Tuiunge mkono Serengeti Boys iende Madagascar

WADAU wa soka nchini wakiwamo mashabiki kwa sasa hawana wanachokiwaza zaidi ya ufunguzi wa mechi za Ligi Kuu Bara msimu mpya wa 2016-2017 inayoanza kesho Jumamosi.

Mashabiki na wadau wengine wana hamu ya kutaka kuona timu wanazoshabikia nchini katika ligi hiyo zitafanya nini baada ya kufanya maandalizi ya kutosha ikiwamo kusajili na kuvifua vikosi vyao tangu msimu uliopita ulipomalizika.

Ligi hiyo licha ya kuwa na dosari kadha wa kadha, lakini bado ina mvuto mkubwa kwa mashabiki wake wanaoifuatilia hatua kwa hatua.

Kinachosisimua zaidi ni kwamba ligi hiyo ya Viodacom maarufu kama VPL, inaanza ikiwa imepita wiki moja tu tangu kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya England, iliyoanza rasmi wikiendi iliyopita.

Ligi ya England maarufu kama EPL ni moja ya ligi zenye mvuto kwa mashabiki wa soka nchini na duniani kwa jumla, imekuwa ikifuatiliwa kwa ukaribu na kuwatia watu hamasa kubwa ya kutaka kujua kila kinachoendelea.

Ukichanganya na kuanza kwa msimu mpya wa VPL, ni wazi mashabiki vichwani mwao kwa sasa hakuna wanachokiwaza ila ligi hizo mbili pamoja na nyingine zilizoanza kutimua vumbi lake barani Ulaya.

Hata hivyo, kuna jambo ambalo Mwanaspoti linapenda kuwakumbusha mashabiki na wadau wa soka kwa jumla kuwa, wakati akili, macho na masikio yakielekezwa kwenye VPL na EPL, pia kuna Serengeti Boys.

Timu ya Taifa ya Vijana U17 ambayo wikiendi hii itashuka uwanjani kumalizana na Afrika Kusini.

Timu hiyo ndiyo wawakilishi pekee ambao wamekuwa wakiipeperusha vyema Bendera ya Tanzania kimataifa kutokana na kufanya vizuri katika mechi zake.

Katika mchezo wa kwanza dhidi ya wapinzani wao kuwania kucheza fainali za Afrika kwa Vijana 2017 zitakazofanyika Madagascar, timu hiyo ililazimisha sare ya bao 1-1 ugenini, hivyo kuhitaji angalau sare isiyo na mabao ili isonge mbele.

Kuna haja ya kuunganisha nguvu ya pamoja na kuiunga mkono timu hiyo, ili iweze kukamilisha ndoto zao za kutinga raundi ya tatu kabla ya kukata tiketi ya kwenda Madagascar mwakani.

Tusiweke akili zetu katika ufunguzi wa VPL tu ama kufuatilia EPL, tukawasahau vijana wetu ambao wanapambana kwa manufaa ya taifa letu.

Tanzania haijawahi kucheza fainali kama hizo tangu tuanze kushiriki. Mwaka 2004 tulifuzu, lakini udanganyifu uliofanyika na usaliti uliofanywa na baadhi ya wadau wachache uliifanya Serengeti Boys inyang’anywe haki yake baada ya kufuzu.

Mwanaspoti linaamini kuna ulazima wa kila mdau wa soka kujitolea kwa hali na mali kuiunga mkono timu hii ya vijana ili iweze kushinda mchezo wao wa Jumapili ili itinge raundi inaofuata ambapo itacheza ama na Namibia ama Kongo.

Kuwaunga mkono siyo tu kuonyesha kuwajali na kuwathamini, pia ni njia nzuri ya kusaidia kuongeza morali ya wachezaji wa timu hiyo katika kuisaka tiketi ya kwenda Madagascar kitu ambacho ni fahari kwa kila Mtanzania.

Tuwe bega kwa bega ili kuona Serengeti Boys inafanya kweli na kusonga mbele kutoka raundi ya kwanza kwa kutumia faida ya uwanja wa nyumbani tukiamini kuwa hilo linawezekana kama tutazingatia msemo wa Umoja ni nguvu.

Ikumbukwe kufuzu na kufanya vizuri kwa Serengeti Boys ni hatua nyingine ya kufanya vizuri kwa timu yetu ya Taifa ya Tanzania ‘ Taifa Stars.’

Kama tutawasapoti Serengeti Boys, wachezaji wake ndio watakaoweza kulitangaza zaidi jina la Tanzania katika mipaka ya nchi yetu  na hata baadaye kununuliwa na kwenda kusakataka soka la kulipwa nje ya nchi.