USWAHILINI: Klabu ziache ulimbukeni kwa wageni, wazawa wanatosha

Muktasari:

Sifa ni jambo la kawaida kwa binadamu yeyote na ndiyo maana utamsikia mtu yeyote mkubwa kwa mdogo, akiambiwa kuwa amependeza, mara hiyo itamtoka asante kubwa, lakini akiambiwa maneno au kauli za kukosolewa, basi ataukunja uso na mdomo kwa hasira.

WASWAHILI husema, akili ni nywele kila mtu ana zake. Nikiwa naangalia kituo kimoja cha runinga hapa nchini majuzi nilicheka, nikabaki midomo wazi.

Ni pale niliposoma ujumbe uliotoka kwa msikilizaji wa kipindi kimoja, akisema kuwa, kama akili ni nywele, basi weave ni memory card. Nikaguna, weave, ana maana gani, amekosea, alitaka kusema wivu au la?

Nikajiuliza, alikuwa na maana gani mwandishi wa ujumbe ule, lakini baada ya kufanya tafakuri ya kina, ndipo nikabaini kuwa kumbe ni mambo ya mtandao wa mawasiliano, siku hizi kinadada wanabadili nywele zao, wanaishi kwa kuwaza nywele zao, wanaishi, kula na kuishi wakiwaza habari za kwenda saluni kujiremba na kushonea nywele za bandia.

Nikabaini kwamba weave, alimaanisha mtindo wa nywele na kwamba bila kwenda saluni, mwanadada wa kisasa haoni kama amefika safari yake ya kupendeza na hata kuvutia, kiasi cha kuhitaji kusifiwa.

Sifa ni jambo la kawaida kwa binadamu yeyote na ndiyo maana utamsikia mtu yeyote mkubwa kwa mdogo, akiambiwa kuwa amependeza, mara hiyo itamtoka asante kubwa, lakini akiambiwa maneno au kauli za kukosolewa, basi ataukunja uso na mdomo kwa hasira.

Nimebaini, kumbe hata katika soka letu, huku Uswahilini soka linachezwa kwa kusaka sifa kutoka kwa mashabiki, jambo ambalo linaua ushindani.

Tangu nilipoandika kwenye safu hii nikieleza kwa kirefu kuwa nilikuwa nasubiri kuona mazingaombwe si soka ya uhakika kutoka kwa majirani wale wa Kariakoo, Simba na Yanga, ambao walikutana siku ile ya Septemba 25 kwenye Uwanja wa Taifa na Simba kuumia kwa mabao 2-0, kila aliye shabiki wa damu wa Simba, akiguswa na mtani wake basi anakasirika.

Hasira zile za mabao ya Amissi Tambwe na Malimi Busungu kila kipindi cha mchezo huo zimewafanya majirani wale wa Kariakoo waishi hivi leo kwa kuviziana. Wamenuniana, wanasubiri raundi ya pili waone ni nani jogoo, yupi mtetea?

Ingawa kwa siku 14, Simba na Yanga hazipo uwanjani, zimeachia wachezaji wao kujiunga na kikosi cha Taifa Stars kilichoikabili Malawi, Jumatano jioni na Stars kubuka kidedea kwa mabao 2-0, nimeambiwa kuwa makocha wao, Dylan Kerr na Hans Pluijm hawalali usingizi, wameamua kuwaandaa vijana wao kwa mechi za Ligi Kuu ambazo zitarejea Oktoba 17.

Oktoba 17, nimeambiwa kuwa itakuwa zamu ya Stewart Hall  dhidi ya Pluijm, Mdachi wa Yanga, huku  akiwa na kumbukumbu ya mikwaju ya penalti 8-7 katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Agosti mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa.

Mchezo huo wa Yanga na Azam, timu mbili kubwa n maarufu nchiini ambazo kwa sasa zinaelekea kuwa ndizo zimekuwa zenye ushindani mkubwa zaidi kuliko pengne ilivyokuwa kwa Simba na Yanga, siku hizi ushindani huo wa Yanga na Azam unaashiria nini zaidi katika soka letu huku Uswahilini?

Hakuna shaka, ushabiki na upinzani unafanyika ndani na nje ya soka kwa mashabiki kiasi kwamba safari ya kwenda Uwanja wa Taifa, na kurudi kwa wengine inaonekana ndefu na ngumu kwa mashabiki.

Ninajiuliza, timu zetu zinajiandaa kucheza baina yao, zinakuwa na ushindani mkubwa, zinacheza soka ya kueleweka, ambako siku hizi unaweza kuona pasi kadhaa zikipigwa na wachezaji wetu, mbinu hizi huenda wapi timu zetu zinapocheza na wapinzani wao kutoka nje ya nchi?

Swali hili linanijia ninapoziangalia Yanga na Azam ambazo zina jukumu la kuiwakilisha nchi kwenye mashindano ya Afrika mwakani, ambako hakuna shaka Tanzania imekuwa ikifanya vibaya.

Ninajisemea kimoyomoyo, kama zinaweza kujiandaa kwa mchezo wao wa  Oktoba 17, Yanga na Azam zinasubiri nini kuanza maandalizi ya kina ya mechi za kimataifa mwakani dhidi ya wapinzani wao, ambao zitapangiwa baadaye na Shirikisho la Soka Afrika (CAF)?

Ni maandalizi pekee na mipango ya muda mfupi, muda wa kati na mrefu ndiyo yameziwezesha timu za mbili za Sudan kucheza hadi nusu fainali ya Mabingwa Afrika msimu huu, ambako klabu hizo, El- Merreikh na Al- Hilal zimetolewa kwa idadi au tofauti ya mabao 4-2 na 2-1 na wapinzani wao, TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na USM Alger ya Algeria, ambazo zitacheza fainali.

El- Merreikh na Al- Hilal, ambazo hazikushiriki Kombe la Kagame ambalo Azam ilishinda dhidi ya Gor Mahia ya Kenya kwa mabao, ni timu ambazo zinatoka ukanda mmoja nasi, zimetuonyesha njia kwamba hata Yanga na Azam zikiwa na mipango zinaweza kucheza na kufanikiwa Afrika, lakini zinahitaji maandalizi makubwa.

Kitu kinachoniumiza ni timu zetu kuwasajili wachezaji wa kigeni, ambao baadhi yao hawatumiki. Hiki ni kitendawili kinaniumiza, ninapoziona klabu zetu zikihangaika kutaka kuwa na wachezaji saba wa kigeni, ambao kwa bahati mbaya hawatumiki wote katika mechi, ni kwa ajili ya nini, ufahari?

Ufahari gani huu wa kijinga wa timu zetu kuwasajili wachezaji wa kigeni kwa gharama kubwa ambao wanawekwa benchi hata na vijana wa huku Uswahilini?

Niwapongeze kina Hamis Kiiza, Juuko Murshid na Justice Majabvi ambao wamekuwa wakiichezea Simba kwa mafanikio msimu huu, sawa na kina Tambwe, Donaldo Ngoma, Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima wa Yanga.

Kwa Azam wapo Kipre Tchetche, Allan Wanga, Jean Baptiste Mugiraneza, Pascal Wawa, ambao walau wanacheza mara nyingi kikosi cha kwanza, kiasi cha kuhalalisha usajili wao, lakini wako wapi wengine , wamesajiliwa kwa kazi ipi, hata kama kikosi cha kwanza hawana namba, si bora waachwe tu?

*Ndyesumbilai Florian ni Msanifu Mwandamizi wa Michezo, Mwananchi