Uhuni huu wa mashabiki wa soka usinyamaziwe

Muktasari:

  • Licha ya kelele na majigambo, kilichoonekana kwenye mchezo huo wa juzi Jumamosi haukuwa na ufundi kama kawaida ya mapambano mengi ya timu hizo pinzani kutokana na wachezaji wengi mara nyingi kukamiana uwanjani.

HATIMAYE pambano la Watani wa Jadi wa Soka nchini, Simba na Yanga limechezwa na kumalizika kwa timu hizo kushindwa kutambiana kwa kufungana bao 1-1.

Kabla ya mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam kulikuwa na kelele na tambo nyingi toka kwa wadau wa klabu hizo wakiwamo viongozi, makocha, wachezaji na hata wanachama na mashabiki.

Licha ya kelele na majigambo, kilichoonekana kwenye mchezo huo wa juzi Jumamosi haukuwa na ufundi kama kawaida ya mapambano mengi ya timu hizo pinzani kutokana na wachezaji wengi mara nyingi kukamiana uwanjani.

Ukiachana na matokeo ya mchezo huo ambao yanaendelewa kujadiliwa mitaani na hasa matukio ya mwamuzi Martin Saanya kuonekana kushindwa kuumudu mchezo huo, Mwanaspoti linasikitishwa na uhuni uliofanywa na baadhi ya mashabiki.

Mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Simba, walifanya uhuni wa kung’oa viti, matukio ambayo yalishaanza kusahaulika baada ya kukemewa na kulaaniwa na kila mtu mara yalipoanza kujitokeza kwenye Uwanja wa Taifa.

Tukio hilo lilitokea baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na Amissi Tambwe ambalo lilidaiwa mfungaji kabla ya kutupia nyavuni aliugusa kwa mkono na kuhisi kama timu yao inaonewa na kuchukua maamuzi hayo yasiyokubalika.

Kwa hakika hatupaswi kushabikia vitendo hivi vya kihuni kufanywa kwenye viwanja vya soka na hasa Uwanja wa Taifa.

Hakuna asiyejua uwanja huo umeigharimu serikali fedha nyingi mpaka kukamilika kwake na ni moja ya kivutio cha wageni kwani Uwanja wa Taifa ni miongoni mwa viwanja vichache vya kisasa na vikubwa vilivyojengwa barani Afrika.

Jambo hilo halikubaliki kwani hakuna uhusiano wowote kati ya maamuzi ya waamuzi na vitendo hivyo.

Hata kama waamuzi walikuwa wakitoa maamuzi yenye utata, imekuwaje viadhibiwe viti kwa kuvunjwa na kung’olewa na mashabiki hao kama sio watu kukosa ustaarabu na kuendelea kukumbatia vitendo visivyo vya kistaarabu viwanjani.

Mwanaspoti linaungana na wote wanaokemea na kulaani vitendo hivyo vya kihuni vilivyoanza kurejeshwa tena kwenye uwanja huo wa Taifa na kuleta uharibifu usio wa lazima kwani zipo taratibu za kuwasilisha malalamiko ya klabu inayoona imeonewa. Ni lazima viongozi wa klabu za soka zinazoutumia uwanja huo kuwaelimisha mashabiki na wanachama hao kuepukana vitendo kama hivyo kwani licha ya kuharibu uwanja, lakini pia ni mzigo kwao wanapotozwa faini kufidia uharibifu huo.