UTATA: Tumemlaumu Saanya sasa imetosha, tuhamie kwa mabeki wa Simba na polisi

Muktasari:

  • Ilibidi mwamuzi wa mchezo huo, Omary Abdulkadir kuusimamisha mchezo mpaka Rais Mwinyi alipoondolewa uwanjani kwa ulinzi mkali. Kwa hiyo mechi ilimalizika bila mgeni rasmi kuwepo uwanjani.

NI miaka 14 imepita tangu mashabiki wa Yanga wavunje viti katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru), baada ya Madaraka Selemani wa Simba kufunga bao tata.

Nakumbuka siku hiyo ilikuwa Jumapili, Madaraka aligeuka pamoja na mpira, ukamgonga katika mkono wake jambo ambalo lilimpa nafasi nzuri ya kuuweka vizuri mguuni mwake na kufunga bao la pili katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Yanga.

Fainali hiyo ya Kombe la Tusker nusura ivurugike, kwa sababu mashabiki wa Yanga hawakukubali, walianza kuvunja viti na kuvirusha Jukwaa la VIP alipokuwa amekaa mgeni rasmi, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi.

Ilibidi mwamuzi wa mchezo huo, Omary Abdulkadir kuusimamisha mchezo mpaka Rais Mwinyi alipoondolewa uwanjani kwa ulinzi mkali. Kwa hiyo mechi ilimalizika bila mgeni rasmi kuwepo uwanjani.

Nilikuwa nimetumwa na ofisi kwenda kuripoti mechi hiyo. Ilikuwa hali mbaya, hasa ikizingatiwa kuwa Uwanja wa Uhuru wakati huo ukiitwa Uwanja wa Taifa ulikuwa mdogo na watu walijaa kupita kiasi.

Hata hivyo, niliwapongeza polisi wakati huo ni jinsi walivyoshughulikia tatizo hilo kistaarabu kiasi kwamba hakukuwa na maafa na watu waliondoka salama uwanjani.

Ni miaka 14 imepita tangu tukio hilo, lakini Amissi Tambwe ameturudisha nyuma baada ya kuushika mpira na baadaye kuuweka sawa kabla ya kufunga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba mwishoni mwa wiki.

Sitakuwa miongoni mwa watu wanaomlaumu mwamuzi Martin Saanya kwa kutoona mkono wa Tambwe, ila kama nitalazimishwa kumlaumu mwamuzi huyo ni kwa sababu kwa jumla mchezo ulikuwa mkubwa kwake kuliko uwezo wake.

Kwa matukio yote ambayo yanalalamikiwa kuanzia bao la Ajib Ibrahim mpaka mkono wa Tambwe, huwezi kumlaumu Saanya bila kuwataja waamuzi wasaidzi wake Ferdinand Chacha na Samweli Mpenzu.

Lakini nao huwezi kuwalaumu, kwa sababu kuna mambo mawili; kwanza matukio hayo yalikuwa ya kasi sana na watu wengine wameyaona vizuri kwenye marudio ya televisheni, pili ni kwamba viwango vya waamuzi wote nchini vipo chini.

Bado nasimamia ninachokiandika hapa kila mara kuwa makosa ya waamuzi, lakini yale ya kibinadamu tu ndio yanaufanya mchezo unoge na kuzua mjadala mkubwa, vinginevyo mjadala huu wote usingekuwapo na kusingekuwa na maana ya mchezo wenyewe.

Hata hivyo, kuna mambo mengi ambayo niliyaona hayakwenda sawa katika mchezo huo, na nitayaweka kwa ufupi sana.

1.Mwamuzi ametoka kifungoni

Saanya alitumikia adhabu ya mwaka moja kutokana na kuboronga mechi kati ya Yanga na Coastal Union.

Saanya na mwamuzi msaidizi Jesse Erasmo waliochezesha mechi kati ya Yanga na Coastal Union  walifungiwa mwaka mmoja kila mmoja kwa kutoimudu mechi hiyo Septemba mwaka juzi.

Bila kuangalia makosa aliyoyafanya katika mechi ya watani mwishoni mwa wiki, bado hakustahili kuchezesha mchezo huu kwa sababu mechi ilikuwa kubwa kwake na hasa kwa mtu ambaye amekuwa nje kwa muda mrefu. Kutoona mkono wa Tambwe si tatizo kwangu, kwa sababu tumeyaona mabao ya aina hiyo mengi tu tena kwa waamuzi wa kimataifa, ndio maana siwezi kumlaumu mwamuzi kwa kosa hilo, ila nitailamumu TFF kwa kumpanga mwamuzi aliyefungiwa mwaka mzima kwa kuwa chini ya kiwango.

