NINACHOKIAMINI : TFF ya Malinzi waishike vizuri kamba hii isikatike

Muktasari:

  • Inawezekana umewahi kufika sehemu ambazo hukuzipenda kabisa, lakini bado kuna jambo fulani uliliona na likakuvutia.
  • Kuna sehemu duniani zina matatizo mengi; kama vita, kukosekana kwa huduma muhimu kama hospitali, barabara, maji na mambo mengine, lakini bado kuna mambo fulani huwa ni mazuri.

KATKA maisha tunapaswa kutambua kuwa hakuna kitu ambacho kinaweza kuwa kibaya moja kwa moja.

Inawezekana umewahi kufika sehemu ambazo hukuzipenda kabisa, lakini bado kuna jambo fulani uliliona na likakuvutia.

Kuna sehemu duniani zina matatizo mengi; kama vita, kukosekana kwa huduma muhimu kama hospitali, barabara, maji na mambo mengine, lakini bado kuna mambo fulani huwa ni mazuri.

Kuna taasisi nyingi zina matatizo yake, lakini bado wafanyakazi wanaendelea kufanya kazi kwa sababu kuna mambo fulani mazuri.

Licha ya matatizo mengi yaliyopo katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), angalau sasa wana sehemu wanaweza kushika na kutamba.

Tunajua kuwa pale TFF kuna matatizo mengi kama kusababisha migogoro, kuleta utengano baina ya wanachama wake na mbaya zaidi ni kukosa dira.

Tangu uongozi wa Jamal Malinzi uingie madarakani, tumeshuhudia mambo kadhaa yakiwa hayajakaa sawa kiasi kwamba mifumo iliyokuwa imewekwa na watangulizi wake imepotea au kama bado ipo imebaki jina tu.

Ni katika kipindi hiki ambacho tumeshuhudia migogoro ya vyama vya soka vya mikoa, wilaya na hata klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara au Daraja la Kwanza.

Migogoro ambayo tumeishuhudia Stand United, Coastal Union na hata uchaguzi wa Yanga pamoja na uchaguzi wa Chama cha Soka cha Wilaya ya Kinondoni (Kifa) ni mambo machache tu ambayo yanaonyesha kuwa mambo mengi hayajakaa sawa.

Hiki ni kipindi ambacho dunia imeshuhudia upangaji wa matokeo wa Ligi Daraja la Kwanza kiasi kwamba timu nne zilijikuta zikipewa adhabu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushushwa daraja.

Matokeo yanapangwa bila wasiwasi kwa sababu viongozi wa klabu hawana hofu na utawala, wanajua kuwa baadhi ya viongozi wa TFF nao wanahusika katika upangaji matokeo kwa namna mmoja au nyingine.

Kwa namna moja au nyingine, TFF imesababisha matatizo mengi katika utawala huu na ndio maana inakuwa rahisi kwa mashabiki kuchoshwa na soka letu.

Lakini kama nilivyoanza, hata sehemu yenye matatizo huwa kuna mambo fulani machache mazuri, na hata TFF kuna jambo ambalo wanaweza kujivunia sasa.

Mafanikio ya timu ya Taifa ya Vijana ya Serengeti yanawafanya TFF angalau kutaka kufunika matatizo yote yaliyopo katika soka letu, lakini wanapaswa kujipanga na kuhakikisha timu hiyo inafuzu.

Baada ya kuifunga jumla ya mabao 9-0 timu ya Shelisheli katika mchezo wa kufuzu wa Mataifa ya Afrika, timu hiyo sasa itakuwa na kibarua cha kuitoa Afrika Kusini katika hatua inayofuata ili kufuzu kwa fainali za Madagascar mwakani.

Hatua waliyofikia ni nzuri hata kama watafungwa na Afrika Kusini bado wanapaswa kupongezwa kwa hatua waliyofikia.

Nakiona kikosi hiki kikiunda Taifa Stars imara kwa ajili ya fainali za Mataifa ya Afrika 2019.

Kama vijana hawa hawatavurugwa na siasa za TFF wanaweza kutufanya tukafuzu fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2019 na hilo linawezekana sana.

Malinzi anajua kuwa salama yake TFF ni kuhakikisha kuwa timu hii ya vijana inafanya vizuri, hivyo hana budi kuishika vizuri isikatike.

Mafanikio ya timu hiyo ndio itakuwa jeuri ya Malinzi miaka ijayo, anaweza kujitetea kwa kuzungumza kitu akaeleweka.