MTU WA PWANI : Tuungane kumpiga tafu na kumuombea Manara

Muktasari:

  • Ni mchezo muhimu kwa Yanga ambayo kwa namna yoyote ile inatakiwa kuibuka na ushindi, ili iweze kufufua matumaini ya kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ikitokea Kundi A.
  • Baada ya kupoteza mechi mbili zilizotangulia dhidi ya MO Bejaia ya Algeria na TP Mazembe ya DR Congo, kwa bao 1-0 kila mechi, Yanga ilijikuta ikishika nafasi ya mwisho kwenye kundi hilo ikiwa haina pointi.

KESHO Jumamosi, Yanga itashuka dimbani kuumana na Medeama ya Ghana katika mchezo wa tatu wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Ni mchezo muhimu kwa Yanga ambayo kwa namna yoyote ile inatakiwa kuibuka na ushindi, ili iweze kufufua matumaini ya kufuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo ikitokea Kundi A.

Baada ya kupoteza mechi mbili zilizotangulia dhidi ya MO Bejaia ya Algeria na TP Mazembe ya DR Congo, kwa bao 1-0 kila mechi, Yanga ilijikuta ikishika nafasi ya mwisho kwenye kundi hilo ikiwa haina pointi.

Hivyo, bila shaka yoyote, naamini mpaka sasa uongozi wa Yanga na benchi la ufundi wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo huo wa kesho ambao umeshikilia hatma ya wawakilishi wetu hao.

Ni imani yangu kuwa dua na sala za Watanzania wote, hususan wapenzi wa soka zitaelekezwa kwa Yanga, ili iweze kupata matokeo mazuri yatakayoirudisha kwenye mstari katika mashindano hayo.

Wakati tukiiombea Yanga ifanye vizuri dhidi ya Medeama, ningependa pia kuwakumbusha wadau wa soka nchini kumuweka katika maombi na kumsaidia, Mkuu wa Idara ya Habari wa Klabu ya Simba, Haji Manara ambaye kwa sasa afya yake haijatengamaa.

Kwa takriban wiki mbili sasa, Manara amekuwa akiuguza jicho lake la kushoto ambalo limepoteza uwezo wa kuona, hivyo kumfanya atumie jicho moja la tu ambalo pia nalo halina uwezo wa kuona vizuri.

Kutokana na tatizo hilo, kati ya kesho au keshokutwa, Manara anatarajia kusafiri kuelekea India kwa ajili ya matibabu zaidi.

Ni ukweli usiopingika kuwa Manara ambaye amejizolea umaarufu mkubwa katika miaka ya hivi karibuni, yupo kwenye wakati mgumu katika maisha yake kutokana na tatizo linalomkabili. Ikielezwa kuwa limemtokea ghafla, ikiwa hajawahi kukumbwa na tatizo kama hilo kabla. Hii inaumiza asikwambie mtu.

Manara ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika medani ya soka nchini kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuhamasisha wapenzi na mashabiki wa soka, kujitokeza viwanjani katika mechi mbalimbali za Simba na hata zile ambazo haziihusu timu hiyo.

Katika nyakati hizi ambazo kundi kubwa la mashabiki wa soka Tanzania limeonesha kutekwa na soka la nchi mbalimbali za Ulaya na Amerika Kusini, uwepo wa watu kama Manara una umuhimu mkubwa kwani unasaidia kurudisha hamu ya wapenzi na mashabiki wa soka nchini.

Pamoja na kuhamasisha, Manara sambamba na msemaji wa Yanga, Jerry Muro wamekuwa wakionyesha kwa vitendo dhana ya utani wa jadi ambao Klabu za Simba na Yanga zimekuwa nayo tangu zilipoanzishwa miaka zaidi ya 50 iliyopita.

Ni wazi kuwa kama Manara atashindwa kupata uponyaji wa tatizo linalomkabili, ufanisi wake katika nafasi aliyonayo sasa utapungua na pengine anaweza asiendelee kulitumikia soka letu.

Huu ni wakati wa kuweka kando itikadi za Usimba na Uyanga na kuungana pamoja katika kumsaidia Manara iwe kwa maombi au kumchangia fedha ili afanikiwe kupata tiba sahihi ya tatizo linalomkabili.

Miongoni mwa matukio yaliyonisisimua juzi ni kitendo cha wanachama wa Yanga, kumtembelea Manara nyumbani kwake na kumkabidhi kiasi cha fedha zaidi ya Sh. 1 milioni kwa ajili ya kumsaidia kwenye matibabu yake.

Moyo huo wa kiungwana ulioonyeshwa na Wanayanga, unapaswa kuonyeshwa pia na watu wa klabu nyingine zikiwamo Simba, Azam, Mtibwa, Mwadui na wapenda soka wote nchini kuthibitisha ule usemi kuwa soka ni mchezo wa uungwana.

Litakuwa ni jambo la kushangaza kumtelekeza Manara katika kipindi hiki kigumu kwake wakati tulikuwa tunafurahi naye pamoja katika nyakati tamu za soka.

Kuna dhana mbaya imejengeka kwa muda mrefu nchini kuwa wanamichezo wamekuwa hawatoi msaada pindi wenzao wanapopatwa na matatizo iwe ugonjwa, ajali au misiba na badala yake wamekuwa wakishirikiana katika sherehe na matukio ya furaha tu.

Wakati umefika sasa kwa wanamichezo kuiondoa dhana hiyo potofu vichwani mwa Watanzania kwa kujitokeza kumsaidia Manara jambo ambalo naamini litakuwa chachu ya kuwapa molali wanamichezo ya kusaidiana pale ambapo wanapatwa na matatizo.

Tayari wapenzi na wanachama wa Yanga wameshaonyesha njia kwa kuchangia Manara, nadhani kinachotakiwa kufuata hivi sasa ni sisi wengine tuliobaki kuwaunga mkono kwa kumsaidia mwanamichezo wenzetu.

Na mwisho wa siku utaratibu huu wa kusaidiana haupaswi kuishia kwa Manara tu bali uendelee kwa wanamichezo wengine pindi wanapokumbana na matatizo kama hili lililomsibu msemaji wa Simba.

Wanamichezo tunatakiwa kuguswa na matatizo yanayowapata wenzetu na kuwapa sapoti yetu badala ya kujiweka pembeni na kuwaacha wayatatue wenyewe matatizo yao.

Ni aibu kwetu kumuacha Manara peke yake wakati tunaweza kufanya kitu ambacho kinaweza kumsaidia aweze kupata matibabu stahiki ya tatizo lake la macho.

Manara ni mwenzetu na tumekuwa tukishirikiana naye kila wakati kwenye masuala mbalimbali ya kimichezo. Basi tufanye juu chini kumsaidia ili arudi katika hali yake ya kawaida.

Huu ni wakati wa kumpa sapoti yetu badala ya kumtelekeza.