Taji la ubingwa wa Kili Queens liwe fundisho

Muktasari:

  • Picha mbalimbali zimekuwa zikitumwa zikionyesha viongozi na wanasiasa hao wakijivunia timu hiyo kwa mafanikio makubwa waliyopata kupitia michuano hiyo ya Chalenji iliyorejeshwa tena baada ya kupita miaka 30 tangu ilipoasisiwa mwaka 1986.

KILIMANJARO Queens, timu ya soka ya wanawake ya Tanzania Bara Jumanne wiki hii iliweka rekodi ya kunyakua ubingwa wa michuano ya Kombe la Chalenji katika ardhi ya ugenini nchini Uganda kwa kuifunga Kenya Starlet kwa mabao 2-1.

Tangu wanyakue taji hilo mjini Jinja, kila kona ya nchi watu wanaiimba timu hiyo na wanasiasana viongozi wa serikali wanachomoka walipo kuipongeza timu hiyo na kuitumia kujiongezea sifa mbele ya wananchi na wadau wa soka kwa ujumla.

Picha mbalimbali zimekuwa zikitumwa zikionyesha viongozi na wanasiasa hao wakijivunia timu hiyo kwa mafanikio makubwa waliyopata kupitia michuano hiyo ya Chalenji iliyorejeshwa tena baada ya kupita miaka 30 tangu ilipoasisiwa mwaka 1986.

Hata viongozi wa soka ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kama ilivyo kwa wanasiasa hao wengine nao wametumia taji la Kili Queens kama mtaji wa kutembea kifua mbele kwa kujisifu kwa mafanikio hayo.

Sio vibaya, ila tunajiuliza watu hao wanaojitokeza sasa na kuipongeza timu hiyo, huku wakionyesha mapenzi makubwa kwa vijana wetu hao wa kike kwa kuwatafutia usafiri wa ndege na kuwaandalia hafla zenye hadhi walikuwa wapi wakati timu hiyo ilipokuwa ikielekea Uganda kwenye mashindano?

Hakuna asiyejua Kili Queens ilienda Uganda kama yatima na kuchukuliwa kama timu ya kawaida sana. Ilisafiri kwa basi kwa kilomita nyingi kutoka jijini Dar es Salaam hadi mjini Bukoba mkoani Kagera kisha kuelekea Uganda kuchuana na wenzao.

Hakuna aliyekuwa akiitazamia kama wawakilishi wa nchi na kupewa maandalizi na stahiki sahihi kama timu ya taifa, zaidi tu ya kukabidhia bendera kwa mbwembwe vitu ambavyo vimekuwa vya kawaida katika uwakilishi wa nchi kila uchao.

Nani aliyeguswa na watoto hao wa kike kusafiri kwa basi na kuwapa wakati mgumu wakati kumbe watu walikuwa na uwezo wa kuikodia ndege na kuisafirisha hadi Uganda kama ilivyofanyiwa Starlet ya Kenya?

Wanasiasa na viongozi wa serikali na wale wa TFF hawakujua kama Kili Queens ilikuwa ikienda kupeperusha bendera ya Tanzania na walistahili kuipa heshima zaidi ya kuwakabidhi bendera tu.

Lakini leo baada ya wawakilishi wetu hao kutaka kuwaonyesha waliowapuuzia kuwa, wao wanaweza hata katika mazingira magumu, wanasiasa na viongozi wapenda sifa wamejitokeza bila aibu na kujipiga kifua kutaka kuficha udhaifu wao.

Inawezekana wengi waliichukulia poa timu hiyo, bila kujua kuwa madada zetu walijivika uzalendo na kupamabana mwanzo hadi mwisho kuhakikisha wanaitoa kimasomaso Tanzania hata kama hawakuangaliwa kwa jicho pana hapo awali.

Ni wazi taji la Kili Queens mbali na kuwaumbua wengi, lakini linatoa somo kubwa kwa viongozi wa michezo, serikali na wanasiasa kuwa, kama walivyo wepesi sasa kujitokeza, wanapaswa kufanya hivyo kwenye maandalizi ya timu zetu kuzitia moyo.

Watu wasisubiri mafanikio yatokee ndio wajitokeze, kilichofanyika kwa Kili Queens ni kama kisa cha watu waliokacha kulima mashamba, ila wenzao walioamua kuyalima na kuyapalilia na kuzalisha mazao, kisha huwa wa kwanza kutaka kuvuna na kusifia jinsi mashamba hayo yalivyo na rutuba, ilihali walikwepa majukumu yao awali.  Ili mtu au kiongozi ujiite mzalendo ni lazima awe tayari kupambana kwa ajili ya kufanikisha suala fulani mpaka mwisho na kuwa tayari kupokea mazuri au mabaya ya jambo alilopanda shambani kwake. Sio kungoja mazuri wakati hujashughulika tangu awali. Ya Kilimanjaro Queen yawe funzo kubwa.