Utakuwa mwongo kwenye mapenzi hadi lini? (2)

Muktasari:

  • Kabla hujaendelea kusoma mbele jiulize je una wapenzi wangapi? Je, simu yako unaweza kumpa mkeo au mumeo bila wewe kuwa na presha?

Katika toleo lililopita tuliangalia hali ilivyo kwa baadhi ya wenye wenza. Ukweli ni kwamba kuna baadhi ya watu wamekuwa wakiendekeza sana uongo katika mapenzi.

Kabla hujaendelea kusoma mbele jiulize je una wapenzi wangapi? Je, simu yako unaweza kumpa mkeo au mumeo bila wewe kuwa na presha?

Ikiwa unaweza kumpa mumeo au mkeo bila wewe kuwa na hofu yoyote, hiyo ni ishara nzuri katika maisha.

Watu walio wengi si waaminifu, kiasi kwamba wanajikuta wanaishi maisha magumu kwa kuweka namba za siri na mambo mengine yanayowafanya waonekane wazi kwamba si waaminifu.

Kama kweli unahitaji kuwa na uhusiano mzuri katika maisha, jitahidi sana kuwa mkweli katika mapenzi.

Unaweza kuringa kwa sababu labda wewe ni mzuri kwa hiyo unaona kwamba unayo haki ya kuwa na wanaume au wanawake wengi, lakini siyo kweli kwamba duniani kote watu wameolewa au wamekuoa wewe….ninachotaka kusema hapa ni kwamba unapokuwa na mwenza, jitahidi kuonyesha upendo kwake, onyesha kumjali, onyesha kutenda haki kwake.

Kuna wengine wanajifanya wakimya, lakini wana lugha chafu kana kwamba wametoka kwenye shimo la choo. Ni wiki mbili tu zilizopita kuna mama mmoja alimchukua binti kanisani awe mfanyakazi wake wa ndani.

Huyo binti alikwenda kanisani, kweli walikuwa wakimsifia kuwa ni mzuri kwa namna alivyokuwa akionekana....siku moja kwa bahati mbaya bosi wake alipata safari ghafla kiasi kwamba aliacha fedha kidogo nyumbani.

Akiwa huko mbali na nyumbani akapata ujumbe mfupi kutoka kwa mfanyakazi huyo wa ndani ??ndio fedha gani hiyo umeniachia, mimi huwa sinywi maji ya bomba, nitumie fedha ya kutosha ninunue maji ya dukani, nikinywa ya bomba tumbo linauma?

Huo ni ujumbe wa kutoka kwa binti ambaye kanisani anaonekana ni mtakatifu. Kama hiyo haitoshi wakati bosi wake yuko mbali ikabainika akawa analala na kijana mmoja wa mtaani hapo, bosi akalazimika kumfukuza kwa sababu ya kuona anakwenda kinyume na alivyokuwa akimtarajia.

Unafiki hauko tu katika mapenzi, bali hata maofisini, mwingine anaweza kukuchekea na ukaamini ni rafiki, kumbe anakuchimba...eeeh bwana wengine ni maarufu wa kutangaza mabaya ya wenzao, huku wao wakijiona ni watu safi, wajuaji wa mambo nk.

Ndugu zangu katika maisha ni vizuri kuwa kama ulivyo, simamia kwenye ukweli wala usikubali kuingia kwenye uongo ili upate hiki na kile, maisha tunayoishi ni mafupi, uko leo, hujui kama kesho utafika, yanini kuwa mnafiki? Yanini kusengenya wengine? Yanini kuwa mtu wa majungu, badala ya kuangalia mambo yako ambayo yatakusaidia uwe na maisha bora zaidi kuliko ulivyo sasa?

Tangu mwezi huu uanze hadi leo unaposoma mada hii umeshateta watu wangapi? Umeshafanya unafiki mara ngapi? Je, kati ya maneno unayozungumza kwa siku, mengi ni ya aina gani....unafiki, uongo au heri kwa wengine? Mimi sijui, lakini wewe unalo jibu, lakini kwa vyovyote itakavyokuwa ni vizuri katika maisha pendelea kuachana na tabia za kinafiki.

