VPL isiwe na mizengwe, TFF mjipange

Muktasari:

  • Kabla hata ya kuanza tayari Shirikisho la Soka nchini (TFF) limefanya mabadiliko ya ratiba kwa kile kilichoelezwa kwamba, ni kutokamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Kaitaba uliopo mkoani Kagera.

LIGI Kuu Bara inatarajia kuanza keshokutwa Jumamosi katika viwanja tofauti hapa nchini, timu zimesajili na zimefanya maandalizi ya kutosha ili kuleta ushindani mkubwa ambao utapelekea kumpata bingwa anayestahili.

Kabla hata ya kuanza tayari Shirikisho la Soka nchini (TFF) limefanya mabadiliko ya ratiba kwa kile kilichoelezwa kwamba, ni kutokamilika kwa ujenzi wa Uwanja wa Kaitaba uliopo mkoani Kagera.

Hivyo baadhi ya mechi zimepanguliwa hazitaanza siku hiyo na zitachezwa kwenye uwanja mwingine hasa wa CCM Kambarage uliopo Shinyanga.

Mechi nyingi zilizopanguliwa ni zile zilipangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba ambao upo katika hatua za mwisho na imeelezwa utamalizika ndani ya wiki mbili ama tatu zijazo, pia mechi za Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Inawezekana ni jambo jema lililofanywa na TFF kwani wametoa taarifa mapema, lakini naamini pia Bodi ya Ligi na wanaosimamia uandaaji wa ratiba hiyo wameangalia kwa umakini mkubwa juu ya ratiba nyingine zilizopo mbele kwenye michuano mingine ya kimataifa ambayo itahusisha timu zilizofuzu ikiwemo pia michuano ambayo pengine Taifa Stars itashiriki.

Msimu uliopita ratiba ya VPL ilituvuruga sana, ilichukiza mno na hakuna aliyeipenda kutokana na kubadilishwa mara kwa mara na kupelekea ligi kutokuwa na mvuto, hivyo basi TFF inapaswa kuzingatia umakini katika ratiba ya msimu ujao kwa kutoivuruga kama msimu uliopita.

Wengi walishuhudia hata ruhusa za timu ambazo hazikuwa na mashiko ambazo zilipelekea kuchangia kuharibu ratiba ya ligi. Naamini msimu huu kila kitu kitazingatia weledi na michuano husika itaendeshwa kwa kufuata taratibu bila kuathiri mwenendo wa ligi.

Lakini pia naamini kwa upande wa waamuzi, kama msimu uliopita walivurunda basi wanapaswa kujitathimini upya juu ya utendaji wao wa kazi.

Ni vyema mwamuzi asiye na sifa asichezeshe mechi ama yule mwenye wasiwasi na harufu ya rushwa akawekwa kando mapema ili kuondoa malalamiko ambayo kwa kiasi fulani hupunguza utamu wa soka kuanzia VPL hadi FDL.

Mengi yalitokea kwa upande wa waamuzi ambao hawakuzingatia maadili yao hivyo hayapaswi kujirudia tena, yanaharibu ladha ya michezo na kujiondolea uaminifu kwa mashabiki.

Lingine ni makocha wa timu za VPL wajaribu kuwa na busara na kuacha kulalamikia waamuzi pale wanapopata matokeo mabaya, ni mara chache makocha kuwasifu waamuzi waliochezesha mechi yao pale wanapopata matokeo mazuri, mara kadhaa wakifungwa huwalalamikia waamuzi.

Huwa siamini sana kama waamuzi pekee ndiyo wenye mapungufu katika uchezeshaji bali hata makosa wana kasoro zao kwani, muda mwingine vikosi vyao vinakuwa si imara wala vyenye ushindani katika mechi na kupata matokeo mabovu lakini huwa wanakimbilia kuwalaumu waamuzi.

Makocha wanaojiamini na vikosi vyao wanapokosea huwa wanakiri udhaifu wa na wala huwezi kusikia wakiwalalamikia waamuzi na kikubwa ni kujipanga upya.