitu ambacho hakipo sawa. Hii ndio sababu inayofanya usisikie ulalamishi na lawama kwa wachezaji ama makocha pale timu zao zinapofungwa, tofauti na ilivyo kwa klabu zetu hasa Simba na Yanga.

Ndio maana Mwanaspoti linazikumbusha klabu za Simba na Yanga kuwa zipate somo kubwa kupitia matokeo ya mechi za klabu za Ulaya.