Tuchangie kwa moyo wote timu ya Serengeti Boys

Monday February 13 2017

Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (CCM),

Mbunge wa Tabora Kaskazini, Almas Maige (CCM), akikabidhi sehemu ya mchango wake wa Sh 800,000 kwa nahodha wa timu ya taifa ya vijana, Serengeti Boys, Issa Makamba, nje ya viwanja vya Bunge mjini Dodoma walipotembea Bunge. Wabunge wamejitolea posho za kikao cha siku moja kuichangia timu hiyo inayoshiriki fainali za vijana 2017 baadaye nchini Gabon. Wa pili kulia ni Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF) Jamal Malinzi. Picha| Emmanuel Herman 

KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys kinajiandaa na ushiriki wake wa michuano ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika Kwa Vijana U17 zitakazofanyika Mei, Gabon.

Tanzania imepata bahati hiyo baada ya kushinda rufani yake dhidi ya Congo Brazzaville na Serengeti Boys itashiriki fainali hizo zitakazoanza Mei 21 mpaka Juni 4 ikiwa ni kwa mara ya kwanza.

Tayari maandalizi kuelekea kwenye fainali hizo yameanza na katikati ya wiki iliyopita kikosi hicho kilialikwa bungeni mjini Dodoma kwa ajili ya kupongezwa na kuchangiwa kiasi fulani cha fedha na wabunge wa Jamhuri.

Kabla ya kwenda Dodoma, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alifichua kuwa, gharama kwa ajili ya timu hiyo yakiwamo maandalizi ya mechi za kirafiki ndani na nje ya nchi na mpaka safari yake ya kwenda Gabon si chini ya Sh 1 bilioni. Hizo ni fedha nyingi kwelikweli hata kuzitamka. Malinzi alinukuliwa kuwa kwa muda wote wa ushiriki wa timu hiyo katika mechi zake za kuwania kufuzu fainali hizo na maandalizi yake kwa ujumla waliubeba mzigo wenyewe na kila mtu analifahamu hilo.

Haikuwahi kusikika sio kwa serikali ama wanasiasa na watu wengine kujitosa kuisaidia timu hiyo, zaidi ya Malinzi na TFF yake kuachiwa jukumu hilo na hata walipoikatia rufani Congo, kadhalika waliachwa peke yao.

Bahati nzuri timu imepata nafasi hiyo ya kwenda Gabon, sasa ni wajibu wa kila Mtanzania kwa nafasi yake kuichangia kwa hali na mali Serengeti Boys ili kuwa na nguvu katika maandalizi yake na kwenda kufanya mambo makubwa Gabon.

Zipo taarifa kwamba baadhi ya wabunge walioipokea timu hiyo bungeni ndio waliokubali kuichangia kwa kujitolea posho yao ya siku moja, huku wengine wakichomoa, lakini ukweli ni kwamba Serengeti inahitaji michango yetu sote.

Tunapaswa kushirikiana kuichangia kwa hali na mali ili kuhakikisha inakuwa na maandalizi mazuri kabla ya kwenda kushiriki fainali hizo za Gabon. Tuiunge mkono TFF katika mipango mkakati wake ambao imekuwa ikiifanya tangu awali katika ushiriki wa timu hiyo na hata sasa wakiiweka kwa ajili ya Serengeti kuelekea Gabon, ikiwamo kutaka kuiweka kambi ya mwezi mzima ughaibuni.

Tuwe wepesi wa kushiriki maandalizi ya timu hiyo, ili tuje kuwa washiriki wa mapokezi ya kishujaa pale itakapofanikiwa kufanya vema kwenye michuano hiyo ambayo itatoa pia timu nne za Afrika za kucheza fainali za dunia za Vijana.

Mara nyingi wadau wa michezo hasa wanasiasa na viongozi wamekuwa wepesi wa kujitokeza kifua mbele kujisifu na kufanya mbwembwe nyingine timu zikirudi na mafanikio, ila huwa wagumu kubeba mzigo wa gharama awali.

Ndio maana Mwanaspoti linawakumbusha wadau wote wa michezo kuwa, hii ndio nafasi nzuri ya kuonyesha uzalendo kwa timu yetu ya Serengeti na kuwatia moyo vijana sasa kwa kuwachangia ili wawe na maandalizi mazuri.

Mafanikio yoyote yawe kwa timu na hata kwa jambo lolote halipatikani ila kwa juhudi, maarifa na mipango madhubuti ya maandalizi, hivyo tukiiunga mkono Serengeti sasa kwa hali na mali ni rahisi kutupa furaha mwishowe. Hivyo, shime Watanzania hasa wanamichezo tushirikiane pamoja kuwapa nguvu vijana hawa.