Taifa Stars inakwamishwa na mengi, sio Mkwasa

MASHABIKI wa soka nchini wameendelea kulia na kipigo cha aibu cha mabao 3-0 kilichopata timu yao ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Zimbabwe.

Stars iliifuata Zimbabwe mjini Harare wiki iliyopita katika pambano la kirafiki la kimataifa na kuangukiwa na dhahama hiyo, huku wadau wa soka wakimnyooshea kidole Kocha Mkuu wa timu hiyo, Boniface Mkwasa.

Wengi wao wanaona kama Mkwasa amefikia mwisho wa uwezo wake kuinoa timu hiyo. Hali kama hiyo iliwahi pia kumkumba Mbrazil Marcio Maximo, Jan Poulsen, Kim Poulsen na Mart Nooij aliyekaribia kuambulia kipigo mjini Zanzibar.

Ni kweli kufanya vibaya kwa Stars kunaumiza mioyo ya mashabiki, hata Kocha Mkwasa hafurahii hali hii.

Kama Kocha angependa kuona anafanya vyema akiwa na timu hiyo na kuipa mafanikio makubwa kufunika rekodi za makocha wa kigeni. Angependa kuona Stars inafuzu fainali za Afrika kuanzia Chan mpaka Afcon. Mkwasa kama kocha alikuwa na hamu kubwa ya kuipeleka Tanzania kwenye fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018.

Ingekuwa heshima kwake na taifa kwa jumla, lakini hali haikuwa vyema kwa sababu soka siyo kama chumvi ukiitia kwenye maji inayeyuka punde tu na kutoa ladha, mchezo huo una hatua zake katika kufikia mafanikio ya juu.

Cape Verde ambayo kwa sasa inatikisa soka la dunia, haikufika hapo ilipofikia kirahisi, imefanya kazi kubwa kutoka kwenye unyonge hadi kuwa washindani wa kweli. Ndivyo ambavyo Cameroon, Nigeria, Ghana, Misri na mataifa mengine yavyopigana kufika walipofikia. Stars yetu ina matatizo mengi kuliko suala la kocha mkuu, ndiyo maana wamepita makocha kadhaa lakini mafanikio ni haba. Lazima tuanze kujenga msingi imara kwa wachezaji wetu ili waje kuwa wapiganaji wa Stars.

Kama tunafuta michezo shuleni, tunazuia fainali za Umitashumta na Umisseta kwa sababu ya kusaka fedha za madawati, unatarajia tupate wapi vijana wa kuja kuchukua nafasi za kina Mbwana Samatta? Kwa nini Mkwasa pekee anapewa lawama wakati viongozi wa serikali na wanasiasa wanakwamisha maendeleo ya michezo na soka letu kwa ujumla. Tuacheni siasa kwenye mambo ya msingi, tuzalishe na kuendeleza vijana wenye vipaji, tuwatengenezea mazingira ya kuwa nyota wa baadaye iwe katika riadha, soka, netiboli ama mchezo wowote mwingine, uone Tanzania itafika wapi.

Badala ya kujinyooshea vidole, tunamwonea bure Mkwasa, wakati Maximo, Jan, Kim na Nooij hata wao walikwama kufika tulikokuwa tukiota kwa sababu Stars ina matatizo mengi ya msingi kuliko hata suala la kocha mkuu na matokeo yake.