Uongozi Yanga, ufikirie kwa makini kuhusu uwanja

Muktasari:

  • Ingawa haijafahamika ujenzi huo ungeanza lini, lakini ni kwamba Yanga tayari ilikuwa na uhakika wa kumiliki uwanja baada ya miaka mingi ya kutangatanga

MWISHONI mwa mwezi uliopita, Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji alitoa eneo lake lililopo Gezaulole, Kigamboni pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuruhusu ujenzi wa Uwanja wa klabu hiyo.

Inaelezwa kuwa eneo hilo ambalo jiwe la msingi lilizinduliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Mama Fatma Karume, mmoja ya Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini na walezi wa klabu hiyo, litajengwa Uwanja wa Kisasa kwa ajili ya kumaliza tatizo la uwanja kwa Yanga.

Ingawa haijafahamika ujenzi huo ungeanza lini, lakini ni kwamba Yanga tayari ilikuwa na uhakika wa kumiliki uwanja baada ya miaka mingi ya kutangatanga kutokana na Uwanja wa Kaunda kutoweza kutumika. Wanayanga na hata mashabiki wa soka walipokea taarifa hiyo kwa furaha kubwa kwa sababu ni aibu kubwa kwa klabu kubwa kama Yanga kukosa hata uwanja wa kufanyia mazoezi na kuishia kuhama hama kwenye viwanja vya kukodi.

Hata hivyo wakati mashabiki wakisubiri ujenzi huo, uongozi wa Yanga ulitoa kauli nyingine ambayo inastaajabisha kidogo. Mwenyekiti wao, Yusuf Manji alinukuliwa kwenye mkutano na wanahabari akisema kuwa, Kigamboni kutajengwa Uwanja wa mazoezi tu, lakini uwanja kwa ajili ya mechi utakuwa Kaunda, yaani pale Jangwani.

Manji amesema kwamba eneo la Gezaulole, Kigamboni anataka kuijengea Yanga Uwanja wa mazoezi tu mdogo utakaokuwa pia na gym ya mazoezi na kwamba Uwanja mkubwa na wa kisasa utakuwa Jangwani. Hata hivyo kauli hiyo ni kama inakinzana na taarifa ya awali kwamba kutokana na Yanga kugomewa kuendeleza eneo la makao yao makuu mitaa ya Twiga na Jangwani na hasa kujenga Uwanja wa Kisasa pale Kaunda, ilikuwa lazima ipate eneo nje ya jiji kama ambavyo watani zao Simba na Azam walivyofanya.

Simba inaendelea na michakato yake ya ujenzi wa Uwanja wao wa Bunju, huku Azam ikiwa tayari ina Uwanja wa kisasa kule Chamazi, ambao unatambulika mpaka na Shirikisho la Soka Afrika (Caf). Hata wakati wa uzinduzi wa jiwe la msingi, Waziri Nchemba alinukuliwa akisema anafurahi kuona uongozi wa Yanga umesikiliza ushauri wake wa kusaka eneo la kujenga Uwanja mpya badala ya kung’ang’ania Kaunda ambako ni ngumu kuruhusiwa na serikali kwani eneo lenyewe ni hatarishi. Lakini sasa Manji anauambia umma uwanja wa kisasa utakuwa Kaunda na sio Kigamboni, jambo linalozua maswali yasiyo na majibu. Mwanaspoti haina nia ya kuingilia mambo ya Yanga, lakini linashauri Manji na wenzake kufuta wazo la kujenga Uwanja wa Kisasa eneo la Jangwani. Serikali ilishaigomea na wataalamu wameshawaeleza kwa sababu gani uwanja huo hauwezekani kuwa hapo. Kuendelea kung’ang’ania kutaka kujenga Uwanja pale Kaunda ni kutoa picha kwamba hata eneo lililodaiwa kutolewa huko Gezaulole labda ni kiini macho tu? Kwanini ujengwe uwanja mdogo wa mazoezi na gym kwa ekari 712? Ndio maana tunausihi uongozi wa Yanga kufikiria upya kuweka nguvu kule Kigamboni na si Jangwani.