Takukuru tengueni hiki kitandaliwi cha FDL

Muktasari:

  • Geita iliingia kwenye tuhuma kutokana na kuishinda Kanembwa mabao 8-0

UMEKARIBIA nusu mwaka sasa tangu Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) ilipotangaza kuanza kufanyia uchunguzi sakata la upangaji matokeo ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu uliopita kwa kundi C. Katika sakata hilo klabu nne za Geita Gold Sports, Polisi Tabora, Oljoro JKT na JKT Kanembwa zilituhumiwa kupanga matokeo ya mechi zao za mwisho za kundi hilo ambazo ziliipa nafasi Geita kupanda Ligi Kuu kabla ya kutenguliwa kwa ubingwa wake.

Geita iliingia kwenye tuhuma kutokana na kuishinda Kanembwa mabao 8-0 wakati Polisi Tabora liyokuwa ikichuana na Geita kupanda Ligi Kuu msimu huu nayo ikitoa kipigo cha mabao 7-0 kwa Oljoro JKT waliokuwa nafasi ya tatu katika kundi hilo. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Rais wake, Jamal Malinzi na Kamati zake zilitengua matokeo hayo kabla ya kuja kutoa hukumu kwa waliotuhumiwa kushiriki na hila hizo wakiwamo viongozi wa vyama vya soka, klabu, wachezaji na waamuzi.

Timu zote nne ziliadhibiwa kwa kushushwa daraja, ambapo Geita, Polisi na Oljoro zilishushwa kwenda Ligi Daraja la Pili (SDL) na Kanembwa kucheza Ligi ya Mabingwa Mkoa (RCL).

Viongozi, wachezaji na waamuzi wapo waliopewa vifungo vya kuanzia miaka 10 mpaka maisha na kutozwa faini mpaka Sh10 milioni kulingana na walivyonaswa na hatia za sakata hilo.

Baada ya hukumu hiyo kuliibuka maneno mengi na tuhuma kuelekezwa kwa viongozi wa TFF kabla ya Takukuru kuingilia kati Aprili mwaka huu kwa kutangaza kufanya uchunguzi wake ili kubaini ukweli wa jambo hilo na tuhuma dhidi ya mabosi wa TFF.

Hata hivyo, ni muda sasa umepita huku, ofisi ya Takukuru ikiendelea kuwataka wadau wa soka na Watanzania kwa jumla wavute subira kwani walikuwa wakiendelea na uchunguzi wao na majuzi wamefichua kuwa tayari wameshakamilisha uchunguzi wao na kilichobaki kwa sasa ni kuweka mambo hadharani.

Hata hivyo, wakati Takukuru ikisuasua kutangaza uchunguzi wake, baadhi ya watuhumiwa walioadhibiwa walikata rufaa kupinga maamuzi yao, wapo waliojikuta wakitolewa kifungoni kama ilivyomkuta kipa wa Geita, Richard Dennis aliyepo Simba. Huku rufaa za wengine zikitiwa kapuni na tayari baadhi yao wameendelea kulalamika na kutoa ufafanuzi na siri juu ya vigogo wa TFF, ambao tofauti na wenzao walioamua kung’oka mara baada ya kunyooshewa vidole, wenyewe wamesalia madarakani mpaka sasa.

Kibaya zaidi ni kwamba miezi hiyo sita ya ukimya, tayari Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea na timu ya Mbao iliyochukua nafasi ya Geita katika kundi hilo kupanda Ligi Kuu inaendelea kucheza na hakuna anayejua kipi kitatokea mbele ya safari. Hivyo Mwanaspoti bila kutoa shinikizo au kutaka kuifundisha kazi Takukuru tulikuwa tunadhani ni wakati mwafaka wa kututengulia kitendawili hiki ambacho kimekuwa kikisumbua wadau wengi wa soka kuhusu ukweli wa tuhuma zilizopo.

Ni vyema jambo hilo likatolewa mapema kama kweli limeshakamilika ili kuwaweka huru wale wanaotuhumiwa kujihusisha na kadhia hiyo ama kama watakuwa na makosa basi wabebe stahiki yao na wale waliodhulumiwa wapewe haki yao.

Inawezekana ni kweli uchunguzi ulistahili kuchukua muda mrefu kutokana na ukweli wa suala lenyewe, lakini kwa vile Takukuru imetuthibitishia kuwa jambo hilo limeiva, ni kiu ya wengi kuona kila kitu kinawekwa wazi mapema kujua ukweli ulivyo. Utolewaji wa ripoti ya uchunguzi wa jambo hilo utakata mzizi wa fitina na kuzika shutuma zinazoendelea kutolewa baina ya walioadhibiwa dhidi ya mamlaka ya soka nchini, kwani ukisikiliza matamshi yao ni kama kuna siri nzito nyuma ya sakata hilo.

Ndiyo maana Mwanaspoti inasisitiza na kutoa rai kwa ofisi ya Takukuru kuliweka jambo hili hadharani, ili chuya na mchele juu ya sakata hilo la upangaji matokeo katika FDL limalizike na kufanya mambo mengine yaendelea katika soka la Tanzania.

Hizi kelele zinazoendelea kutolewa na watu kunyoosheana vidole, vinawachanganya wengi hivyo Takukuru ikiweka mambo hadharani itafahamika nini kimefanyika katika sakata hilo. Tunaamini tuhuma zinazoendelea kutolewa na hata kwa wale walioadhibiwa katika sakata hilo wanaumizwa na mambo yanayoendelea kwa vile sio tu zinachafua taswira zao mbele ya jamii na wadau wa soka kwa jumla, pia zinaondolea uaminifu.

Hivyo mambo yakiwekwa hadharani itafahamika nani mkweli na yupi aliyestahili kubeba msalaba katika sakata hilo na wenye haki zao watazipata ama kuzitafuta mbele ya safari katika vyombo vingine vyenye mamlaka kisheria.