Si masikini wala si tajiri, wote kwa pamoja wanahitaji mapenzi kutoka kwa wanaowapenda ili dunia iweze kwenda sawa kwa upande wao. Mapenzi yanapofanyika kwa usahihi kwa maana ya wapenzi wanapojaliana, maisha ya wenza kwa ujumla huwa ni bora zaidi.

Ukipata mpenzi anayekuelewa na kukupenda basi hata dunia iwe ya tabu vipi kwako utaiona inazunguka kama kawaida na maisha yatasonga mbele kwako kwa raha mustarehe, na hata matatizo mengine makubwa kwako huwa madogo kwa sababu tu unapenda na kupendwa kwa dhati.

Ukiumizwa kwenye mapenzi au kutojaliwa kama wewe unavyojali basi hata dunia iwe na raha gani kwako utaiona chungu na hata raha ya maisha hutakuwa nayo hata kama una hela kiasi gani na hata kama una cheo kikubwa kama mfalme au hata rais.

Wengine hufikia hatu ya kuteseka tu bila kuondoka kwenye mahusiano kwa kuogopa kuumizwa tena huko waendapo na wengine huondokawakiwa tayari wamechelewa.

Ninachotaka kusisitiza ni kwamba hakuna kitu kibaya kama uongo kwenye mapenzi, uongo wa aina yoyote ile si mzuri kwa wanaopendana kwa dhati kwa sababu huweza kupunguza mapenzi na uaminifu kwa kiasi kikubwa sana miongoni mwa wanaopendana hasa kama mmojawapo akigundua kuwa mwenzi wake ni muongo/anamdanganya.

Kuna vitu vingine hata kudanganyana haileti maana wala haina tija, kwa hiyo kuwa mkweli kwa mpenzi wako kwa lolote lile ni jambo jema sana kuliko kuwa unamdanganya kila siku hadi aje kugundua unamdanganya itakuwa matatizo na unaweza kusababisha kuachana.

Aidha miongoni mwa vitu hatari pia kwenye mahusiano ni pamoja na hili la usiri wa kupitiliza. Kama una vitu moyoni na upo kwenye mapenzi/mahusiano bora kabisa si vizuri kuvificha na hasa vile vinavyohusiana na mapenzi yenu moja kwa moja.

Ni kweli kuna vingine huwezi kumwambia kwa sababu havina mahusiano ya moja kwa moja na mahusiano yenu ila kuna vingine ni lazima avijue ili kutoleta ugomvi au matatizo hao baadae.

Kama kuna kitu hukuwahi kumwambia na unahisi ukimwambia atakasirika ni bora umtafutie nafasi nzuri umwambie kuliko aje kugundua mwenyewe itakuwa shida sana kukuelewa, kwa mfano mpo kwenye mahusiano mwaka wa 4 sasa na kumbe kabla ya kuwa na yeye ulishawahi kuoa/kuolewa na una watoto wawili kwa huyo mke/mume wa mwanzo ni bora umwambie kuliko kumficha, anaweza kukuelewa lakini mara nyingi ni kwa shingo upande.

Huna sababu yoyote ya kuwa na pesa na mpenzi wako akawa anapata tabu kama vile humuoni. Sijasema utoe pesa hata kwa mambo yasiyo na msingi lakini at least utimize majukumu yako kwa mpenzi wako kila unapohitajika.

Kuna vitu vingine hata huhitaji kuambiwa kama unatakiwa kuvishughulikia, ni wewe mwenyewe tu kuwa responsible kumhudumia mpenzi wako. Na hii huwa ina-apply sana kwa wavulana kutokana na kasumba iliyojengeka na mila tulizozikuta.

Ninachotaka kusisitiza katika makala hii ni kwamba ni suala la msingi sana kwa wanandoa kushirikiana na kufanyiana vitu ambavyo kweli vina maana katika maisha yao.

Kila siku, kila mwenye mwenza anapaswa kujiuliza je anayofanya kweli yana msaada kwa mwenzi wake. Je, unayofanya ungependa kufanyiwa? Kama ukipata jibu SIYO, acha kuyafanya. Jione una deni la kumfanyia mwenzi wako mambo yaliyo mema.

Makala hii imeandikwa na Dismas Lyassa 0754 498972