NINACHOKIAMINI: Tambwe ametuonyesha uwezo wetu wa kufikiri unapoishia

WATANZANIA bwana utawapenda tu. Hawana haraka wala hawapendi presha wanapofanya mambo yao.

Wanapenda kujadili mambo yao kwenye mitandao ya kijamii. Wanafurahia kuweka siri za familia zao kwenye mitandao ya kijamii. Hakuna siri tena siku hizi.

Mtu akiwa na familia yake kwenye ufukwe wa bahari, anataka sisi wote tujue na ndio maana anaweka picha kwenye mitandao ya kijamii ili kila mmoja aone.

Mijadala kwenye mitandao ya kijamii, ni masimango, kusingiziana, kutuhumiana, kukashifiana, ushabiki na ujuaji. Kila mmoja anajiona ana akili kumzidi mwingine.

Mijadala mizito haitakiwi siku hizi na ndio maana utakutana na mijadala ya kujadili mambo ya kiwango cha chini kwa kiwango cha chini kama kwamba akili zetu zipo chini.

Inaingia siku ya kumi tangu Amissi Tambwe afunge bao tata kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kila mmoja anakubali kuwa kabla ya kufunga bao, Tambwe alikuwa ameushika mpira lakini mwamuzi Martin Saanya hakuona tukio hilo.

Saanya si wa kwanza kukosea, tumeona matukio mengi ya wachezaji kufunga mabao kwa mkono kabisa, lakini yakabaki kuwa hivyo kwa sababu mwamuzi hakuona.

Tatizo letu limebaki kama lilivyo, Watanzania tunapenda kulalamika, na hasa vitu vyenyewe vikiwa vidogo vidogo.

Kwenye mitandao ya kijamii, Saanya katukanwa matusi yote, waamuzi wasaidizi wa pembeni nao wametukanwa matusi yote na Tambwe mwenyewe katukanwa.

Mjadala wa siku kumi zote umekuwa ni bao la Tambwe, watu hawataki kusikia wala kuambiwa, wamebaki na mjadala wa Tambwe tu kana kwamba hakuna jambo lolote la msingi lililokuwepo katika mechi hiyo ya watani wa jadi.

Hakuna anayetaka kujadili kwa kina Serikali kuzifukuza Simba na Yanga katika Uwanja wa Taifa. Hakuna anayetaka mjadala huo, wala hakuna anayeuliza hizi klabu zitakwenda wapi?

Hakuna anayetaka kujua kuwa mashabiki waliovunja viti Uwanja wa Taifa ndio walewale ambao huingia mechi za Taifa Stars, je wataruhusiwa kuingia kwenye mechi za timu ya taifa au itakuwaje?

Hakuna anayetaka kujadili mkataba wa Yanga kukodiwa miaka kumi. Hakuna anayejiuliza kwanini mambo yamekwenda kimyakimya. Kwanini hakukuwa na hafla yoyote ya kusaini jambo kubwa kama hilo.

Watu hawataki mambo makubwa, wanataka bao la Tambwe tu, wanatamani Tambwe afukuzwe nchini au afungiwe kwa sababu ya masuala ya kawaida kabisa ya uwanjani.

Inawezekana Tambwe hakufanya jambo la kiungwana (fair play), lakini anapaswa kusifiwa kwa kupigana na hata kuhakikisha timu yake inapata bao. Ningekuwa na timu, Tambwe angekuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa.

Mjadala wa Tambwe umetufanya Watanzania tujuane vizuri uwezo wetu, ushabiki wetu na hata mihemko yetu.

Tuanze kujadili kwanini Uganda imefuzu kwenye fainali za Mataifa ya Afrika. Huyu Tambwe tumuache kidogo, tujadili mambo makubwa sasa.

Ni wakati sasa angalau tuanze kujadili mambo makubwa ambayo yatafanya soka letu kupiga hatua. Tujadili kwanini hatuna waamuzi katika mechi za Mataifa ya Afrika au Kombe la Dunia.

Kwanini hatuna mchezaji yeyote wa Tanzania anayecheza Ligi Kuu England, kwanini TFF inahitaji mabadiliko makubwa. Hiyo ndiyo iwe mijadala sasa.