Suala la kutoona mkono wa Tambwe, si tatizo kwangu, hata beki wa Arsenal, Laurent Koscielny amefunga bao la mkono dhidi ya Burnley juzi Jumapili, lakini mwamuzi Craig Pawson hakuona.

2.Bao la Ajib

Nilikuwepo uwanjani, tena nikiwa nimekaa sehemu nzuri kabisa. Kwa haraka na mimi niliamini kuwa Ajib alikuwa ameotea, lakini baada ya kuangalia marudio ya mechi hiyo usiku, nikagundua hakuwa ameotea. Na ndio maana hata wachezaji wa Simba hawakulalamikia uamuzi wa Saanya kulikataa bao hilo kwa sababu nao waliamini kuwa Ajib alikuwa ameotea. Mwamuzi msaidizi wa pembeni Ferdinand Chacha alishindwa kumsaidia Saanya katika hili. Lilikuwa ni tukio la haraka, kwa sababu mabeki wa Yanga walihama haraka mpira ulivyopigwa.

3.Kosa kubwa la Simba

Simba walianza mchezo taratibu sana. Nilikuwa nazungumza na jirani yangu uwanjani hapo na kumwambia ‘Simba wanaonekana kuchoka, sijui nini kimewatokea.’ Walicheza taratibu na kwa hofu, inawezekana kwa sababu Yanga walipiga sana viatu dakika za mwanzo. Jambo hilo liliwafanya Yanga wafurahie, kwa sababu huwa wanasumbuliwa sana na timu ambazo zinacheza pasi halafu kwa kasi. Lakini dakika 20 za mwanzo, Yanga walionekana kutawala licha ya Simba kuwa na nahodha wake, Jonas Mkude uwanjani.

4.Yanga walikosea zaidi

Wakati Mkude amepewa kadi nyekundu dakika ya 26, wachezaji wa Simba walichanganyikiwa, walikubali kipigo, lakini Yanga wakashindwa kutumia mwanya huo kupeleka mashambulizi mengi langoni mwa Simba. Ilifika kipindi ikaonekana kabisa kuwa Simba walikuwa wanataka mapumziko yafike haraka ili wakajipange upya. Yanga wakafanya uzembe wa mwaka, wakakubali kwenda mapumziko wakiwa wanaongoza bao 1-0 tu. Waliporudi kipindi cha pili, Yanga walirudi na fomesheni ile ile, wakati Simba walibadilika na kujiamini zaidi huku wakiwa wamejipanga upya.

5.Polisi na mabomu yao

Hakukuwa na haja ya polisi kurusha mabomu katika umati kama ule, kwa kufanya vile polisi walisababisha vurugu kubwa zaidi, kuna watu walikanyagana, wengine walizimia kwa hofu, wengine wakataka kugongwa na magari nje ya uwanja wakikimbia. Ilikuwa hatari kubwa. Sitaki kuingilia kazi ya polisi, lakini haikuwa busara kutumia nguvu kubwa kiasi kile. Huwa tunaona wenzetu wa nje, polisi huwa wanapanda huko huko majukwaani kutuliza mashabiki bila hata kufyatua mabomu ya machozi. Kama yangetokea maafa, polisi wangekuwa chanzo.

6.Simba ilaumu mabeki wake

Simba wanamlaumu mwamuzi Saanya kutokana na bao la Tambwe. Kuna swali la kujiuliza, hivi anayepaswa kulaumiwa ni mwamuzi au mabeki wa kati wa Simba, Method Mwanjali na Novatus Lufunga? Kwa ujumla walishindwa kumdhibiti Tambwe katika mchezo huo. Tena angewafunga mapema kabisa kama si shuti lake kutoka nje ya lango.

7.Mashabiki wa Yanga bwana!

Siku zote, mashabiki wa Yanga huwa hawataki Simon Msuva acheze mechi dhidi ya Simba. Wamemsingizia tuhuma zote unazozijua kuhusu Simba. Lakini katika mchezo huo baada ya kipindi cha pili, mashabiki hao walianza kupiga kelele wakitaka kocha amuingize Msuva. Nilibaki nimeduwaa tu na kuwashangaa mashabiki hawa kuwa vigeugeu.

Suluhisho

Kwa jumla mchezo huo haukuwa mzuri, kutokana na timu zote kushindwa kuonyesha kuwa ni timu kongwe. Mpira haukuvutia na hakukuwa na ufundi.

Yanga wanapaswa kujilaumu zaidi kwa sababu baada ya kufunga bao la Tambwe walianza kujihami na kuwaacha Simba wapate nguvu kipindi cha pili.

Inashangaza kuwa Yanga wanadaiwa mabao 5-0 waliyofungwa miaka mitatu iliyopita, nafasi kama hizo wanapaswa kutumia ili kulipa kisasi, lakini wanachezea bahati.