Uamuzi wa serikali ni sahihi, ila adhabu iangaliwe upya

HAKUNA anayefurahia vitendo vya kihuni vya kuvunja viti kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam. Kwa muda mrefu sasa mashabiki wa soka hasa wa Simba na Yanga wamekuwa wakituhumiwa kufanya vitendo visivyo vya kiungwana kwa kuvunja na kung’oa viti kisha kuvitupa uwanjani kila wanapopandwa na hasira.

Kwa Simba imekuwa ni kama ada kwao, wamekemewa, klabu yao imeadhibiwa, lakini ni kama watu hawajali. Hatuwezi kuliunga mkono jambo hilo.

Yanga kadhalika kuna wakati walitaka kuingia kwenye mkumbo huo wa kung’oa viti, lakini baada ya kekemewa walitulia na kuishia kujikita kwenye kuvunja mageti kila wanapopatwa na jazba kwenye uwanja huo.

Hata hili nalo halikubaliki wala kuungwa mkono, kwa sababu vitendo hivyo vinaharibu miundo mbinu na mandhari ya uwanja huo uliojengwa kwa gharama kubwa na serikali kwa kutumia fedha za umma na msaada kutoka kwa nchi wahisani ya China.

Juzi Jumamosi uhuni huo wa kung’oa viti na kuvunja mageti uwanjani hapo ulijiri tena na serikali juzi Jumapili imetoa tamko la kuzizuia Simba na Yanga kuutumi uwanja huo kwa sasa mpaka itakapotoa taarifa nyingine.

Pia, imetangaza kuzuia mgao wa mapato ambao timu hizo zilistahili kuupata kupitia pambano hilo mpaka kwanza tathimini ya uharibifu ifanyike na klabu kulipishwa fidia kadiri ya uharibifu huo.

Ni jambo zuri kweli na la kupongezwa. Hii inaweza kuwaamsha viongozi wa klabu hizo kuweka mkazo katika kuwakemea na kuchukua hatua kali kwa mashabiki wao wasio wa kistaarabu. Hata kama ni kweli ni vigumu kuwadhibiti wasifanye ujinga uwanjani hapo.

Hata hivyo, Mwanaspoti linadhani adhabu za kuzihamisha Simba na Yanga ghafla kuutumia uwanja huo sio sahihi, ila klabu hizo zingeweza kupewa adhabu mbadala ikiwamo kucheza bila mashabiki katika mechi zao kwenye uwanja huo.

Ndivyo ambavyo tumekuwa tukishuhudia klabu mbalimbali duniani zikipewa adhabu kama hizo pale mashabiki wao wanaposhindwa kuonyesha ustaarabu. Tunaamini kama Simba na Yanga zitacheza mechi zao bila mashabiki na kupoteza mapato walioyatarajia kuyavuna katika mechi hizo, itawaumiza viongozi wa klabu hizo na kuchukua hatua kali.

Hawatakubali tena kuwalea mashabiki na wanachama wao ambao huacha ustaarabu majumbani mwao kila wanapoenda Uwanja wa Taifa kuzishangilia timu hizo. Inawezekana wengi wanafanya upuuzi huo kwa vile tu, wanajua hawawajibiki kwa adhabu zozote zinatolewa na mamlaka ya soka ama serikali kama ilivyotokea sasa, siku zote wao hawaguswi na badala yake klabu zao ndizo zinazobebeshwa mzigo wote.

Lakini kwa kuwazuia kuingia uwanjani iwe kwa mechi hata tatu ama tano kama adhabu ya uhuni uliofanyika Jumamosi ni wazi, itawafanya wale wanaowalea wanapofanya uhuni huo wasiwanyamazie tena, watadhibitiwa na kuwachukulia adhabu.

Picha mbalimbali zimepigwa juzi zikiwaonyesha mashabiki wa Simba wakivunja viti. Wale hawatoki sayari nyingine ni watu wanaofahamika mbele ya wenzao, lakini hakuna hata mmoja atakayenaswa kwa sababu watu wanawachukulia poa na kuwalinda, ilihali klabu zinazobebeshwa mzigo, hazikuwatuma kufanya upuuzi huo, ila ni ulimbukeni wao tu.

Ndio maana tunaamini kuwa, Simba na Yanga zinastahili adhabu kwa uhuni uliofanywa na mashabiki wao, lakini bado hili la kuwaondoa ghafla Uwanja wa Taifa liangaliwe upya kwani haliwezi kuwatia adabu wafanya uhuni huo ila kuzibebesha mzigo klabu hizo.

Badala yake hata mashabiki nao kwa namna moja wapewe adhabu ikiwamo hiyo ya kuwazuia kuingia uwanjani, kwani itawafanya wajione wajinga na kuacha upuuzi wao hata pale watakaporuhusiwa tena kuhudhuria mechi uwanjani hapo.

Kwa sababu kuendelea kuwaacha watambe mitaani ni kuruhusu vitendo hivyo kuendelea kuota mizizi miongoni mwa mashabiki hao.

Lakini kwa kuadhibiwa kwao, sio tu itatoa fundisho kwa wengine, lakini pia itasaidia kuzinusuru klabu kuondokana na mzigo usio wa lazima ambao wakati mwingine wala huwa hawana  habari kama kuna watu wataenda kufanya upuuzi wao viwanjani.

Hivyo, kwa kuzuiwa Simba na Yanga Uwanja Taifa haitakuwa imesaidia kuondoa tatizo kwa sababu wahusika wa vitendo hivyo wataendelea tu kufanya upuuzi wao hata huko ambako klabu hizo zitaenda kucheza baada ya kutimuliwa uwanjani hapo.

Tunaamini jambo hili la kuwashughulikia watenda maovu hayo, ni njia nzuri zaidi kuliko hii ya kuzitimua klabu hizo Uwanja wa Taifa huku ikizingatiwa kuwa, serikali imetumia fedha kutengeneza mfumo wa  tiketi za elektroniki uwanjani hapo.