HISIA ZANGU : Tumemsahau Nyosso, inawezekana amebadilika na tumfikirie

Muktasari:

  • Pamoja na usela wa rafiki yangu, Nyosso bado katika hulka ya mwanadamu hakuna mtu mbabe sana mbele ya njaa. Nyosso naye ana tumbo yule. Anasikia njaa kama wanadamu wengine. Kama ilivyo kwa mimi na wewe.

TUMEMSAHAU Juma Nyosso na maisha yanaendelea. Mchukie au mpende, Nyosso ni mmoja kati ya mabeki imara wa kati nchini. Ukabaji wake ni wa kiwango cha juu. Tatizo lake ni moja tu, wakati mwingine anakuwa msela sana.

Pamoja na usela wa rafiki yangu, Nyosso bado katika hulka ya mwanadamu hakuna mtu mbabe sana mbele ya njaa. Nyosso naye ana tumbo yule. Anasikia njaa kama wanadamu wengine. Kama ilivyo kwa mimi na wewe.

Alifungiwa kwa kosa la kumfanyua kitendo cha udhalilishaji mshambuliaji wa Azam, John Bocco. Halikuwa kosa lake la kwanza kwa sababu alishawahi kufanya hivyo kabla. Hata hivyo, katika kosa lake la kwanza Nyosso hakupata njaa kwa sababu hakufungiwa.

Hata hivyo, kuna umuhimu wa kuipima njaa ya sasa ambayo Nyosso anaipata kwa kufungiwa. Namjua, maisha yake yalikuwa yanategemea soka tu. Nadhani kwa sasa atakuwa anahaha bila ya msaada mkubwa katika maisha yake.

Tujiulize, tumechukua jitihada gani za kuchunguza kama Nyosso amebadilika au bado ni yule yule? Na hasa katika nyakati hizi ambazo anacheza soka la kihuni mitaani.

Katika soka hakuna msamaha unaotokana na tabia nzuri za mchezo baada ya makosa yake ya kishenzi? Wenzetu katika lugha nyingine huwa wanaita Parole.

Tunamkomoa Nyosso kwa kumfungia miaka miwili mpaka atimize yote, lakini kumbe tungeweza kumrudisha atoe ushuhuda wa kuyumba kwa maisha yake na kisha ajutie kosa lake kiasi kwamba wanasoka wengine wahuni wangepata fundisho.

Tatizo kubwa la wafungwa wa Tanzania huwa hawana msaada tena kwa jamii. Iwe wafungwa wa makosa ya jinai au wafungwa wa vifungo vya nje kama hawa wa soka. Wanaisaidia vipi jamii baada ya kutoka vifungoni?

Nadhani huu ni wakati sahihi wa TFF kukaa chini na Nyosso na kupima kama anajutia kosa lake, kama amebadilika, kama anahitaji kuwa balozi wao dhidi ya wachezaji wenye tabia za kihuni ambao wamejaa katika soka letu.

Kwa hulka za Nyosso nadhani hajaweza kuomba msamaha hadi sasa kwa sababu najua ni mtu ambaye hajui aanzie wapi hata kama anajutia makosa yake.

Na kwa mchezaji wa aina yake aliyetokea mtaani nadhani hata washauri wake watakuwa si watu wenye busara.

Kwa mtazamo wangu, mwaka mmoja nje ya uwanja unamtosha sana Nyosso, sasa angeweza kurudishwa uwanjani.

Kwa wakati ule inawezekana kumfungia miaka miwili lilikuwa jambo sahihi kiasi cha kuweza kumuumiza kisaikolojia, lakini ilipofika Nyosso anaweza kurudi uwanjani na kucheza bila ya matatizo. Alichokipata nje ya uwanja kimemtosha.

Wenzetu huwa wanamfungia mchezaji kwa idadi ya mechi na si miezi. Bado hasara inakuwa kubwa kwa mchezaji na lengo linatimia. Hapana shaka kwa Nyosso lengo limeshatimia na kama halijatimia basi labda tulikuwa na dhumuni la kumfungia asicheze soka kwa maisha yake yote.

Kwa mtazamo mwingine tunaweza kusema hizi ni adhabu za kukomoana au kuna watu walipanga kwamba Nyosso asicheze tena soka katika maisha yake.

Kama si dirisha hili, Nyosso anaweza kurudishwa katika dirisha dogo lijalo la uhamisho na kisha akacheza chini ya uangalizi maalumu.

Januri 1995, FA ya England ilimfungia kwa miezi minane staa wa zamani wa Manchester United, Eric Cantona kwa kosa la kumpiga teke la Kung-Fu shabiki wa Crystal Palace, Matthew Simmons, ambaye alikuwa akimtukana nje ya uwanja.

Sitaki kupima kosa la Nyosso na kosa la Cantona, lakini hapo hapo Cantona alipewa adhabu ya kwenda mitaani kuwafundisha watoto soka. Ina maana pamoja na ujinga wake, lakini kipaji chake kinahitajika hata anapokuwa amefungiwa.

Pengine ndicho kitu ambacho tunapaswa kukifanya kwa sasa. Kama tunajaribu kuiga mambo ya Ulaya, basi kuna mambo mengine mazuri kama haya ambayo tunapaswa kuyaiga.

Tusiendeshwe na hisia kali kwa muda mrefu huku tunatokomeza vipawa vya wanasoka wetu. Nyosso angeweza kuwa mwalimu wa mabeki wa kati pale viwanja vya Karume wakati akitumikia adhabu yake fupi. Tuwe wavumilivu na walimu wazuri wa kutoa adhabu pale wachezaji wetu wanapokosea ili tusiwapoteze, labda kama wanataka kupotea wenyewe.