Taifa Stars ina matatizo mengi kuliko badiliko la jezi

Muktasari:

  • Kwa sasa Stars huvaa jezi za rangi ya bluu kwa mechi za nyumbani na nyeupe inapokuwa ugenini na zilishaanza kuzoeleka kwa mashabiki wa soka.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetangaza tenda kwa wabunifu kwa ajili ya kubuni jezi mpya za timu ya taifa, Taifa Stars.

Tangazo hilo limekuja ikiwa imepita muda wa mwaka mmoja na ushei tu, tangu Stars ibuniwe jezi mpya zilizozinduliwa rasmi Juni mwaka jana na zinazoendelea kutumika na timu hiyo kwa mechi za nyumbani na ugenini.

Kwa sasa Stars huvaa jezi za rangi ya bluu kwa mechi za nyumbani na nyeupe inapokuwa ugenini na zilishaanza kuzoeleka kwa mashabiki wa soka.

Hata hivyo wakati tukiwa tumeshindwa kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ndani (Chan), iliyofanyika hapo Rwanda tu, pia tukikwama kwenda Gabon katika Afcon 2017 na fainali za Kombe la Dunia za 2016 kule Russia, TFF limekuja wazo la kubadilisha jezi za Taifa Stars.

Katika taarifa yake TFF imesema inataka kuona Stars ikiwa na muonekano mwingine mpya kwa ajili ya msimu wa  2017-2018 na 2018-2019 na kuwaalika wabunifu kuwasilisha ubunifu wao kabla ya Novemba 30 kuing’arisha Stars.

Mwanaspoti halipingi wazo la TFF la kuipa Stars jezi mpya, lakini kwa yakini kuna mambo mengi ya msingi ambayo yatakiwa kufanywa kwa timu yetu ya taifa, kuliko kuibadilisha jezi kila msimu.

Kuna mantiki gani ya kuipendezesha Stars kimuonekano wakati uwanjani haina matokeo mazuri yanayowafariji mashabiki? Inashangaza na ndio maana tunaikumbusha TFF kuumiza kichwa kufikiria mambo ya muhimu zaidi kwa timu yetu zaidi ya badiliko la jezi.

Tunaweza kubadilisha jezi kila mwezi, lakini kuna faida gani kwa mustakabali wa soka la Tanzania anga la kimataifa kama kila shindano tunalotia mguu tunakuwa wasindikizaji na kutolewa kwa aibu?

TFF ni lazima ijifunze kwa mataifa mengine ambayo yamekuwa yakielekeza nguvu zao kusaka mafanikio kisoka kama ilivyotokea kwa Cape Verde na hata majirani zetu Uganda ambayo wamevunja mwiko wa miaka 38 ya kutocheza Afcon na mwakani wanaenda Gabon!

Hata ndio mambo ambayo Watanzania na mashabiki wa soka wanayataka zaidi kwa timu yao ya taifa ni mafanikio kuliko muonekano wa kibishoo wa jezi, ilihali mataifa mengine yanatuacha nyuma kila mwaka.

Viongozi wa TFF, lazima wachangamshe akili zao ya kutatua mambo mazito yenye tija kwa soka letu, kuliko kufanya mambo kama waliojitoa fahamu. Umefika wakati wajielewe na wasikie kilio cha  Watanzania ambao wanategemea kuona mipango madhubuti na yenye mashiko.