Tunachojidanganya Wabongo kuhusu kwenda kucheza Ulaya

Muktasari:

Ukimaliza kusikiliza habari hiyo unacheka na kutafakari jinsi tunavyojidanganya kuhusu Ulaya. Tunaona kama ni sehemu ambayo mchezaji anaweza kwenda tu kwa kuwa ametaka kwenda. Hatutaki kuzungumza ukweli.

WABONGO tunapenda uongo na ndio sababu tunatumia muda mwingi kudanganyana. Hii ndio sababu inayonifanya kutoshangazwa na taarifa kuwa kiungo wa Simba, Said Ndemla ataachana na timu hiyo hivi karibuni kwani anajiandaa kwenda kucheza Ulaya.

Ukimaliza kusikiliza habari hiyo unacheka na kutafakari jinsi tunavyojidanganya kuhusu Ulaya. Tunaona kama ni sehemu ambayo mchezaji anaweza kwenda tu kwa kuwa ametaka kwenda. Hatutaki kuzungumza ukweli.

Katika hali ya kawaida mchezaji ambaye hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Simba anawezaje kwenda kucheza Ulaya? Ama ni Ulaya nyingine tofauti na hii ambayo ninaifahamu mimi.

Kwenda kucheza Ulaya sio kazi rahisi. Siyo sehemu ambayo kila mtu anaweza kwenda kucheza. Hii ndio sababu mpaka sasa Tanzania yenye watu zaidi ya milioni 50 tuna mchezaji mmoja tu anayecheza Ulaya, Mbwana Samatta. Ulaya ni pagumu kwelikweli.

Sehemu pekee ambayo mchezaji anayeweza kuamua kwenda kucheza soka muda wowote ni Uarabuni maana huko kuna michuano hata isiyokuwa na kichwa wala miguu. Waarabu wanapenda soka na kwao kuwalipa wachezaji ili tu wacheze Kombe la Mafuta mtaani kwake sio tabu.

Hii ndio sababu hadi Danny Lyanga aliyekuwa hana nafasi Simba amekwenda Uarabuni na anacheza. Hiyo ndiyo sababu Mrisho Ngassa ameshindwa maisha Sauzi, lakini ameenda Uarabuni na anacheza. Hii ndio sehemu pekee nyepesi kucheza soka.

Hii Ulaya tunayoambiwa anakwenda Ndemla sio mchezo, labda kama anaenda kucheza muziki. Ili mchezaji akacheze Ulaya ni lazima awe amekamilika.

Ni lazima awe na kipaji halisi cha soka na awe anacheza kwa kiwango cha juu kwa uwiano sawa na kwa muda mrefu. Ni lazima awe na nidhamu ya ndani na nje ya uwanja. Ni lazima awe anajitambua kwelikweli.

Ukikosa kitu kimoja kati ya hivyo, ni vigumu kwenda kutamba Ulaya. Haruna Moshi ‘Boban’, alikuwa na uwezo mkubwa uwanjani, lakini maisha ya nje ya uwanja yalimbana na akarudi mapema tu. Emmanuel Okwi pamoja na kipaji chake anasugua benchi pale Denmark. Ulaya sio mchezo mchezo ati.

Thomas Ulimwengu na uwezo wake. Na nguvu zake pamoja na kasi yake yote bado hana uhakika wa kupata timu Ulaya wakati wa dirisha dogo litakalofunguliwa Januari mwakani. Bado Ulimwengu ataenda kufanya majaribio katika klabu kadhaa ili kupata nafasi.

Kumbuka hapa tunamzungumzia Ulimwengu ambaye alikuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza cha TP Mazembe iliyotwaa Kombe la Shirikisho Afrika mapema mwezi huu. Ni Ulimwengu ambaye alikuwa na nafasi katika kikosi cha kwanza cha Mazembe iliyotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana. Ni Ulimwengu mwenye wasifu wa kutisha, lakini kwenda Ulaya ananyata.

Miaka ya nyuma kulikuwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa katika Taifa la Tanzania lakini hawakuweza kwenda kucheza Ulaya.

Labda Ndemla amewasikia kina Edibily Lunyamila, Zamoyoni Mogella Mohammed Salim na hata Augustino Peter ‘Peter Tino ambao walikuwa mahiri kwelikweli lakini walichemsha.

Je, Ndemla ambaye hana hata wasifu unaoeleweka ndio atakwenda huko? Ndemla ambaye anawekwa benchi na Mzamiru Yassin pale Msimbazi. Hata hivyo, huu ndio uongo ambao Watanzania wanaupenda. Tunapenda kujidanganya na mwisho wa siku tunaishi katika uongo.

Wachezaji wetu mahiri bado wanafeli majaribio katika klabu za Afrika Kusini na Congo halafu tunatamani waende kucheza Ulaya. Kama unashindwa kushindana na nyota wa hapa Afrika, utawezaje kwenda kucheza Ulaya.

Saimon Msuva akiwa katika ubora wake alifeli majaribio Bidvest Wits ya Afrika Kusini kama ilivyokuwa pia kwa Jonas Mkude. Kama unafeli kucheza Sauzi utakwenda kucheza Ulaya ipi?

Uongo huu ndio uliowapeleka Abuu Ubwa na Haruna Chanongo katika majaribio pale TP Mazembe mwaka jana. Kwangu ilikuwa ni kama kupoteza muda pamoja na rasilimali tu. Mchezaji anayeshindwa kuivutia Azam FC. Mchezaji ambaye ameachwa na Simba ama Yanga anawezaje kwenda kucheza TP Mazembe? Kwa nini Watanzania hatupendi kuambiana ukweli?

Soka la kulipwa nje ya nchi linahitaji kujitoa na kujituma pia. Je, ni mchezaji gani wa Tanzania ambaye anafanya mazoezi masaa sita ama zaidi kwa siku? Jibu ni jepesi tu, hakuna. Kama hakuna, ni nani ataweza kwenda Ulaya?

Samatta pamoja na kipaji chake na uwezo wake mkubwa wa kufunga bado amekumbana na ugumu pale Ubelgiji. Ushindani ni mkubwa na sasa amecheza kwa miezi miwili bila kufunga bao. Ni sehemu ngumu kwelikweli.

Hapa tunamzungumzia Samatta ambaye amekwenda Ulaya baada ya kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani. Tunamzungumzia Samatta ambaye hana mambo mengi nje ya uwanja na anafanya mazoezi kwa masaa sita ama zaidi kwa siku.

Samatta ambaye ana kipaji, anajielewa na kufuata miiko yote ya soka. Katika hali kama hiyo unawezaje kutuaminisha kuwa Ndemla anataka kwenda Ulaya? Ni kwanini tunapenda kuambiana uongo. Kama ni kweli anakwenda Ulaya pengine ni kwenda tu kufanya utalii ama manunuzi (shopping). Pengine anakwenda kufanya mambo mengine na kuachana na mchezo wa soka.