Ukimuelewa vizuri Chanongo hakupi shida

Muktasari:

Na inawezekana klabu zetu mbili, Simba na Yanga zina watu wa intelijensia. Inawezekana kabisa. Ndio maana kila wakati wachezaji wetu wanafukuzwa au kusimamishwa kwa kosa la kuhujumu timu.

MIAKA ya karibu lilizuka neno intelijensia. Watu wanaochunguza mambo kwa undani zaidi na kuyafuatilia kwa umakini zaidi kabla ya kutoa taarifa kwa watu wa ngazi za juu.

Na inawezekana klabu zetu mbili, Simba na Yanga zina watu wa intelijensia. Inawezekana kabisa. Ndio maana kila wakati wachezaji wetu wanafukuzwa au kusimamishwa kwa kosa la kuhujumu timu.

Ndio maana hata winga mdogo anayejaribu kuja juu, Haruna Chanongo amesimamishwa. Inasemekana taarifa za kiitelijensia zimewaambia viongozi wa Simba kuwa Chanongo ni Yanga. Inasikika kuwa anaihujumu timu yao hasa inapocheza na Yanga.

Aliwahi kukosa bao la wazi katika pambano la marudiano kati ya Simba na Yanga msimu uliopita. Lakini pia anaambiwa kuwa mienendo yake ndani na nje ya uwanja imekaa Kiyanga zaidi. Unawezaje kuwabishia wazee wa intelijensia?

Lakini ndani ya uwanja Chanongo hakupi sana shida kama ukimchunguza kwa sababu za kisoka. Kama ukiamua kuyachukua mapungufu yake na kuyaita hujuma, basi hata akienda Yanga ataambiwa anaihujumu timu.

Chanongo ni mchezaji mzuri. Anajua sana kukokota mpira. Hata hivyo, anapoteza ufahamu wake wakati anapokaribia eneo la hatari la lango. Hapo ndipo akili yake inapoondoka na anakosa uamuzi wa busara.

Anakosa uamuzi wa aina tatu. Kwanza kabisa hana ushujaa wa kuingia ndani ya boksi kwa kasi ileile na kujiamini kulekule ambako alitoka nako katikati ya uwanja au katika eneo fulani la uwanjani.

Akifika hapo anaweza kugeuka haraka na kumtazama beki wake wa kushoto alipo ili atoe pasi. Bahati nzuri nilisafari kwenda naye Angola Februari mwaka jana nikamwambia kuhusu tatizo hilo.

Ulikuwa wakati mzuri kwake kutangaza jina lake na ufalme wake ndani ya Simba kwa sababu ndio kwanza Emmanuel Okwi alikuwa amepata mkataba wa kuichezea Etoile du Sahel ya Tunisia na Simba walikuwa na matumaini kuwa ataziba pengo la Okwi.

Kama alikuwa mchezaji mwenye kichwa chepesi, Okwi alikuwa somo kubwa kwake. Tabia ya Okwi ni kuwafuata mabeki walipo huku akikokota mpira kwa ufasaha.

Anapokaribia katika eneo la hatari anazidi kujilegeza lakini hana muda wa kugeuka nyuma kumtafuta beki wake wa kushoto. Ni ama atafanya atakalo au atachezewa faulo.

Chanongo hayuko hivyo. Uwezo wake wa kujiamini katika kuingia katika eneo la hatari upo chini. Lakini hapo hapo Chanongo ana tatizo jingine. Hajui ni wakati gani wa kumpasia mchezaji mwenzake anayesubiri mpira au aliye katika eneo zuri.

Tatizo lake la tatu ambalo ni kubwa pia ni lile la kuwa na papara pindi anapoamua kuchukua uamuzi wa kufunga mwenyewe. Inakuwa kama vile nyasi zina moto.

Ukichunguza uhodari wa kina Mbwana Samatta, Kipre Tchetche na Okwi mwenyewe, basi ni jinsi wanavyoweza kutulia katika eneo hilo huku mabeki wakiwa karibu yao.

Kimpira, Ramadhani Singano ‘Messi’ aliwahi kupevuka zaidi katika maeneo haya matatu kuliko Chanongo. Messi alikuwa anajiamini zaidi na ndio maana msimu uliopita ghafla aliibuka kuwa tegemeo la timu.

Baada ya kuibuka kuwa tishio, kutokana na utoto wake, Messi sasa amezidisha chumvi katika vitu anavyovifanya uwanjani na anaonekana kama vile anacheza na jukwaa. Kuna mashabiki wa Simba wameanza kumchukia wanamuona anacheza mpira kama yuko kwenye michezo ya shule za sekondari nchini (Umisseta).

Tukirudi kwa Chanongo hayo ndio matatizo yake makubwa. Sijui makocha wake wanamsaidia vipi. Lakini kipindi hiki kilikuwa kizuri kwake kupata mwendelezo pengine kuliko kutupiwa shutuma za mara kwa mara kwamba anahujumu timu.

Kwa ninavyomuona, hata hao Yanga wakimsajili (nasikia wanahusishwa kumchukua), nadhani haitapita kipindi kirefu kabla nao hawajaanza kumshutumu kuwa anahujumu timu kwa sababu kwa mtazamo wangu matatizo aliyonayo ni ya ufundi zaidi na yanahusu saikolojia katika soka.

Lakini hata Simon Msuva alikuwa na matatizo hayo hayo wakati akiendelea kukua. Yanga walikuwa wanamtukana na kumzomea.

Alipoambiwa ajirekebishe katika kufanya uamuzi wa mwisho ameibuka kuwa mchezaji muhimu zaidi pale Jangwani. Na umuhimu wake unazidi ule wa Mrisho Ngassa kwa sasa.

Katika soka la Tanzania kuna sayansi ya mpira na kuna sayansi ya siasa ndani ya mpira. Nimejaribu kutumia sayansi ya kwanza, lakini nadhani viongozi wa Simba wataamini zaidi katika sayansi ya pili.