UCHAMBUZI: Elimu ya maadili na nidhamu ni muhimu sasa

Muktasari:

Kwa kauli ile waziri mkuu yule wa zamani aliona kuwa Beckham ataendelea kuishi na heshima ileile hata baada ya kumaliza mpira wakati heshima aliyonayo kama waziri mkuu ingepungua kama si kutoweka baada ya kumaliza kazi hiyo

ASSALAAM aleiykhum wasomaji wa makala zetu na wanamichezo wenzangu kwa jumla. Soka ni mchezo maarufu na wenye mashabiki na wafuasi  katika kila kona ya dunia na una historia ya kipekee kabisa ukilinganisha na  michezo mingine duniani.

Vitabu mbalimbali vya historia na baadhi ya machapisho yanaelezea historia ya soka   kuwa ulikuwa ukichezwa enzi za utumwa ambapo watwana walicheza mpira usiokuwa na sheria, wakitumia, miguu na mikono ili kuwafurahisha mabwana zao.

Yote kwa yote lakini bado mchezo huu umeendelea kuwa mchezo unaochezwa na watu wanaotoka katika famila za kimasikini au zile zenye uwezo wa kati ingawa  wamewahi kutokea wachezaji mahiri wachache waliotoka katika familia za kitajiri.

Kadiri miaka inavyozidi kwenda mbele  mchezo huu umeendelea kutoa ajira kwa wachezaji wengi waliotoka kwenye familia masikini na kuwapatia utajiri mkubwa, hivyo kuwa  kivutio kwa vijana wengi  wa Kiafrika, Amerika ya Kusini, Ulaya na hata Bara la Asia.

Kuna wakati aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tonny Blair alisema,  pamoja na kuwa yeye  waziri mkuu wa Uingereza  lakini anatamani angekuwa David Beckham,kipindi  hicho Beckham alikuwa akiichezea Manchester united mwishoni mwa miaka ya 2000. Aliitoa kauli hiyo huku akihusisha umaarufu wake kama waziri mkuu na utajiri na heshima aliyonayo Beckham sio tu kwa Waingereza, bali kwa wapenzi wa soka duniani kote  ambayo ameipata kupitia mchezo wa soka.

Kwa kauli ile waziri mkuu yule wa zamani aliona kuwa Beckham ataendelea kuishi na heshima ileile hata baada ya kumaliza mpira wakati heshima aliyonayo kama waziri mkuu ingepungua kama si kutoweka baada ya kumaliza kazi hiyo .

Hapa Bongo pia tumeshuhudia thamani ya mchezo wa soka jinsi inavyoendelea kupanda kila kukicha kiasi cha kusababisha makampuni mbalimbali ya biashara kuingiza fedha nyingi katika mchezo huu kupitia udhamini kwa klabu pamoja na ligi mbalimbali. Ndio maana leo hii tunaona  thamani ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiongezeka kutoka  Sh 3.5 bilioni  mwaka 2013  hadi kufikia zaidi ya Sh 6  bilioni mwaka  2015 huku thamani ikitarajiwa kuongezeka maradufu  kwa miaka michache ijayo.

Yote haya hayajatokea kwa bahati mbaya kwani  kuna watu waliokaa chini na kuuumiza vichwa vyao kwa  kuchanganua na kuweka mipango inayopangika. Ndio maana leo hii mchezo wa soka unatukuzwa na kuitwa mchezo wa kiungwana na wa kistaarabu.  hivyo kuvutia watu wa aina zote na makampuni makubwa ya biashara kama tunavyoona.

Nimezungumzia thamani ya soka kwa kuwa kuna kazi kubwa ya kuusafisha mchezo  huu imefanyika hadi leo tumefikia hapa. Hivyo tukio lolote la ndani ya uwanja au la nje ya uwanja linaloashiria kuurudisha mchezo wa soka nyuma linatakiwa kupingwa kwa nguvu zote kwani tulikotoka ni mbali na pachungu zaidi kuliko kule tunakoelekea.

Wiki yote hii imekuwa na mijadala juu ya kile kilichotokea kwenye mechi kati ya  Azam na Mbeya City ambapo kwa hakika Watanzania na wapenzi wa soka  wameungana na kuonesha hasira zao juu kitendo  kile cha udhalilishaji. 

Nami pia siwezi kuwa mbali na maoni ya wengi juu ya suala hilo la ukosefu  wa nidhamu  na upungufu wa maadili wa kiwango hicho kwani ni kinyume na maadili yetu na mfanyaji wa kitendo kile inaonekana hakujifunza pale alipopewa adhabu ya kupumzika mechi nane msimu uliopita kwa kufanya kosa kama hilo.

Sio nia yangu leo hii kuizungumzia adhabu ya miaka miwili iliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi ya kumfungia  mchezaji huyo miaka miwili na faini ya Sh 2 milioni ambazo pia sitaki kujua kama kuna kiasi pengine kitaenda kwa mwathirika wa tukio hilo au la!  Bali  nia yangu ni kwenda mbele zaidi adhabu tu katika kutibu matatizo ya wachezaji yanaoambatana na tabia.

Mwalimu wangu aliwahi kunifundisha kuwa, utaratibu wa kuweka sheria huanza  kwa kutolewa elimu  juu ya faida na madhara ya kitu kinachotarajiwa kuwekewa sheria, ili  mhusika ajue madhara yake ma faida zake  kisha ndipo sheria ianze kufanya kazi. Ingawa  dhana hii inakinzana na msimamo wa kisheria za kibinaadamu kama wanavyosema kuwa  ‘ignorance is not an excuse’ yaani ujinga sio sababu ya mtu kufanya kosa.

Ni ukweli usipingika kuna haja sasa ya kutolewa elimu ya nidhamu na maadili  kwa wachezaji kwani wengi   hawajapata mafunzo ya maadili na nidhamu ambayo kwa vijana wanapokuwa  mashuleni.